Na John
Gagarini, Kibaha
MASHIRIKA na
taasisi za biashara zimetakiwa kurejesha faida kwa jamii wanayoihudumia na si
kutaka faida pekee ili nao wafaidi uwepo wa vyombo hivyo.
Hayo yalisemwa
jana mjini Kibaha na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry
Koka wakati akitoa salamu zake wakati wa kukabidhi madawati 50 kwenye shule za
Msingi Jitihada na Lulanzi zilizopo wilayani Kibaha, madawati hayo yaliyotolewa
na kampuni ya kutoa mikopo ya Faidika.
Koka alisema
kuwa makampuni hayo kwa kuwa yanahudumia jamii lazima yatoe mrejesho kwa
kusaidia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
“Mashirika haya
yasitake kupata faida tu lazima nayo yachangie jamii ili iondokane na changamoto
zilizopo kwa kutoa sehemu ya faida wanayoipata katika shughuli zao,” alisema
Koka.
Alisema serikali
inapaswa kuyaangalia makampuni hayo ambayo yanafanyabiashara kwa jamii ili nayo
yatoe sehemu ya faida kwa wananchi kwani mafanikio wanayoyapata ni kutokana na
mapato yawananchi hao.
“Lazima nayo
yaone umuhimu wa kusaidia jamii kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na
afya, maji, elimu na zinginezo kwa kuzipatia ufumbuzi,” alisema Koka.
Kwa upande
wake mwakilishi wa kampuni ya Faidika Harun Zuberi alisema kuwa kampuni yake
mbali ya kutoa mikopo kwa watumishi pia imeweka mkakati wa kurudisha faida
wanayopata kwa kuisaidia jamii.
“Tumekuwa
tukisaidia sekta mbalimbali ambapo kwa sasa tumeamua kuisaidi sekta ya elimu
kwani tunaamini serikali peke yake haiwezi lazima ishirikiane na wadau ndiyo
sababu ya sisi kutoa misaada,” alisema Zuberi.
Zuberi
alisema kuwa wameona umuhimu wa kuchangia kwenye sekta ya elimu ili kuhakikisha
kuwa wanafunzi wanasoma wakiwa kwenye mazingira mazuri naya kuvutia kwani
mazingira ya baadhi ya shule ikiwemo vifaa imekuwa ni tatizo kubwa.
Kwa upande
wao walimu wa shule hizo Elizabeth Daniel na Anna Bilal waliipongeza kampuni
hiyo kwa kujitolea kusaidia tatizo hilo ambalo ni changamoto kubwa kwa shule
zao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment