Na John Gagarini, Kibaha
MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Abdul Ramadhan (35)
amewatapeli baadhi ya wakazi wa Kwa Mathias wilayani Kibaha mkoani Pwani kwa
kuwachimbisha kaburi kisha kutoweka na kuwaachia kaburi tupu bila ya kuzikwa
marehemu kama alivyowaomba azike ndugu yake.
Tukio hilo lilitokea juzi kwenye mtaa huo baada ya mtu huyo
kufika hapo na kuomba kusaidiwa kumzika mfanyakazi wake ambaye alidai kuwa hana
uwezo wa kumsafirisha kwani kwao ni mbali.
Mbali ya kuwachimbisha kaburi wakazi hao pia alifanikiwa
kuwaibia simu mbili pamoja na kamera moja pamoja na kuacha deni kwenye vyakula
ambavyo vilitumiwa na wachimba kaburi huku kingine kikiwa kimeandaliwa bila ya
kuliwa.
Akielezea mkasa huo Ustaadhi wa Masjid Kadiriya uliopo Kwa
Mathias Said Omary alisema kuwa mtu huyo alifika msikitini hapo na kukutana na
kiongozi kasha kuomba kuwa asaidiwe kuzikiwa mfanyakazi wake, msikiti
ukamkubalia na taratibu zikaanza kufanyika.
Omary alisema kuwa baada ya kuelekezwa na mkuu wake alitakiwa
ashughulikie suala hilo na kwenda na mtu huyo kwenye makaburi ya mambo akiwa na
watu wengine watatu kwa ajili ya kuchimba kaburi kwa ajili ya kumsitiri
marehemu.
“Tulikwenda makaburini na wachimbaji wakaanza kazi ya
kuchimba kaburi akawaletea chain a maandazi 20 wakanywa wakaendelea na kazi yao
mimi akaniambia twende hospitali ya Tumbi aliko marehemu kwa ajili ya kumwandaa,”
alisema Omary.
Alisema wakiwa njiani alimwambia kuwa anaomba simu yake ili
awasiliane na ndugu zake kwani ya kwake imeisha chaji pia amtafutie mpiga picha
kwa ajili ya tukio hilo kwa ajili ya kuwaonyesha ndugu juu ya mazishi hayo.
“Tulikwenda kwa mpiga picha wakakubaliana apige picha akasema
kabla ya kwenda Tumbi wakachukue nyama na vitu vingine kwa ajili ya msiba huo
na walipofika Maili Moja wakachukua nyama kilogramu 25 na,”alisema Omary.
Aliongeza kuwa wakati
wameshapima nyama aliwaambia ngoja akanunue viungo vingine lakini hakurudi tena
na kutoweka kusikojulikana huku kaburi likiwa limeshachimbwa na liko wazi hadi
sasa.
Kwa upande wake mpiga picha Jum Said ambaye yeye aliibiwa
kamera na simu alisema kuwa walikubaliana apige picha 36 hadi 40 ambazo gharama
yake ni sawa na shilingi 36,000 au 40,000.
Alisema wakati wako kwenye harakati ya kunua nyanya
alimwachia begi likiwa na kamera na simu lakini aliporudi hakumkuta akiwa yeye
na Ustaadhi na dereva wa teksi ambayo aliikodisha kwa shughuli za mazishi hayo.
“Alituacha mimi na ustaadhi tukiwa na nyama huku tukimsubiria
hali amabyo ilitufanya tuingie matatani kwani wauzaji nyama ilibidi watubana
ndipo tulipowaelewesha juu ya hali halisi ndiyo ikawa salama kwetu na kuondoka,”
alisema.
Watu waliokumbwa na hali hiyo walisema kuwa mbali ya
kudanganya mambo yote hayo pia aliweka oda ya chakula sahani 20 kwenye hoteli
lakini hakuonekana tena, katika kufuatilia walibaini jina la mtu huyo kwani
siku moja kabla ya tukio hilo alilala kwenye nyumba ya kulala wageni ya Iwawa
iliyopo mtaa wa Kwa Mbonde jirani na hapo wakazi hao walitoa taarifa kwenye
kituo cha polisi Kwa Mathias juu ya tukio hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment