Thursday, June 23, 2016

MILIKINI MAENEO KIHALALI KUEPUKA MIGOGORO YA ARDHI-RC

Na John Gagarini, Kibaha

MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wakazi wa mkoa huo kufuta taratibu na sheria za kumiliki ardhi ili kuepukana na migogoro ya ardhi ambayo kwa sasa imeshamiri na inaweza kuhatarisha amani.

Aidha amesema kuwa mkoa hautasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu ambao wanavamia maeneo ya watu na kuyauza kama wanavyofanya baadhi ya watu kwani ni kinyume cha sheria na watachukuliwa hatua kali ili waachane na tabia hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na baadhi wananchi kutoka wilaya ya Mkuranga Ndikilo alisema kuwa kumekuwa na migogoro mingi ambayo imesababisha wananchi kutokuelewana wao kwa wao.

“Moja ya mfano ni Kijiji cha Kazole Kitongoji cha Magodani Kata ya Vikindu wilaya ya Mkuranga kuna baadhi ya watu wanajifanya kamati ya ardhi ya Kijiji hicho kulivamia shamba la kampuni ya Soap Allied Industry ambalo lina ukubwa wa hekari 1,750 likiwa na hati ya umiliki 271 ambayo iliipata tangu mwaka 1988 ambalo lilitengwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji,”alisema Ndikilo.

Ndikilo alisema kuwa kamati hiyo ambayo imekuwa ikiuza viwanja kwenye eneo hilo inafanya makosa kwa kuwauzia watu kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria kwani eneo hilo lina mmiliki halali ambaye anamiliki kisheria.

“Kama haitoshi watu hao walikwenda kwenye vyombo vya sheria lakini walishindwa na kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mtu hivyo hawapaswi kuingie kwenye eneo hilo lakini wanakamati hao bado wanaendelea kuwauzia watu na kujipatia mamilioni ambayo yote yanaingia mifukoni mwao na wamejinufaisha kupitia shamba hilo lakini wanawaibia watu kwani mmiliki mwenyewe yupo,” alisema Ndikilo.

Aidha alisema kuwa suala la shamba hilo linachukuliwa kisiasa lakini mwisho wa siku linaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwani watu waliotoa fedha zao watakapoambiwa waondoke watadai fedha zao na hakuna mtu wa kuwarejeshea hivyo kuleta migogoro ambayo haitakiwi.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa ni vema watu wakafuata sheria bila ya shuruti kwani eneo hilo limeshatolewa maamuzi baada ya watu waliouziwa kwenda mahakamani na kuonekana kuwa kampuni hiyo ndiyo yenye uhalali wa kumiliki eneo hilo hivyo watu kuingia humo ni kuvunja sheria na wanaweza kukamatwa na polisi

Mushongi alisema kuwa watu hawapaswi kuingia kwenye eneo hilo ambapo hivi karibuni zaidi ya watu 20 waliingia kwenye shamba na kukamatwa na kwa kuwa hati ya umiliki bado haijatenguliwa watu wasiingie na kama wanaona wana haki ni vema wakaenda mahakama za juu kudai haki yao lakini si kulivamia.


Mwisho.       


No comments:

Post a Comment