Saturday, June 18, 2016

WAVUNJUA VIOO VYA MADIRISHA WAPAKA KINYESI OFISI YA KATA

BOMOABOMOA YALIZA WENGI KIBAHA

MIGOGORO YA NDOA ISIWANYIME HAKI ZA MSINGI WATOTO

Tuesday, June 14, 2016

WATATU WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA DEREVA WA NOAH

Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa gari la abiria aina ya Toyota Noah Mohamed Ramadhan (21) mkazi wa Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao walimkodisha dereva huyo.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 13 mwaka huu majira ya saa 19:45 usiku eneo la Vigwaza Tarafa ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo.
“Watu hao walimuua dereva huyo kwa kumkaba shingoni kisha kupora gari hilo lenye namba za usajili T 119 DDM rangi nyeupe lililokuwa likitumiwa na marehemu baada ya kumkodi wakimataka awapeleke Kanisa la Pentekoste Vigwaza,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watu hao kabla ya kumuua marehemu walimkaba wakiwa njiani ambapo alipiga kelele kuomba msaada na madereva bodaboda walizisikia na kuamua kufuatilia gari hilo barabara ya vumbi kwenye njia kuu ya umeme wa Tanesco.
“Watu wale walipoona taa za bodaboda waliamua kusimama na kutoka ndani ya gari na kuanza kukimbia kutokomea porini lakini mmoja wao alikamatwa palepale na walipoangalia ndani walikuta mwili wa marehemu ukiwa umewekwa kiti cha nyuma kwa lengo la kwenda kuutupa mwili huo porini ili kuondoka na gari hilo,” alisema Mushongi.
Aidha alisema kuwa juhudi za wananchi, dereva bodaboda na polisi zilifanikisha kukamatwa watuhumiwa wawili ambao majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa ili kutoharibu upelelezi kwani watu hao ni mtandao wa majambazi ambao wengine wako Jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi kusubiri ndugu na uchunguzi wa daktari kwa ajili ya mazishi.
Aliwataka madereva wa vyombo vya moto hasa wale wanaofanya biashara za usafirishaji nyakati za usiku kuwa makini ili kujiepusha na matukio kama hayo ya wizi.
Mwisho.         

    

Thursday, June 9, 2016

RC ATAKA MKATABA WA UWEKEZAJI KUPITIWA UPYA

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ametaka kupitiwa upya mkataba wa kuuziwa mwekezaji eneo la Magofu ya Chole wilaya ya Mafia mkoani Pwani ambapo kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development Ltd imemilikishwa ambapo eneo hilo kuna gereza walilokuwa wanafungwa watumwa enzi za ukoloni wakati wa Utawala wa Wajerumani.
Aidha ameunda tume ya kufuatilia undani wa mkataba huo na amezuia marekebisho yaliyokuwa yanafanywa na kampuni hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi pale ufumbuzi wa kujua namna mkataba huo ulivyoingiwa baina ya Kijiji cha Chole na mwekezaji huyo kama umezingatia taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Chole Mjini kata ya Jibondo kwenye mkutano wa hadhara Ndikilo alisema kuwa mkoa hauna nia mbaya na mwekezaji huyo ambaye amepewa hati miliki ya eneo hilo kwa kipindi cha miaka 33.
Ndikilo alisema kuwa eneo hilo ambalo lina kumbukumbu mbalimbali ambalo liko jirani na Bahari ya Hindi lilikuwa likitumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na soko la Watumwa pamoja na gereza lina ukubwa wa hekta 3.7 ambapo eneo hilo liko chini ya Wizara ya maliasili na Utalii Idara ya Malikale.
“Mkataba huo ambao ulisainiwa mwaka 2007 shamba namba 2031 baina ya mwekezaji  Dk Jean de Villiers na Kijiji hicho ambapo mwenyekiti wa Kijiji hicho Maburuki Sadiki alisaini kwa niaba ya Kijiji na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya wakati ule Manzie Mangochi pasipo kuishirikisha Halmashauri ya wilaya ambayo haipati mapato yoyote kutokana na uwekezaji huo licha ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi wa Kijiji cha Chole” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amemtaka mwekezaji huyo kusimamisha ukarabati na kuunda tume ya kufanya uchunguzi na itatoa majibu baada ya mwezi mmoja ili kujiridhisha na kumilikishwa eneo hilo mtu binafsi eneo la serikali la kihistoria na kujengwa hoteli ya kitalii kwa kukarabati jengo la zamani.
Alibainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma barua ambayo iliyosainiwa na John Kimaro kwa niaba ya katibu mkuu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuhirikiana na mwekezaji na kusema kuwa sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979 na sera ya Malikale ya mwaka 2008 inasema Malikale au Magofu yanaweza kumilikiwa na mtu binafs, taasisi na serikali.
Barua hiyo inaendelea kusema kuwa jukumu la serikali (Idara ya Mambo ya Kale) ni kuhakikisha kuwa mmiliki hatabomoa au kufanya chochote katika magofu hayo kinyume cha sheria.
Akitoa maelezo juu ya umiliki wake mkurugenzi wa Chole Mjini Conservation and Development Company Ltd Anne De Villiers amesema kuwa kampuni hiyo iliingia Mafia na kukuta hali ya majengo hayo ya kale yakiwa kwenye hali mbaya ndipo walianza mchakato wa kuyakarabati.
Dk Villiers alisema kuwa lengo la kuchukua eneo hilo ni kuhakikisha uasili wa mahali hapo haupotei kwa kuyafanyia ukarabati magofu hayo ambapo moja lilibaki ukuta mmoja na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati huo.
Naye mkuu wa wilaya ya Mafia Dk Nasoro Hamid alisema kuwa serikali haishirikishwi jambo lolote wala haijui ni watalii wangapi wanaoingia hapo wala mapato yanayopatikana kwenye eneo hilo.
Dk Hamid amesema kuwa Kijiji cha Chole ndicho kiliingia mkataba na mwekezaji huyo ambapo hugawana asilimia kutokana na watalii wanaoingia kwenye eneo hilo la makumbusho lakini tatizo haijulikani kinachopatikana hapo ni kiasi gani katika mgawanyo huo wa mapato.
Awali baadhi ya wanakijiji wakizungumzia suala hilo wakiongozwa na Ally Sikubali na Hemed Ally walisema kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo ni mkataba Kiswahili unasema kuwa endapo kutakuwa na kutoeleweka mkataba wa Kiingereza ndiyo utakaotumika.
Waliomba mkataba huo uangaliwe upya na kufanya marekebisho ili kila upande unufaike kwani kwa sasa inaonekana kuwa pande nyingine hazinufaiki na mkataba huo.     
Mwisho.
   

 
   


WATAKA TAARIFA KUHUSU ENEO LA UWEKEZAJI BAADA YA MRADI WA MIWA KUFUTWA

Na John Gagarini, Bagamoyo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imetakiwa kutoa taarifa rasmi kwenye vijiji vilivyokuwa kwenye mradi wa kilimo cha miwa chini ya kampuni ya Eco Energy uliosimamishwa na serikali ili eneo hilo lisije kuchukuliwa na mtu mwingine ili hali wananchi hao hawajalipwa fidia.
Mradi huo ulisimamishwa kupitia majibu ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa anajibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe aliyetaka kujua ni kwanini serikali imeshindwa kuweka jitihada za makusudi ili mradi huo ukamilike ambao ulibainika kuwa ungetumia maji mengi ya Mto Wami na kuathiri usatawi wa wanyama kwenye Mbuga ya Saadani.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Bagamoyo katibu wa kamati ya ardhi ya Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Mkombozi Bakari Salum alisema kuwa     kwa kuwa kauli ya Waziri Mkuu ni agizo ni vema Halmashauri ingetoa tangazo rasmi kwa wananchi husika.
“Kwa kuwa wakati anakuja mwekezaji kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya mradi huo kulikuwa na taarifa rasmi na wananchi walitoa maeneo yao kwa ajili ya kilimo hicho cha miwa ambacho baadaye kungejengwa kiwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari hivyo baada ya kushindikana wangewajulisha wananchi,” alisema Salum
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Jackson Mkango alisema kuwa eneo ambalo lilichukuliwa na mwekezaji ni hekari zaidi ya hekta 22,000 wananchi hao hawajalipwa fidia yoyote licha ya kuwa tathmini kufanyika mwaka 2011 hadi leo hawajalipwa.
Mkango alisema kuwa sheria inasema kuwa tathmini ikifanyika walengwa wanapaswa kulipwa ndani ya kipindi cha miezi sita lakini sasa imepita miaka mitano sasa.
“Tunaiomba Halmashauri kutoa tamko juu ya ardhi hiyo ya wananchi ambayo toka imechukuliwa wananchi hawakufanya chochote licha ya kuwa eneo hilo walikuwa wakitegemea kwa ajili ya kilimo na hawajui hatma yao kwani walitegemea wangelipwa fidia,” alisema Mkango.
Vijiji vilivyokuwa kwenye mpango huo ni Razaba, Matipwili, Kitame, Fukayosi, Makaani na Gongo ambapo kuna jumla ya wananchi zaidi ya 700 ambao walikuwa wakiishi kwenye maeneo hayo yaliyoingizwa kwenye mradi huo ambao ulikuwa na lengo la kukabiliana na upungufu wa sukari hapa nchini.

Mwisho.

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUDUMISHA AMANI YA NCHI

Na John Gagarini, Mafia
MKUU wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo amewataka wawekezaji kwenye Visiwa vilivyopo Wilayani Mafia kushirikiana na serikali ili kudhibiti usalama wa nchi kukabiliana na wageni wasio waaminifu ambao wanaoweza kuvitumia visiwa hivyo kuhatarisha amani ya nchi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilipotembelea Kisiwa cha Shungimbili kwenye Hoteli ya Thanda ambayo inamilikiwa na raia wa kigeni na kusema kuwa kuna haja ya kuwa na kituo cha kufuatilia wageni wanaoingia na kutoka.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na hali ya sasa kuwa mbaya kiusalama kutokana na matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanatokea hapa nchini ni vema ulinzi ukaimarishwa.
“Kuna haja ya kuwa na ushirikiano na baina ya wawekezaji na serfikali ili kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kutumia visiwa kujiingiza hapa nchini na kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa dunia ya sasa imebadilika na baadhi ya watu wamekuwa wakitumia njia ya Bahari kupitisha wahamiaji haramu, dawa za kulevya pamoja na uingizwaji wa silaha.
“Serikali haina nia mbaya ya kutaka kujua mambo yanayofanywa na wawekezaji kwa kujua wageni wanaoingia na kutoka na wameleta nini wanatoka na nini na hapa kutakuwa na kituo cha ukaguzi ambacho kitakuwa na polisi kwa ajili ya kulinda eneo la Kisiwa kwani wageni watakuwa wanafika kwa wingi,” alisema Ndikilo
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Thanda Island Tanzania Ltd Oscar Pucci alisema kuwa hana tatizo na ushirikiano na serikali kwani anashirikiana vizuri na Halmashauri.
Pucci alisema kuwa wamekuwa wakisaidia shughuli za maendeleo kama kuchangia kwenye Hospitali ya wilaya na hata wavuvi wanaovua jirani na hoteli yao.

Mwisho.