Na John Gagarini, Kibaha
MTAA wa Lumumba wilayani Kibaha unahitaji zaidi ya shilingi
milioni tisa kwa ajili ya kuweka nguzo tatu za daraja la mbao kwenye kivuko cha
mto Mpiji mpakani mwa wilaya ya Kibaha na Kinondoni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa mtaa
huo Gidion Tarimo alisema kuwa daraja hilo ni muhimu kwao kwa ajili ya kupata
mahitaji yao ya kila siku ambayo huyapata mtaa wa Kibwegere wilaya ya Kinondoni
Jijini Dar es Salaam.
Tarimo alisema kuwa wilaya ya Kinondoni kwao ni karibu
ukilinganisha na Kibaha Maili Moja hivyo daraja hilo linahitaji kufanyiwa
matengenezo ili liweze kupitika kwa urahisi hasa kupitisha magari mbapo kwa
sasa hayapiti.
“Tumeazimia kujenga daraja hilo hadi magari yaweze kupita
ambapo kwa sasa magari hayapiti hata hivyo tumepiga hatua kwani zamani watu
walikuwa wakipita mtoni moja kwa moja lakini kwa sasa hawagusi maji na maji
yalipokuwa yakijaa watu walikuwa hawawezi kuvuka kwenda ngambo ya pili,”
alisema Tarimo.
Alisema kuwa hadi kufikia hatua hiyo wametumia kiasi cha
shilingi milioni nane ambapo wananchi wamejitolea huku fedha za mfuko wa Jimbo
ni kiasi cha shilingi milioni mbili.
“Changamoto za matumizi ya daraja hili ni kubwa kwani ili mtu
upate huduma mbalimbali za kijamii lazima uvuke na kama kuna mamamjamzito
lazima ashushwe kwenye pikipiki ambazo hutumika hali ambayo si salama kwa
wagonjwa wa namna hiyo,” alisema Tarimo.
Aidha alisema kuwa tayari wameshapeleka barua kwa mkurugenzi
wa halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya kusaidiwa fedha kwa ajili ya
ujenzi wa daraja hilo.
Aliwaomba watu na mashirika mbalimbali kuwasaidia ili
kufanikisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2015 ili
kurahisisha mawasiliano na sehemu za huduma.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment