Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani
linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa gari la abiria
aina ya Toyota Noah Mohamed Ramadhan (21) mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha
mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura
Mushongi alisema kuwa watu hao walimkodisha dereva huyo.
Mushongi alisema kuwa tukio
hilo lilitokea Juni 13 mwaka huu majira ya saa 19:45 usiku eneo la Vigwaza
Tarafa ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
“Watu hao walimuua dereva huyo
kwa kumkaba shingoni kisha kupora gari hilo lenye namba za usajili T 119 DDM
rangi nyeupe lililokuwa likitumiwa na marehemu baada ya kumkodi wakimataka
awapeleke Kanisa la Pentekoste Vigwaza,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watu hao kabla ya
kumuua marehemu walimkaba wakiwa njiani ambapo alipiga kelele kuomba msaada na
madereva bodaboda walizisikia na kuamua kufuatilia gari hilo barabara ya vumbi
kwenye njia kuu ya umeme wa Tanesco.
“Watu wale walipoona taa za
bodaboda waliamua kusimama na kutoka ndani ya gari na kuanza kukimbia kutokomea
porini lakini mmoja wao alikamatwa palepale na walipoangalia ndani walikuta mwili
wa marehemu ukiwa umewekwa kiti cha nyuma kwa lengo la kwenda kuutupa mwili huo
porini ili kuondoka na gari hilo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa juhudi za
wananchi, dereva bodaboda na polisi zilifanikisha kukamatwa watuhumiwa wawili
ambao majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa ili kutoharibu upelelezi kwani
watu hao ni mtandao wa majambazi ambao wengine wako Jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa mwili wa
marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi kusubiri ndugu
na uchunguzi wa daktari kwa ajili ya mazishi.
Aliwataka madereva wa vyombo
vya moto hasa wale wanaofanya biashara za usafirishaji nyakati za usiku kuwa
makini ili kujiepusha na matukio kama hayo ya wizi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment