Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka
wawekezaji kwenye Visiwa vilivyopo Wilayani Mafia kushirikiana na serikali ili
kudhibiti usalama wa nchi kukabiliana na wageni wasio waaminifu ambao wanaoweza
kuvitumia visiwa hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati ya Ulinzi na
Usalama ya mkoa ilipotembelea Kisiwa cha Shungimbili kwenye Hoteli ya Thanda
ambayo inamilikiwa na raia wa kigeni na kusema kuwa kuna haja ya kuwa na kituo
cha kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na hali ya sasa kuwa mbaya
kiusalama kutokana na matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanatokea hapa nchini
ni vema ulinzi ukaimarishwa.
“Kuna haja ya kuwa na ushirikiano na baina ya wawekezaji na
serfikali ili kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kutumia visiwa kujiingiza
hapa nchini na kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa dunia ya sasa imebadilika na baadhi ya watu
wamekuwa wakitumia njia ya Bahari kupitisha wahamiaji haramu, dawa za kulevya
pamoja na uingizwaji wa silaha.
“Serikali haina nia mbaya ya kutaka kujua mambo yanayofanywa
na wawekezaji kwa kujua wageni wanaoingia na kutoka na wameleta nini wanatoka
na nini na hapa kutakuwa na kituo cha ukaguzi ambacho kitakuwa na polisi kwa
ajili ya kulinda eneo la Kisiwa kwani wageni watakuwa wanafika kwa wingi,”
alisema Ndikilo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Thanda Island Tanzania
Ltd Oscar Pucci alisema kuwa hana tatizo na ushirikiano na serikali kwani
anashirikiana vizuri na Halmashauri.
Pucci alisema kuwa wamekuwa wakisaidia shughuli za maendeleo
kama kuchangia kwenye Hospitali ya wilaya na hata wavuvi wanaovua jirani na
hoteli yao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment