Na John Gagarini, Bagamoyo
SHULE ya Msingi Ludiga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani
inakabiliwa na uhaba wa madarasa hali ambayo inasababisha baadhi ya wanafunzi
wa madarasa mawili kusoma chumba kimoja cha darasa huku wengine wakitakiwa
kulala ili wasisikilize wanachofundishwa wenzao.
Akizungumza mbele ya mbunge wa Jimbo la Chalinze Said
Bwanamdogo alipotembelea Kijiji cha Talawanda kata ya Talawanda, mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo Selestin Casian
alisema kuwa shule hiyo ina madarasa matatu tu.
Casian alisema kuwa mbali ya wanafunzi wa madarasa mawili
kusomea chumba kimoja pia wanafunzi wengine husomea nje kwenye miti kutokana na
upungufu huo wa vyumba vya madarasa.
“Inabidi tuwaambie wanafunzi wa darasa moja walale ili
wasisikilize kinachofundishwa na mwalimu ambaye yuko darasani hasa pale mwalimu
mwingine anapokuwa bado hajaingia,” alisema Casian.
Aidha alisema kuwa licha ya shule hiyo kuwa na mwaka wa 10
sasa tangu kuanzishwa kwake shule hiyo ina walimu watano ambapo ina jumla ya
wanafunzi 320.
“Kwa kweli tunachangamoto kubwa ya madarasa hali ambayo
inasababisha wanafunzi kutopatiwa elimu ipasavyo hivyo tunaiomba halmashauri
kutusaidia ili tuweze kuepukana na adha hii kwani wanafunzi wanashindwa kusoma
vema,” alisema Casian.
Kwa upande wake mbunge wa Bwanamdogo alisema kuwa atapeleka
suala hilo halmashauri ili iweze kutatua changamoto hiyo ambayo inakabili
baadhi ya shule za Jimbo hilo.
“Changamoto ya madarasa na walimu ni kubwa katika Jimbo la
Bagamoyo, lakini kama mnavyojua tatizo kubwa ni fedha kwani halmashauri yetu
haina fedha za kutosha hata hivyo tutaendelea kuhimiza ujenzi kwa kushirikiana
na wananchi,” alisema Bwanamdogo.
Aliitaka jamii kujitolea kwenye ujenzi wa madarasa na si
kuisubiri serikali kwani nayo inakabiliwa na mambo mengi ya kimaendeleo hivyo
wahimizane kuchangania kujenga madarasa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment