Monday, May 20, 2013

WAKAZI WAHITAJI DARAJA LA KUDUMU


Na John Gagarini, Kibaha
MTAA wa Lumumba wilayani Kibaha unahitaji zaidi ya shilingi milioni tisa kwa ajili ya kuweka nguzo tatu za daraja la mbao kwenye kivuko cha mto Mpiji mpakani mwa wilaya ya Kibaha na Kinondoni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa mtaa huo Gidion Tarimo alisema kuwa daraja hilo ni muhimu kwao kwa ajili ya kupata mahitaji yao ya kila siku ambayo huyapata mtaa wa Kibwegere wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Tarimo alisema kuwa wilaya ya Kinondoni kwao ni karibu ukilinganisha na Kibaha Maili Moja hivyo daraja hilo linahitaji kufanyiwa matengenezo ili liweze kupitika kwa urahisi hasa kupitisha magari mbapo kwa sasa hayapiti.
“Tumeazimia kujenga daraja hilo hadi magari yaweze kupita ambapo kwa sasa magari hayapiti hata hivyo tumepiga hatua kwani zamani watu walikuwa wakipita mtoni moja kwa moja lakini kwa sasa hawagusi maji na maji yalipokuwa yakijaa watu walikuwa hawawezi kuvuka kwenda ngambo ya pili,” alisema Tarimo.
Alisema kuwa hadi kufikia hatua hiyo wametumia kiasi cha shilingi milioni nane ambapo wananchi wamejitolea huku fedha za mfuko wa Jimbo ni kiasi cha shilingi milioni mbili.
“Changamoto za matumizi ya daraja hili ni kubwa kwani ili mtu upate huduma mbalimbali za kijamii lazima uvuke na kama kuna mamamjamzito lazima ashushwe kwenye pikipiki ambazo hutumika hali ambayo si salama kwa wagonjwa wa namna hiyo,” alisema Tarimo.
Aidha alisema kuwa tayari wameshapeleka barua kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya kusaidiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
Aliwaomba watu na mashirika mbalimbali kuwasaidia ili kufanikisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2015 ili kurahisisha mawasiliano na sehemu za huduma.
Mwisho.
    
   
 Mwenyekiti wa mtaa wa Lumumba Gidioni Tarimo akipita juu ya daraja la mbao la Mto Mpiji ambapo wanahitaji kiasi cha shilingi milioni tisa kwa ajili ya kuweka nguzo kwa lengo la kuliimarisha ili liweze kupitika ambapo kwa sasa magari hayawwezi kupita, wakazi wa mtaa huo hupata huduma za Kijamii mtaa wa Kibwegere wilaya ya Kinondoni

VIONGOZI WAASWA


Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI Umma nchini wametakiwa kuzingatia weledi wakati wa kutimiza wajibu wao kwa watumishi na wananchi ili waweze kuleta ufanisi kwenye utendaji kazi.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Kamishna ofisi ya Rais - Tume ya Utumishi wa Umma, Cecilia Shirima alipoongea na sekretarieti na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.
 Shirima amesema kuwa ili kufanikisha utendaji kazi kwa viongozi ni vema wakatumia sharia kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Amesema viongozi wanapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani bila ya kuzingatia utartibu wa utumishi wa umma kutasababisha ufanisi wa kazi kuwa chini na kutokuwa na tija,” alisema Shirima.
Kwa upande wake katibu wa tume hiyo Claudia Mpangala amesema kuwa lengo la kuja hapo ni kupeleka ujumbe kwa wadau wa tume hiyo kwenye mikoa kote nchini juu ya kuzingatia weledi wakati wa kufanya kazi zao.
Mpangala amesema kuwa kiongozi bora ni Yule anayefanya kazi kwa kutumia taratibu zilizopangwa juu ya utumishi uliotukuka na kuacha kufanya kazi kwa matakwa yao.
Ameongeza kuwa ili nchi iweze kufanikiwa viongozi na watumishi wanapaswa kuzingatia taratibu za utumishi wa Umma kama zinavyoelekeza.
Amebainisha kuwa tume hiyo tayari imeshatembelea mikoa 21 na sasa inatarajia kutembelea wakala wa serikali na ilianza kutekeleza majukumu yake mwaka 2004, ikiwa na kazi kubw aya kufuatilia na kusimamia utumishi wa umma ili kuhakikisha unaendeshwa kwa mujibu wa sharia, kanunia na taratibu.
Mwisho.   

Kamishna ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma Cecilia Shirima katikati akizungumza na sekretarieti ya mkoa na watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani, kushoto ni katibu Tawala mkoa huo Beartha Swai na kulia ni katibu wa tume ya utumishi wa umma Claudia Mpangala.

Friday, May 17, 2013

AJIFANYA USALAMA ADAKWA


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia John Semindu mkazi wa Kibamba CCM kwa tuhuma za kujifanya kuwa ni mtumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha usalama na kujipatia fedha kwa watu mbalimbali kwa ahadi ya kuwatafutia kazi serikalini.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia kitambulisho cha usalama wa Taifa kujipatia fedha kwa njia hiyo ya udanganyifu.
Matei alisema kuwa katika upekuzi mtuhumiwa alikutwa na vyeti vya watu mbalimbali vya kitaaluma kwa madai ya kuwatafutia nafasi za kazi serikalini.
“Mtuhumiwa tunamshikilia na uchunguzi bado unaendelea ambapo alikuwa akitumia gari aina ya Suzuki Escudo rangi ya bluu yenye namba za usajili T 383 ARA,” alisema Matei.
Kamanda Matei aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu ijayo kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Mwisho.


  

Wednesday, May 15, 2013

WAMWAGIWA VIFAA VYA MICHEZO


Na John Gagarini, Kibaha
MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani David Mramba ametoa mipira sita kwa timu za mpira wa pete za kata ya Kibaha.
Mramba alikabidhi mipira hiyo kwa manahodha wa timu za Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa matawi ya kata hiyo kwa lengo la kucheza ligi ili kupta timu ya kata.
Alisema kuwa  aliona changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa vya michezo ikiwemo mipira ndiyo sababu ya yeye kutoa mipira hiyo ili iweze kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
“Mipira hii iwe changamoto kwenu katika kukabiliana na ukosefu wa vifaa kwani kwa sasa michezo mbali ya kuimarisha afya zenu pia ni ajira hasa kwa vijana ambao wengi hawana ajira,” alisema Mramba.
Aidha alisema kuwa mipira hiyo itasaidia kufanikisha kufanya mashindano ya ngazi ya matawi ambayo inatarajiwa kuanza kufanyika mwezi wa Julai.
“Mashindano hayo yataleta mahusiano mazuri baina ya wanachama wa CCCM na hata jamii kwa ujumla hivyo mipira hiyo itumike na si kuiweka ndani kama mapambambo,” alisema Mramba.
Naye Diwani wa Viti Maalumu Selina Wilson alizitaka timu hizo kuanza maandalizi mapema kwani tayari wameshapata mipira ambayo ilikuwa ikiwafanya washindwe kufanya mazoezi na kukutana kwenya mashindano tu.
Akishukuru kukabidhiwa mipira hiyo katibu wa UWT kata ya Kibaha Sada Duda alisema kuwa kwao hiyo ni changamoto ambayo itawafanya wahamasike na kushiriki michezo ipasavyo. Matawi yaliyopewa mipira hiyo kila tawi likipata mpira mmoja ni Mwendapole A, Kwa Mfipa, Changombe, Kitende, Simbani na Mwendapole B.
Mwisho.   







MATAWI YA CCM YATAKIWA KUANZISHA VITEGA UCHUMI


Na John Gagarini, Kibaha
MATAWI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini yametakiwa kuanzisha vitega uchumi ili kujiongezea kipato badala ya kuyafanya matawi hayo vijiwe vya kukaa bila ya tija.
Hayo yalisemwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) kutoka wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Rugemalira Rutatina, wakati akizindua tawi la Mtazamo lililopo kata ya Tumbi wilayani humo.
Rutatina alisema kuwa matawi hayo ndiyo msingi wa chama hivyo lazima matawi hayo yajianzishie vyanzo vya kupata mapato badala ya kukaa tu na kubweteka.
“Hili ni kati ya matawi ambayo yameonyesha mwanga kwani kuwa na fedha kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ni kitu muhimu na si vema tawi kuwa sehemu ya kukaa tu bila ya kubuni vyanzo vya mapato na si kusubiri kusaidiw akwa kila kitu,” alisema Rugemalila.
Alisema kuwa kwa kuwa matawi ndipo sehemu ya kukiimarisha chama lazima matawi hayo yawe na nguvu za kiuchumi ili waweze kukiimarisha chama.
“Mkiwa na uchumi imara mnaweza kuisaidia jamii mfano kutoa vitanda kwa wagonjwa kwenye hospitali au kuihudumia kwa njia yoyote ile ili iwe mfano mzuri,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa wanachama wa CCM wanatakiwa kuwaeleza viongozi changamoto zilizopo na si kuanzisha makundi ambayo hayana manufaa.
Aliwataka Watanzania kuwa na imani na chama na kukataa propaganda za wapinzani kuwa hakuna kilichofanyika tangu nchi kupata uhuru jambo ambalo ni upotoshaji.
Mwisho.

Sunday, April 28, 2013

ATOA MIPIRA KWA VIJANA


Na John Gagarini, Kibaha
MJUMBE wa Baraza Kuu Taifa kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Pwani Mariamu Chaurembo ametoa mipira mitatu ya mpira wa miguu kwa chipukizi wa Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini ili washindanie.
Alitoa mipira hiyo juzi mjini Kibaha wakati wa ziara ya mwenyekiti wa chipukizi Taifa Gabriel Amos Makala, alipotembelea mkoa wa Pwani kujua shughuli zinazofanywa na umoja huo.
Chaurembo alisema kuwa lengo la kutoa mipira hiyo ni chipukizi hao waweze kukuza, kuendeleza na kuibua vipaji kwa kufanya mashindano ambapo mshindi wa kwanza hadi watatu ndiyo watakaojinyakulia mipira hiyo.
“Nimetoa mipira hii ili iweze kuwaniwa na vijana kwenye wilaya ya Kibaha kwani mbali ya vipaji pia ni moja ya njia ya kuwajengea uwezo wa kujua wajibu wao katika kukitumikia chama,” alisema Chaurembo.
Alisema njia mojawapo ya kuwapata vijana ni kupitia michezo hivyo aliona kuna haja ya kuwaunganisha vijana kupitia michezo mbalimbali ambapo kwa sasa ameanza na soka.
“Mimi napenda sana michezo hivyo nimeona njia ya kuwaweka vijana pamoja ni michezo hivyo wazazi nao wanapaswa kuwaendeleza vijana wao kupitia michezo,” alisema Chaurembo.
Wakati huo huo katibu wa hamasa wa chipukizi Taifa Omary Moris ameahidi kutoa mipira 10 na jezi seti moja kwa chipukizi kwenye mkoa huo ili kuhamasisha michezo.
Moris alisema kuwa vifaa hivyo atavitoa baada ya wiki mbili kuanzia sasa ili vijana waweze kufanya michezo na kukuza vipaji vyao vya mpira wa soka.
Mwisho.    
  

HABARI PWANI


Na John Gagarini, Kibaha
VIKUNDI vya Ujasiriamali wilyani Kibaha mkoani Pwani vinakabiliwa na chanagamoto ya kutokuwa na akaunti jambo ambalo linasababisha fedha wanazopewa na wafadhili kutotumika kwa malengo waliyoziombea.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya ofisi ya mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka kukabidhi fedha na vifaa alivyoahidi kupitia fedha za mfuko wa Jimbo na binafsi kwenye kata mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya ziara hizo msaidizi wa mbunge huyo Method Mselewa alisema kuwa vikundi vingi bado havijaweza kufungua akaunti kwa ajili ya kutunza fedha zao hivyo fedha hizo huishia kugawana.
“Jambo la kwanza kabla ya kuwapa fedha tunawashauri kufungua akaunti ili fedha hizo zipitie huko kuliko kuwakabidhi fedha taslimu na endapo tunawapa mkononi basi huwa tunawashirikisha wanachama wote pamoja na uongozi wa serikali ya mtaa pamoja na chama ili kila mtu ashuhudie,” alisema Mselewa.
Alisema changamoto hii ni kubwa na endapo wanahitaji vifaa Fulani hawawapi fedha bali wanawapatia vifaa ili kuepusha fedha kutumia vibaya ikiwa ni pamoja na kugawana jambo ambalo liatawarudisha nyuma kimaendeleo.
 “Lengo la kutoa fedha na vifaa kwenye sekta mbalimbali ni kuchochea maendeleo ya wananchi kwa kuunga mkono miradi ambayo wao wameiibua na ni changamoto kwao,” alisema Mselewa.
Alivitaka vikundi vya ujasiriamali kuhakikisha kuwa vinakuwa na akaunti ili fedha zao ziweze kuwa salama kwa ustawi wa kiuchumi na maendeleo ndani ya jamii.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Tumbi Charles Kapama alimshukuru mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi zake kwa lengo la kuhamasisha maendeleo kwa wakazi wa Jimbo hilo. Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa ahadi za mbunge jumla ya kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 10 zimetumika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kibaha wametakiwa kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kwenye ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa mwaka 2014 na si kusubiri viti vya kuteuliwa ili kufikia lengo la 50 kwa 50.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini  Mwanaid Kiongoli alipokuwa akiongea na wajumbe wa baraza la utekelezaji la kata ya Kibaha.
Kiongoli alisema kuwa endapo kuna wanawake wanauwezo ni vema wakaungwa mkono na si kuwawekea ngumu ili waweze kuwania nafasi hizo za uongozi.
“Tusibweteke kwenye nafasi za kuteuliwa lazima nasi tujiamini kwa kuingia kwenye kinyanganyiro kwa wale wenye uwezo wa kuongoza kwani tumeshawezeshwa sasa na sisi tujitegemee kwa kuingia kwenye kinyanganyiro kuanzia 2014 hadi 2015 kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Kiongoli.
Aidha alisema kuwa wanawake wasiwakatishe tama wale wanaotaka kuwania nafasi za uongozi kwa kuwaunga mkono na wawe na upende na mshikamano kwani wao ndiyo wapiga kura wakubwa hivyo ni rahisi kuwachagua kuwa viongozi.
 “Huku tukijiingiza kwenye harakati za kuwnaia uongozi pia tukumbuke kuwa na miradi ya maendeleo hasa ile ya ujasiriamali ili kuweza kuziinua familia zetu na kuacha kubweteka na kutochangamkia fursa za kiuchumi,” alisema Kiongoli.
Aliwataka wanawake kuwa na umoja na kuacha kutengana na manunguniko ambayo hayataweza kuwasaidia kujikwamua na hali ngumu ya kimaisha kwani endapo watakuwa na miradi wataweza kuwasomesha watoto wao na kuwapunguzia mzigo akinababa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
CHIPUKIZI kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wametakiwa kuchagua viongozi bora na si kuchagua mtoto wa mkubwa fulani.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mwenyekiti wa Chipukizi Taifa Gabriel Amos Makala alipofanya ziara ya siku moja mkoani Pwani na kusema kuwa endapo watachagua watoto wa wakubwa wale wazazi wao ambao ni watu wachini hawataweza kupata fursa hiyo.
Makala alisema kuwa kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa chipukizi kila mtu bila ya kujali kuw ani mtoto wa nani ana haki ya kuwa kiongozi.
“Chagueni kiongozi ambaye atafaa kuongoza na si kuangalia huyu ni mtoto wa Fulani kuwa ndiye anafaa kuongoza hapan hiyo si sahihi kila mtu ana mwenye sifa anauwezo wa kuongoza hata Yule wa mkulima anaweza kuja kuwa kiongozi,” alisema Makala.
Alisema kuwa kinachohitajika ni mshikamano baina ya viongozi na wanachama na kuachana na makundi ambayo si mazuri ndani ya chama kwani yanakigawa chama na kusabnabisha wapinzani kupata nguvu hasa kipindi ch auchaguzi.
Kwa upande wake Omary Moris ambaye ni katibu wa hamasa chipukizi Tiafa na mjumbe wa kiamati kuu ya (CCM NEC) alisema kuwa kazi yake kubwa ni kuifufua chuipukizi ambayo kwa kipindi Fulani iliyumba.
“Chipukizi wakithaminiwa watalisaidia Taifa na wasiwe wanatumikia kipindi cha uchaguzi pekee kwani endapo wataandaliwa kwenye miradi wanaweza kuwa tegemeo kubwa kwa chama na Taifa kwa ujumla,” alisema Moris.
Aliwataka vijana kuwa na mshikamano kwani wao ndiyo tegemeo la nchi na waache kuwa na makundi ambayo hayatasaidia zaidi ya kuleta mifarakano.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WATANZANIA wametakiwa kuacha kulalamika juu ya baadhi ya mambo kutokwenda vizuri badala yake watoe ufumbuzi ya nini kifanyike kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (CCM NEC) kutokea Kibaha Mjini Rugemalila Rutatina, wakati wa hafla ya kuchangia ujenzi wa kituo cha afya cha kanisa la Living Weter Centre kinachojengwa Kilimahewa kata ya maili Moja wilayani Kibaha.
Rutatina alisema kuwa watu wamekuwa mahiri kulalamika kuwa jambo Fulani haliendi vizuri lakini hawatoi njia ya kufanyika ili jambo husika kwenda sawa.
“Tunalishukuru kanisa kwa kutoa jibu la changamoto ya huduma ya afya haya ndiyo watu wanapaswa kutoa majibu ya nini kifanyike na si kulaumu tu na hawa sasa baada ya kuona kuna tatizo la huduma hii wametoa suluhisho,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa ni kweli serikali inakabiliwa na chanagamoto nyingi lakini sekta binafsi nayo inatakiwa kushirikiana na wananchi ili kutoa majibu ya kero mbalimbali.
“Tunalipongeza kanisa kwa kuona chanagamoto hiyo katika kata ya Maili Moja ambayo haina kituo cha afya jambo ambalo linawafanya wananchi wa kata hiyo kupata huduma mbali na maeneo yao na nitatoa kiasi cha shilingi milioni 2 kuunga mkoni jitihada hizi,” alisema Rutatina.
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa hilo Paschal Mnemwa alisema kuwa alifikia uamuzi wa kujenga kituo cha afya baada ya kuona mama mjamzito akitaabika kwa kubebwa kwenye pikipiki kupelkwa hospitali umbali wa kilomita zaidi ya saba.
“Kitu kingine kilichonifanya nifikirie kujenga kituo cha afya kwa kushirikiana na waumini na wadau wengine ni kifo cha mtoto ambaye alikuwa akifika kanisani hapo kufariki baada ya kuzidiwa na homa na kabla ya kupata matibabu kutokana na umbali alifariki dunia,” alisema Mch Mnemwa.
Mch. Mnemwa alisema kuwa wanahitaji kiasi cha shilingi milioni 335 katika awamu ya kwanza ya ujenzi itakayochukua mwaka mmoja na hadi kitakapokamilika kitatumia zaidi ya shilingi bilioni 1.5 hadi sasa wametumia kisi cha shilingi milioni 40 ikiwa ni sadaka za waumini wa kanisa hilo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amelipongeza kanisa la Living Water Centre wilayani Kibaha kwa kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya ili kukabiliana na chanagamoto ya ukosefu wa huduma za kiafya kwenye kata ya Maili Moja.
Aliyasema hayo mjini Kibaha alipokuwa mgeni rasmi alipomwakilisha Naibu Waziri wa Fedha Janeth Mbene wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo hicho utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 335.
Koka alisema kuwa ni watu wachache ambao wamekuwa na maono kisha kuyafanyia kazi kwa lengo la kuisaidia jamii na kufikiri kuwa kila kitu kitafanywa na serikali.
“Hii ndiyo kazi ya Mungu kuisaidia jamii na serikali kwani kama tujuavyo mipango ya serikali ni mingi hivyo hata utekelezaji wake unachukua muda mrefu hivyo hawa wameonyesha njia ya kuwajibika hivyo lazima tuwaunge mkono kwa kazi nzuri,” alisema Koka.
Alisema kuwa kwa sasa kituo cha afya cha Mkoani kimeelemewa na wagonjwa na hospitali ya Tumbi baada ya kufanywa kuwa ya Rufaa imekuwa haichukui wagonjwa wa moja kwa moja hivyo ujenzi huu utasaidia kukabiliana na changamoto ya matibabu kwa wananchi wa Maili Moja na wilaya ya Kibaha.
“Hili ni jambo letu sote kwani mara kitakapokamilika kitapunguza msongamano kwani kwa sasa kituo cha Mkoani na Tumbi bado zinakabiliwa na changamoto kwani maandalizi ya kuwa kama inavyotakiwa yalikuwa bado hivyo changamoto ni nyingi,” alisema Koka.
Akielezea juu ya ujenzi huo Mchungaji wa kanisa hilo Paschal Mnemwa alisema kuwa maono ya kujenga kituo hicho kwa ushirikiano na wamuni yalikuja baada ya kuona wakazi wa kata ya maili Moja wakienda umbali mrefu kupata huduma za afya.
Alisema kuwa tayari wameshapata eneo na ujenzi umeshaanza ambapo tayari hadi sasa wameshatumia zaidi ya milioni 40 na wanahitaji kiasi cha shilingi milioni 335 kwa ajili ya awamu ya kwanza na hadi kukamilika zitatumika bilioni 1.5.
Koka aliahidi kuchangia kisi cha shilingi milioni 1.5, Profesa samweli Wangwe aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 2, mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Nec Rugemalila Rutatina aliahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 2 ambapo fedha taslimu ilikuwa milioni 70 na ahadi milioni 20.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Mwendapole Charles Beatus 31 Maarufu Ngoye amehukumiwa kwenda jela miaka 10 kwa kupatikana na hatia ya wizi wa Mtandaoni na kuaminiwa kiasi cha Milioni 7,610,000 za Gwelimo Wlfred mkazi wa Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Alihukumiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha HeriethMwailolo, baada ya mtuhumiwa kupatikana na makosa hayo mawili.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa chini ya Wakili wa Serikali Salim Msemo ilimkuta na hatia, ambpo kosa la kwanza mahakama ililezwa kuwa mnamo 3.5.2011 ni alihamisha fedha kiasi cha m 3,180,000 Kwenye akaunti ya mlalamikaji Gwelino Wilfred mkazi wa Kongowe.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alihamisha fedha hizo kutoka kwenye akaunti namba 2121606490 ya NMB kwa njia ya mtandao wa simu ya mkononi 0767122144 (Nmb Mobile) kwenda kwenye Akaunti yake namba 2031614880.
Kosa la iili ni wizi wa kuaminiwa kiasi cha shilingi milioni 4,430,000 hivyo kukutwa na hatia na baada mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo mahakama iliamuru alipe kiasi hicho lakini alishindwa na kulipa shilingi milioni 2,800,000 tu hivyo kushindwa kujinusuru na kuhukumiwa kwenda jela miaka 10.
Mwisho.