Friday, June 7, 2013

SUMATRA KUDHIBITI MADEREVA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Udhibiti wa usafiri Majini na Nchini Kavu (SUMATRA) imefungua ofisi yake mkoani Pwani na kuwataka wananchi kutoa taarifa za mabasi yanayokatisha ruti na kutotoa tiketi kwa abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ofisa mwandamizi wa SUMATRA wa mkoa Iroga Nashoni alisema kuwa abiria wanapaswa kukitumia chombo hicho ili kuondoa kero kwa wasafiri.
Iroga alisema kuwa ofisi hiyo imefunguliwa mwezi uliopita kwa lengo la kusogeza huduma kwa wateja wao ambapo inaendelea kujitanua kwenye mikoa, mingine ikiwa ni Singida, Iringa, Musoma na Rukwa.
Alisema kuwa changamoto kubwa waliyoiona ni mabasi mengi ya abiria kushindwa kumalizia safari zao Kukatisha Ruti) na kutotoa tiketi kwa abiria jambo ambalo ni kinyume cha sheria ambapo watawapiga faini hata ikibidi kuwafungia leseni madereva watukutu.
“Changamoto hiyo inakuwa kubwa kutokana na abiria wengi kutokuwa na elimu ya kujua haki zao za msingi wanapokuwa wanasafiri hivyo kuwapa mwanya madereva kufanya watakavyo,” alisema Iroga.
Aliongeza kuwa wataendelea kutoa elimu kwa pande zote ikiwa ni pamoja na abiria, madereva na wamiliki wa mabasi hayo ili waweze kufuata sheria bila ya kushurutishwa.
“Jana tulifanya operesheni kukamata magari yenye makosa mbalimbali ambapo magari manne yamekutwa na makosa na kupigwa faini kutegemea na makosa,” alisema Iroga.
Alibainisha kuwa wataendelea kufanya operesheni za kushtukiza za mara kwa mara ili kukabiliana na madereva wengi kukiuka sheria za barabarani na kuwataka wananchi kutoa taarifa na si kulalamika bali wachukue hatua.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment