Thursday, June 23, 2016

KITONGOJI CHA MWEMBEBARAZA KUPATA MAJI KARIBUNI


Na John Gagarini, Kibaha

WAKAZI 200 wa Kitongoji cha Mwembebaraza kwenye mamlaka ya Mji  Mdogo wa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani wanatarajia kuanza kupata maji ya bomba mwanzoni  mwa mwezi Julai mwaka huu baada ya mradi wa maji ya mkopo kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) wilaya ya Kibaha kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake meneja wa Dawasco wilaya ya Kibaha Erasto Emanuel alisema kuwa katika kuhakikisha wanatatua changamoto ya maji walikaa na uongozi wa Kitongoji hicho na kuwataka wananchi kuchimba mitaro kwa ajili ya kupitisha mabomba yatakayopitisha maji imeshakamilika.

Emanuel alisema kuwa mitaro hiyo ilikamilika muda mrefu lakini kulikuwa na tatizo ambalo hata hivyo walishalifanyia kazi na tayari wameshawapeka wataalamu kwa ajili ya kupima na zoezi la upimaji limekamilika wanchosubiri ni taarifa toka kwa wataalamu hao ili waanze kuyatandaza mabomba hayo.

“Maji haya ni ya mkopo ambapo mwananchi hatochangia chochote ila atalipa ndani ya miezi 12 huku akiwa analipa na bili za kila mwezi na tunatarajia hadi mwanzoni mwa mwezi Julai maji yataanza kutoka hivyo wasiwe na wasiwasi,” alisema Emanuel.

Awali wananchi hao walitoa malalamiko yao kwa meneja huyo kuwa licha ya kuambiwa wachimbe mitaro kwa ajili ya kupatiwa maji kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwli iliyopita bila ya kupelekewa huduma hiyo ya maji.

Wakizungumza na waandishi wa habari wananchi hao wakiongozwa na Tausi Said, Mwantumu Salmin, Juma Salum na Abdala Ally walisema kuwa kutokana na tatizo la maji katika kitongoji hicho waliambiwa wachimbe mitaro hiyo kwa ajili ya kupelekewa maji ya mkopo toka Dawasco.

Walisema kuwa waliahidiwa kuwa mara watakapokamilisha zoezi hilo watapelekewa mabomba kwa ajili ya kupata maji kupitia mradi wa maji ya mkopo ambayo waliambiwa ndani ya mwezi mmoja watakuwa wamepelekewa huduma hiyo lakini mwezi unaisha hakuna kinachoendelea hadi sasa.

“Kinachotushangaza ni kwamba Kitongoji jirani cha Disunyala ambacho kiko mbele yao kimepata maji huku wao wakiwa wamerukwa na wenzao kupelekewa maji licha ya kuwa mfereji uliochimbwa ni mmoja ambapo kila kaya ilichimba mfereji huo ambao umeunganishwa kwenye vitongoji hivyo kwani ulikuwa kwenye mradi mmoja,” walisema wakazi hao.

Mwisho

No comments:

Post a Comment