Monday, June 20, 2016

MWENYEKITI WA MTAA AWAZAWADIA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI

Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani umewapa zawadi mbalimbali wanafunzi wa darasa la saba waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya katikati ya muhula.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati wa kukabidhi zawadi hizo kwa wanafunzi hao Rashid Likunja alisema kuwa ameweka utartibu huo kwa wanafunzi wa darasa la saba ili kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye mtihani wa kumaliza darasa la saba.

Likunja alisema kuwa zawadi anazotoa ni mfuko wake aliouanzisha kwa ajili ya kuwapa hamasa ya wanafunzi wa mtaa huo kusoma kwa bidii na kuongeza ufaulu.

“Unajua mtaa huu hakuna shule ya msingi ambapo wanafunzi huwabidi kwenda kusoma mtaa jirani wa Visiga ambapo wengine wanatembea kilometa nane kila siku hivyo kuwakatisha tamaa watoto hivyo kutotilia makazo elimu,” alisema Likunja.
Aidha alisema kuwa kabla ya kuanza utaratibu huo wanafunzi wa mtaa huo walikuwa wakishika nafasi za nyuma kuanzia 35 na kushuka chini lakini a kwa sasa wameanza kuhamasika na wameweza kuingia kwenye 10 zaidi ya wanafunzi watano.

“Nimeanzisha mfuko wa kuwasaidia wanafunzi wa mtaa wetu naomba na wadau wengine wajitokeze kusaidia ili zawadi ziwe kubwa kwani nianazotoa ni ndogo lakini naamini wadau zaidi watajitokeza kuniunga mkono juu ya suala la elimu ambalo nimelipa kipaumbele cha kwanza,” alisema Likunja.

Moja ya wazazi ambao mwanae kapewa zawadi baada ya kuwa moja ya wanafunzi walioingia kwenye 10 bora Mwajabu Suleiman alisema kuwa mwenyekiti wao amewapa changamoto kubwa ya kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii.

Suleiman alisema kuwa watamuunga mkono mwenyekiti wao kwa kuwahamasisha watoto wao kusoma kwa bidii ili wawe chachu ya wanafunzi wenzao wanaoanza madarasa ya awali.


Mwisho.    

No comments:

Post a Comment