Sunday, July 7, 2013

HABARI ZA PWANI



Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amepongeza utaratibu wa viongozi wa dini za kikristo kufunga siku 40 kwa ajili ya kuombea amani ya nchi ili iweze kuondelea baada ya kutokea matukio yaliyokuwa yakiashiria uvunjifu wa amani.
Akizungumza juzi na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali na uongozi wa jeshi la polisi mkoani humo, alisema kuwa jambo wanalolifanya ni kubwa na linapaswa kuungwa mkono na wapenda amani.
Mahiza alisema kuwa siku za hivi karibuni kulitokea matukio makubwa ya uvunjifu wa amani hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutokea milipuko ya mabomu mkoani Arusha ambapo watu kadhaa walipoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa.
“Tukikumbuka hata kule Kusini mkoani Mtwara zilizuka vurugu kubwa ambazo nazo matokeo yake hayakuwa mazuri kwani watu kadhaa walipoteza maisha na mali huku wengine wakijeruhi hivyo kuna haja ya kuwa na mkakati wa kukabilina na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuiombea nchi amani,” alisema mahiza.
Aidha alisema kuwa amani kuipoteza ni rahisi lakini gharama ya kuirudisha ni kubwa sana hivyo lazima kila mtu aangalia ni namna gani anaweza kunusuru hali hiyo.
“Tunaunga mkono jitihada za viongozi wa dini kuamua kufunga na kufanya maombi maalumu ili kuinusuru nchi yetu ili isiingie kwenye machafuko ambayo mara nyingi husababisha vifo na watu kushindwa kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Mahiza.
Alisema kuwa sehemu yoyote yenye machafuko maendeleo hakuna hivyo kuna kila sababu ya kuiombea nchi ili iepukane na hayo yanayotaka kujitokeza.
Kwa upande wake katibu wa umoja wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Pwani Mchungaji Gervase masanja alsiema kuwa endapo amani itatoweka hata uhuru wa kumwabudu mungu hautakuwepo.
“Baadhi ya watu wameingiza siasa makanisani jambo ambalo linaweza likawa chanzo cha vurugu hivyo tunawaomba waumini wasiiingize siasa kwenye sehemu za kuabudia kwani ni hatari na ndiyo sababu ya sisi kuamua kufunga kuombea amani iliyopo isivunjike,” alisema Mch Masanja.
Kikao hicho pia kiliwajumuisha wakuu wa wilaya, wakuu wa polisi wa wilaya, vyama vya siasa, vyama vya watu wenye ulemavu na watu maarufu ndani ya jamii kwenye mkoa huo.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) mkoa wa Pwani imekunjua makucha yake baada ya kumtaka kondakta wa basi la kampuni ya Mbazi kuwarudishia nauli waliyoizidisha tofauti na ile iliyopangwa na serikali.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki kwenye stendi ya maili Moja wilayani Kibaha baada ya abiria kulalamika kuwa wamezidishiwa nauli wakati wakikata nauli kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Kondakta wa basi hilo ambalo linafanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Arusha alijikuta matatani baada ya basi lake kuzuiliwa na kurejesha nauli ambazo zilikuwa zimezidi kwa abiria 19.
Baadhi ya abiria ambao waliongea na waandishi wa habari kuhusiana na kuzidishiwa nauli kati yao ni Nagi Nurdin aliyekuwa akienda Moshi alisema kuwa yeye alikatiwa nauli kwa shilingi 29,000 badala ya shilingi 22,700 ambapo alikata kwenye ofisi za basi hilo.
Naye Forida Faustin alisema kuwa yeye naye alikuwa akienda Moshi alitozwa 33,000 huku YUda Nduti akitozwa 30,000 ambapo walianza kumtajia nauli ni shilingi 40,000.
Kwa upande wake ofisa mfawidhi wa SUMATRA Pwani Iroga Nashon alisema kuwa hatua ya kwanza waliyoichukua ni kumwamuru kondakta wa basio hilo lenye namba T 600 APN kuwarejeshea nauli zilizozidi abiria hao.
“Baada ya kurejesha nauli zilizozidi ambazo zilikuwa ni zaidi ya 300,000 pia tuliwapiga faini ya shilingi 250,000 kwa kosa hilo kwa kuzingatia kifungu cha sheria cha 34 na ndipo tuliporuhusu basi hilo kuendelea na safari yake,” alisema Nashon.
Kwa upande wake kondakta wa basi hilo hakuwa tayari kuzungumza na waandishi na kusema kuwa yeye siyo msemaji ambapo alidai abiria hao walikatiwa tiketi stendi ya Ubungo.
Nashon aliwataka abiria kutoa taarifa kuhusiana na wamiliki au makondakta na madereva kuwanyanyasa kwa makusudi huku wakijua sheria za uendeshaji wa mabasi hayo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wanaokiuka.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari la kunyanyulia vitu vizito (Crane) ikiwemo magari yanayoharibika kwenye barabara za mkoa huo.
Chanagamoto hiyo ilionekana juzi baada ya magari kukwama kwa zaidi ya saa tano baada ya magari mawili kuharibika kwenye daraja linalounganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam eneo la Kiluvya wilayani Kibaha.
Magari yaliyoharibika ni ya mizigo ambapo la kwanza ni Scania namba T 503 DTJ na Fuso lenye namba za usajili T 515 DSA magari haya yaliziba kabisa barabara hivyo kusababisha magari kushindwa kuingia wala kutoka kwa muda huo.
Akizungumza kwenye eneo la tukio hilo kamanda wa polisi wa kikosi cha usalama barabarani wa mkoa huo Nasoro Sisiwaya alisema kuwa ilibidi watumie nguvu ya ziada kuliondoa gari moja ili magari yaweze kupita kwani lori kubwa liliharibika katikati ya daraja la mto Mpiji.
“Kwa kweli gari la kunyanyua vitu vizito ni changamoto kubwa kwani magari yanayo anguka au kupata ajali yanashindwa kuondolewa kwa wakati kutokana na kukosa huduma ya gari hilo,” alisema Sisiwaya.
Sisiwaya alisema kuwa tayari wameshaiomba serikali na wakala wa barabara TANROADS ili wanunue gari hilo na liwe hapa Kibaha kwani kutegemea litoke Dar es Salaam ni tatizo kubwa.
“Tumeandika sehemu husika kuomba gari hilo ili kukabiliana kwani tukio hili limesababisha usumbufu mkubwa sana kwa magari yanayopita barabara hii ya Morogoro ambayo ndiyo mlango wa kuingilia na kutoka Dar es Salaam.
Aidha alisema wataiomba TANROADS kujenga barabara mbadala kwani kutegemea barabara moja ni tatizo kubwa na kutokana na tukio hili tumeona jinsi gani watu walivyohangaika na kusababisha usumbufu mkubwa.
Mwisho.    

No comments:

Post a Comment