Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Halima Kihemba
amewataka wananchi kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi uliopo kwenye mtaa wa
Mtakuja kulimaliza suala hilo na mmiliki wa eneo hilo kwani yeye hawezi
kulitolea maamuzi eneo la mtu ambaye ana hati miliki.
Aliyasema hayo jana kwenye mtaa huo ambako baaadhi ya
wananchi kuingia kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa hekari zaidi ya 100 kisha
kujenga makazi, mali ya Mohamed Suma na kusababisha mgogoro mkubwa.
Kihemba alisema kuwa licha ya kukaa vikao mbalimbali juu ya
eneo hilo ambapo watu zaidi ya 600 wameingia kwenye eneo hilo bila ya mmiliki
kuwaruhusu kwani alitoa eneo lenye ukubwa wa hekari 16 kwa watu nane tu.
“Nimekuwa nikipata barua nyingi toka kwa kamati ya
kushughulikia suala hili wakinitaka nitoe tamko juu ya eneo hili kwani mwenye
maamuzi ya eneo hili ni mmiliki mwenyewe na mimi sina uwezo wa kusema lolote,”
alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa anashangaa kwamba kama watu hao walipewa
bure na baadhi ya viongozi wa mtaa basi waliachie waondoke ni kwanini hawataki
kuondoka kama wanataka wafuate sheria kwani anashangaa kuona licha ya kuambiwa
wasiendeleze lakini watu wamejenga na wengine wanaendelea na ujenzi.
Mmoja ya wananchi waliouziwa viwanja kwenye eneo hilo Kandege
Jafar alisema kuwa wanashangaa halmashauri kuweka matangazo ya kuwataka
waondoke ili hali mmiliki mwenyewe alisema kuwa atakapokuja atatoa muafaka wa
nini kifanyike.
Jafar alisema kuwa kutokana na hali halisi ilivyo yeye mkuu
wa wilaya awasaidie kwani endapo wataendelewa watakuwa wamepata hasara kubwa Kutokana
na kuyaendeleza maeneo hayo hivyo ni vema akawasaidia.
“Mkuu wa wilaya sisi tunaomba utusaidie hebu angalia umati
wote huu tuko hapa hatujui hatma yetu tunaomba utusaidie ili tusipate haki zetu
kwani haitapendeza watu wote kuona wakitaabika bila ya sababu za msingi,” alisema
Jafar.
Naye mwenyekiti wa awali wa mtaa huo ambaye ndiye aliyekuwa
akisimamia eneo hilo Longino Kasonta alikanusha kuwa aliwauzia wananchi hao
maeneo alisema kuwa yeye aliambiwa atoe eneo lenye ukubwa wa hekari 16 kwa watu
nane lakini watu wengine yeye hausiki.
“Mimi ndiye niliyeagizwa na mmiliki wa shamba hili nigawe
viwanja 16 kwa watu nane ambapo kila mmoja hekari mbili, lakini viongozi wa
mtaa nao wakaendelea kuwagawia watu maeneo hadi watu kufikia 600,” alisema Kasonta.
Kasonta alisema kuwa baadhi ya watu walivamia shamba hilo na
kuanza kuuza maeneo mengine hasa ikizingatiwa shamba hili ni kubwa sana hivyo
watu wanampakazia kuwa yeye kawauzia maeneo jambo ambalo si la kweli.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment