Na John Gagarini, Kibaha
MTAA wa Zegereni wilayani Kibaha umefayatua matufali 2,500 kwa ajili ya
kuanza ujenzi wa shule ya Msingi katika mtaa huo ambao unategemea mtaa wa
Visiga kuwapeleka watoto wao umbali wa kilometa nane.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake wakati wa zoezi la kuwapa zawadi wanafunzi wa
darasa la saba ambao wamefanya vizuri na kuwa kwenye 10 bora mwenyekiti wa mtaa
huo Rashid Likunja amesema kuwa wanatarajia kuanza ujenzi wa shule hiyo kuanzia
Julai Mwaka huu ili ifikapo mwakani watoto wao waanze kusoma kwenye shule hiyo.
Likunja amesema
kuwa fedha za kununulia kiwanja chenye ukubwa wa hekari sita zimetokana na
mchango wa shilingi 5,000 kila kaya ambapo hatua ya ujenzi itaanza kwa kutumia
tofaali hizo huku wakiwa na mifuko 12 ya simenti wakianza na madarasa mawili,
ofisi na matundu manne ya vyoo.
Amesema kuwa
kwa sasa wako kwenye harakati za kupata kibali cha ujenzi pamoja na ramani toka
Halmashauri ya Mji ili waweze kuanza ujenzi huo na utawapunguzia watoto wao
kwenda kusoma mbali pia huwabidi kuvuka barabara ya Morogoro ambapo ni hatari
kwao kwani wengine ni wadogo sana.
Aidha amewataka
wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia ili waweze kutekeleza azma yao ya ujenzi
wa shule hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa watoto wanaotoka mtaa huo ambao
wanafikia zaidi ya 200 wanaosoma madarasa mbalimbali kutoka mtaa huo ambao
wanasoma shule jirani ya Visiga.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment