Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametoa ofa ya kuwalipia gharama za mafunzo ya madereva wapya wa pikipiki maarufu kama (Bodaboda) ili kila mmoja awe na leseni.
Koka alitoa ofa hiyo jana alipokuwa akizungumza na madereva na wamiliki wa pikipiki, mbele ya mkuu wa wilaya ya Kibaha, uongozi wa halmashauri, maofisa wa mamlaka ya mapato (TRA) na jeshi la polisi mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa ameamua kujitolea kuwasaidia madereva wote wapya wa Bodaboda ili wawe na leseni ili wajue kanuni na taratibu za barabarani kwani wengi wao hawana leseni hali inayosababisha ajali nyingi kutokea.
“Lengo langu ni kutaka mfanye kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani kwani ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na baadhi yenu kutokuwa na leseni kwani wanakuwa hawajapata mafunzo ya matumizi sahihi ya sheria wawapo kazini,” alisema Koka.
Aidha alisema kuwa vijana wamejiajiri kwenye uendeshaji wa pikpiki hivyo lazima wajengewe mazingira mazuri ya kufanyia kazi ili wasipate buguza.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima kIhemba aliwataka madereva hao kuzingatia sheria ili kuepukana na ajali ambazo si za lazima ambazo zinasababisha kupoteza maisha au viungo kwa wateja wao au wao wenyewe.
Kihemba pia aliwataka wawe walinzi wa amani na kukabiliana na vitendo vya uhalifu kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiwatumia kwenye vitendo vya kihalifu na vitendo vya vurugu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment