Na John Gagarini, Bagamoyo
WAZAZI na walezi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kutowanyima haki za msingi ikiwa ni pamoja na elimu watoto wao kutokana na migogoro yao ya ndoa.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwenye wilaya hiyo yaliyofanyika shule ya Msingi Mwanamakuka Bagamoyo.
Sharifu alisema kuwa ugomvi baina ya wazazi imekuwa ikisababisha watoto wengi kukosa haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na elimu hali ambayo imesababisha wakose maadili mazuri.
“Kutokana na migogoro ya kifamilia au ndoa imekuwa ikisababisha watoto wengi kukosa elimu ambayo ndiyo urithi pekee ambao anaweza kurithishwa mtoto na si mali ambazo zinaweza kwisha lakini elimu ni urithi wa kudumu,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa mbali ya changamoto ya watoto kukosa elimu pia watoto wa kike hujikuta wakipata mimba za utotoni ambazo ni hatari kwa masiha yao kutokana na maumbile yao.
“Tunataka mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali kuwachukua wale wote wanaobainika kuwapa mimba lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa kufuata mkondo wake ili kukomesha tabia hiyo mbaya,” alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa watoto wenye ulemavu wa viungo na walemavu wengine wana haki kama wengine hivyo jamii isiwanyanyapae ni lazima haki zao zitazamwe na kuwashirikisha katika mikutano mbalimbali na shughuli za kijamii ili kuibua vipaji vyao viweze kuwasaidia kuacha vitendo vya kuwaajiri watoto. Kwa upande wake mkurugenzi wa Kaya Fm, Marie Shaba alisema katika bara la Afrika, Kusini, Mashariki, mitaa, kwenye familia watoto walio wengi hawaishi kwa raha na wanakosa haki zao ambapo sherehe hizo zinapaswa kuwakumbusha kwa yaliyotokea nchini Afrika ya Kusini huko Soweto ambapo watoto 700 walifariki kwa kudai haki zao.
Kwa upande wa watoto akiwemo Fatuma Sadik, kutoka shule ya msingi Mbaruku alisema kufiwa na wazazi pia husababisha baadhi ya watoto kufukuzwa na ndugu na jamaa kwa tamaa za mali zilizoachwa na wazazi.
Alisema suala hilo husababisha watoto kukosa haki zao msingi za kuishi kwa amani na upendo na kwa mtazamo wa haraka hiyo si migogoro bali ni vita, machafuko na ukosefu wa amani na haki za msingi dhidi ya watoto na aliiomba jamii ilinde haki zao na kuzifanyia kazi kisheria ikiwemo haki ya kupata elimu, kulindwa, kusikilizwa na kupendwa pasipo kubaguliwa. Mwisho |
Saturday, June 18, 2016
MIGOGORO YA NDOA ISIWANYIME HAKI ZA MSINGI WATOTO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment