Na John Gagarini, Chalinze
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani kimesema kuwa kitashirikiana na uongozi wa Chuo Cha Kilimo na Mifugo cha Kaole ili kuhakikisha elimu inayotolewa ina kuwa na
manufaa kwa nchi.
Hayo yalisemwa Lugoba wilayani humo na mwenyekiti wa Jumuiya
hiyo Abdul Sharifu wakati wa baraza la Wazazi na kusema kusema kuwa chuo hicho
ambacho kinamilikiwa na jumuiya kitaboreshwa masomo yanayotolewa chuoni hapo
ili wahitimu wake wabadilishe sekta hiyo na kuleta faida kwa wafugaji na
wakulima nchini.
Sharifu alisema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto
mbalimbali ambazo watahakikisha wanaziondoa kwa kushirikiana na makao makuu ya
Jumiya hiyo ili kiweze kutoa elimu bora ambayo itasaidia kuboresha ufugaji na
kuwa wa kisasa na wenye tija.
“Chuo kinakabiliwa na changamoto lakini tutazikabili kadiri
ya uwezo wetu ili tuboreshe elimu inayotolewa chuoni hapo hasa tukizingatia
ufugaji ni moja ya chanzo kikubwa cha pato la Taifa na kilimo kwa ajili ya
chakula,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa chuo hicho kinajijenga upya baada ya awali
kubadilishwa na kuwa shule ya sekondari lakini sasa kimerudishwa mikononi mwao
hivyo watahakikisha kinakuwa moja ya vyuo bora hapa nchini kwa kutoa elimu
inayokubalika.
“Tunaomba wadau mbalimbali kujitokeza kukisaidia chuo chetu
ili kiweze kuboresha wasomi ambao watakubalika kule watakakopangiwa hasa
ikizingatiwa wahitimu hao watakuwa ni maofisa ugani wataboresha kilimo na
ufugaji,” alisema Sharifu.
Kwa upande wake mjumbe wa baraza la jumuiya hiyo Yahaya
Msonde alisema kuwa lengo lao ni kutoa elimu itakayokidhi mahitaji ya wakulima
na wafugaji ili waboreshe shughuli zao.
Msonde alisema kuwa kilimo ni uti wa mgongo hivyo lazima
kiwekewe mikakati ya kuinuliwa kwa kuzalisha wataalamu wenye uweze na mbinu za
kisasa na kwa wafugaji nao waweze kukabiliana na ufugaji usiokuwa na tija.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment