Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA Kuwa mawasiliano endapo yatatumika vizuri yana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji hapa nchini na kusababisha wananchi kutambua fursa za maendeleo zilizopo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakatia akifungua mafunzo ya siku moja ya wadau wa maweasiliano yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) juu ya zoezi la uzimaji simu bandia linalotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi huu.
Ndikilo alisema kuwa makampuni na mashirika kuanzia yale ya nje na ndani ya nchi yameweza kuongeza uwekezaji kwenye sekta mbalimbali kupitia mawasiliano yakiwemo ya Mitandao ya Kijamii ,Simu, Redio, Televisheni na Magazeti.
“Mawasiliano ni chombo cha maendeleo endapo kinatumika vizuri na tumeona faida ya mawasiliano hasa yale ya intaneti ambapo wananchi wameweza kujua fursa mbalimbali za kufanya biashara za ndani na nje nchi nah ii yote imetokana na kuboreshwa suala la mawasiliano,” alisema Ndikilo.
Alisema kupitia mitandao kasi ya maendeleo imekuwa kubwa kup[itia mitandao kwa wale waliotumia vizuri ila kwa wale wanaotumia vibaya imekuwa ni kero kwani baadhi wameitumia kwa kutoa lugha chafu, wizi, utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.
“Faida ni nyingi ikilinganishwa na hasara na katika uboreshaji wa kuondoa simu bandia itasaidia kukabiliana na wizi, matumizi mabaya kama vile kashfa na vitendo vibaya vilivyokuwa vinatumika kupitia mitandao kwani hata wale wezi wa kukwapua simu mwisho wao umefika,” alisema Ndikilo.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa TCRA Isaac Mruma alisema kuwa wameamua kutoa elimu hiyo kwa wananchi kabla ya kufikia hatua ya kuzima simu bandia ili wawe wanajua na namna ya kugundua simu hizo ambazo zitasitishwa matumizi yake ifikapo Juni 16 mwaka huu.
Mruma alisema kuwa wametoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya mafundi simu, wauzaji wa simu, maofisa wa kamati za ulinzi na usalama, waandishi na wananchi wa kawaida kwenye kanda ambapo kanda ya Mashariki ni ya mwisho ikiwa na mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara, Dar es Salaam na Morogoro.
Naye meneja mradi Injinia Imelda Salum alisema kuwa mbali ya kuondolewa bidhaa bandia za mawasiliano pia zoezi hilo litaambatana na rejesta ya utambulisho wa watumiaji wa wa vifaa vya simu ili kuboresha huduma za mawasiliano.
Salum alisema kuwa kwa mafundi wa simu wanapaswa kutozirekebisha simu hizo ili kuwaaminisha kuwa simu fulani ni aina fulani kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai ambapo mhusika anaweza kuchukuliwa hatua ya kisheria.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment