Sunday, May 26, 2013

DKT AISHI CHUMBA CHA KUZALISHIA



Na John Gagarini, Bagamoyo
 WANANCHI wa Kijiji cha Msinune kata ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba serikali kuwasaidia kujenga nyumba ya mganga ambaye anaishi kwenye chumba cha kuzalishia kwenye zahanati ya kijiji hicho.
Akizungumza mbele ya mbunge wa Jimbo la Chalinze Said Bwanamdogo wakati wa kikao cha Halamshauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Kiwangwa, mwenyekiti wa Kijiji hicho Kesi Hassan alisema mganga huyo inabidi afanye hivyo kutokana na kukosa nyumba.
Hassan alisema kuwa mganga pamoja na muuguzi wanatumia wanaishi humo kutokana na uhaba wa nyumba za watumishi katika kijiji hicho.
“Tunaiomba serikali na kwa kupitia kwako kutusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi kwani kutumia chumba kinyume na matumizi si sawa na haipendezi mazingira ni magumu,” alisema Hassan.
Aidha alisema kuwa watumishi wengi hawana nyumba za kuishi hivyo kuwapa wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuwahudumia wananchi.
“Suala la nyumba za watumishi ni changamoto ambayo inatukabili hivyo ni vema kukawa na nguvu ya ziada kutoka juu ili kutusaidia watumishi wetu waweze kukaa kwenye mazingira mazuri.
Kwa upande wake Bwanamdogo alisema kuwa suala hilo amelipata na ataangalia jinsi gani ya kuweza kulifanyia kazi ili mganga huyo na watumishi wengine waweze kuweza kuwa na nyumba.
Bwanamdogo aliwataka viongozi na wananchi kwenye vijiji vya Jimbo hilo kujitolea kwa kutumia nguvu zao ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za watumishi na ofisi yake itachangia.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment