Na John Gagarini, Kibaha
MAOFISA wa serikali kwenye Idara ya Mifugo wametakiwa
kutumia uzalendo wakati wa kuingiza madawa ili kuepuka kuingizwa madawa yasiyo
na viwango.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mwakilishi wa kitaifa wa
kampuni ya Laprovet ya nchini Ufaransa Ephrahim
Massawe alipoongea na waandishi wa habari na kusema kuwa baadhi ya maofisa hao
wamekuwa wakiingiza madawa yasiyo na viwango.
Massawe alisema kuwa kutokana na kuagizwa madawa yasiyo na
viwango kumesababisha madhara makubwa kwa mifugo ikiwa ni pamoja na kufa hivyo
wafugaji kupata hasara kubwa.
“Kufa kwa mifugo kunatokana na magonjwa mbalimbali hapa
nchini kunatokana na baadhi ya madawa kuwa kwenye kiwango cha chini hivyo
kushindwa kuzuia au kutibu magonjwa yanayokabili mifugo,” alisema Massawe.
Aidha alisema kuwa tatizo kubwa ni ubadhirifu na kutokuwa na
uadilifu kwa maofisa hao hali ambayo inasababisha mifugo mingi kufa kwa kupata
matibabua ambayo hayalingani na uwezo madawa hayo toka nje ya nchi.
“Maofisa hao baadhi yao si waaminifu kwa kuingiza madawa
ambayo hayana viwango licha ya kuwa madawa mazuri yapo hasa baada ya kuingia
soko huria, hivyo wasiangalie maslahi binafsi bali waangalie utu na uzalendo
kwa nchi yao,” alisema Massawe.
Massawe ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa waganga wasaidizi
wa mifugo nchini (TAVEPA) alisema kuwa endapo maofisa hao watakuwa waadilifu
watasaidia kuboresha kipato cha wafugaji.
Alibainisha kuwa ili kuhakikisha wafugaji wanajua matumizi
sahihi kampuni hiyo inatoa mafunzo pamoja na ushauri wa namna ya ufugaji wa kisasa
ili kuongeza tija kwani ufugaji ni mkombozi wa nchi kwani inaliingizia pato
kubwa la Taifa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani imeanza mkakati wa
kukabiliana na uchafu kwenye Mji huo mkongwe hapa nchini kwa viongozi kushiriki
kwenye zoezi la usafi kila mwanzo wa mwezi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mkuu wa
wilaya hiyo Ahmed Kipozi alisema kuwa mkakati huo una lengo la kuwapa hamasa
wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya usafi.
Kipozi alisema kuwa tayari mkakati huo umeshaanza kwa
viongozi wa wilaya, halmashauri, kata, mitaa na wananchi kufanya usafi kwenye
mji huo pamoja na maeneo wanayoishi.
“Usafi bado ni changamoto kubwa kwa wakazi wa Bagamoyo lakini
tunajaribu kuwaelimisha wananchi kuona umuhimu wa kusafisha mazingira yao
yanayowazunguka na tumeshaanza kuona mabadiliko na mji umeanza kupendeza,”
alisema Kipozi.
Alisema kuwa pia wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya
kuhifadhia takataka kwenye maeneo mbalimbali ya mji huo lakini watahakikisha
kuwa wanaweka vifaa hivyo ili wananchi wasikose sehemu ya kuhifadhia uchafu.
“Kikubwa tunachoomba ni ushirikiano kwa wananchi ili kuweza
kufanikisha usafi kwenye mji wetu ambao ni wa kihistoria na unabeba historia
kubwa ya nchi hii hivyo lazima uendane na hali hiyo kwa kuwa kwenye hali ya
usafi,” alisema Kipozi.
Alisema kuwa kwa kuwa mji huo tayari umepewa hadhi ya kuwa
mji mdogo hivyo lazima usafi uzingatiwe na watatumia sheria ndogondogo za mji
ili kukabiliana na wale wote ambao watakuwa wanakwenda kinyume na kanuni za
usafai.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment