Thursday, June 9, 2016

RC ATAKA MKATABA WA UWEKEZAJI KUPITIWA UPYA

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametaka kupitiwa upya mkataba wa kuuziwa mwekezaji eneo la Magofu ya Chole wilaya ya Mafia mkoani Pwani ambapo kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development Ltd imemilikishwa ambapo eneo hilo kuna gereza walilokuwa wanafungwa watumwa enzi za ukoloni wakati wa Utawala wa Wajerumani.
Aidha ameunda tume ya kufuatilia undani wa mkataba huo na amezuia marekebisho yaliyokuwa yanafanywa na kampuni hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi pale ufumbuzi wa kujua namna mkataba huo ulivyoingiwa baina ya Kijiji cha Chole na mwekezaji huyo kama umezingatia taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chole Mjini kata ya Jibondo kwenye mkutano wa hadhara Ndikilo alisema kuwa mkoa hauna nia mbaya na mwekezaji huyo ambaye amepewa hati miliki ya eneo hilo kwa kipindi cha miaka 33.
Ndikilo alisema kuwa eneo hilo ambalo lina kumbukumbu mbalimbali ambalo liko jirani na Bahari ya Hindi lilikuwa likitumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na soko la Watumwa pamoja na gereza lina ukubwa wa hekta 3.7 ambapo eneo hilo liko chini ya Wizara ya maliasili na Utalii Idara ya Malikale.
“Mkataba huo ambao ulisainiwa mwaka 2007 shamba namba 2031 baina ya mwekezaji  Dk Jean de Villiers na Kijiji hicho ambapo mwenyekiti wa Kijiji hicho Maburuki Sadiki alisaini kwa niaba ya Kijiji na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya wakati ule Manzie Mangochi pasipo kuishirikisha Halmashauri ya wilaya ambayo haipati mapato yoyote kutokana na uwekezaji huo licha ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Kijiji cha Chole” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amemtaka mwekezaji huyo kusimamisha ukarabati na kuunda tume ya kufanya uchunguzi na itatoa majibu baada ya mwezi mmoja ili kujiridhisha na kumilikishwa eneo hilo mtu binafsi eneo la serikali la kihistoria na kujengwa hoteli ya kitalii kwa kukarabati jengo la zamani.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma barua ambayo iliyosainiwa na John Kimaro kwa niaba ya katibu mkuu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuhirikiana na mwekezaji na kusema kuwa sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 na sera ya Malikale ya mwaka 2008 inasema Malikale au Magofu yanaweza kumilikiwa na mtu binafs, taasisi na serikali.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa jukumu la serikali (Idara ya Mambo ya Kale) ni kuhakikisha kuwa mmiliki hatabomoa au kufanya chochote katika magofu hayo kinyume cha sheria.
Akitoa maelezo juu ya umiliki wake mkurugenzi wa Chole Mjini Conservation and Development Company Ltd Anne De Villiers amesema kuwa kampuni hiyo iliingia Mafia na kukuta hali ya majengo hayo ya kale yakiwa kwenye hali mbaya ndipo walianza mchakato wa kuyakarabati.
Dk Villiers alisema kuwa lengo la kuchukua eneo hilo ni kuhakikisha uasili wa mahali hapo haupotei kwa kuyafanyia ukarabati magofu hayo ambapo moja lilibaki ukuta mmoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati huo.
Naye mkuu wa wilaya ya Mafia Dk Nasoro Hamid alisema kuwa serikali haishirikishwi jambo lolote wala haijui ni watalii wangapi wanaoingia hapo wala mapato yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Dk Hamid amesema kuwa Kijiji cha Chole ndicho kiliingia mkataba na mwekezaji huyo ambapo hugawana asilimia kutokana na watalii wanaoingia kwenye eneo hilo la makumbusho lakini tatizo haijulikani kinachopatikana hapo ni kiasi gani katika mgawanyo huo wa mapato.
Awali baadhi ya wanakijiji wakizungumzia suala hilo wakiongozwa na Ally Sikubali na Hemed Ally walisema kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo ni mkataba Kiswahili unasema kuwa endapo kutakuwa na kutoeleweka mkataba wa Kiingereza ndiyo utakaotumika.
Waliomba mkataba huo uangaliwe upya na kufanya marekebisho ili kila upande unufaike kwani kwa sasa inaonekana kuwa pande nyingine hazinufaiki na mkataba huo.     
Mwisho.
   

 
   


No comments:

Post a Comment