Tuesday, July 23, 2013

MATUKIO PWANI

Na John Gagarini,Kibaha

HALMASHAURI ya Kibaha mjini Mkoani Pwani imeanza mchakato wa tathmini ya kutekeleza miradi ya soko pamoja na stendi ya kisasa zitakazojengwa kwenye eneo la kitovu cha Mji huo kilichopo mkabara na barabara kuu ya Morogoro.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kibaha Adhudadi Mkomambo alisema kuwa huo ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo iliwekewa mkakati mwaka wa fedha wa  2010-2011 ambapo upembuzi upembuzi yakinifu unatarajia kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mkomambo alisema kuwa wameshaingia ubia na banki ya rasilimali (TDB) ambayo ndio itakayosaidia kufanikisha gharama za ujenzi kwa ushirikiano na halmashauri hiyo.

“Taratibu zilizopo sasa ni kufanya tathmini ya uhakika ya gharama za miradi hiyo kabla ya Desemba mwaka huu kisha zoezi la ujenzi litaanza mara moja baada ya tathmini kupatikana,” alisema Mkomambo.

Alibainisha kuwa stendi hiyo itakuwa na uwezo wa kuegesha magari 50 kwa wakati mmoja na upande wa soko la  kisasa litakalokuwa na eneo la soko la kawaida litakalohusisha wakulima wadogowadogo,na soko la kisasa litakalovutia wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri amebainisha kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza mapema mwakani na kutarajiwa kukamilika mwaka 2015-2016 na litatumia heka Tisa.
Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha
KAMANDA wa Jumuiya ya vijana (UVCCM) wilaya ya kibaha Mjini Mkoani Pwani Silvestry Koka amesema kuna kila sababu ya kuendelea kuimarisha chipukizi ndani ya chama ili kuwajenga vijana na watoto wakue kwa misingi ya kizalendo.

Akifungua mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa Chipukizi wilayani humo, alisema tangu enzi za waasisi wetu walitambua kwa kuweka taratibu ya kuwa na chipukizi kutokana na kuwa  nguzo kwa maslahi ya chama na Taifa.

Koka alisema kuanzia sasa atahakikisha anakuwa mlezi wa kutatua changamoto za chipukizi wilayani humo ikiwa ni sanjali na kuwawezesha kwenye mafunzo mbalimbali, michezo ili kuwalinda na kuwapa motisha .

matokeo ya uchaguzi huo Katibu wa UVCCM kibaha mjini Khalid King alisema viongozi hao wapya wataongoza kwa kipindi kingine cha mika mitatu.

King alimtaja Shadya Ibrahim kuwa ni Mwenyekiti wa chipukizi aliyepata kura 74 baada ya kumshinda mpinzani wake Imran Mohamed aliyepata kura 58.

Katika  nafasi ya Mjumbe wa mkutano mkuu wa chipukizi  ngazi ya mkoa amechaguliwa Jesca Mkenda , mwakilishi wa mkutano mkuu wa Wilaya ikishikiliwa na Zainabu Mpemba ,na nafasi ya kamati ya uendeshaji ya Chipukizi ngazi ya Wilaya ni Joseph Ernest,Marwa Mwise na Neema Ahmed .
 Mwisho

 Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI wa Skauti nchini wametakiwa wametakiwa kuzingatia uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao ya kikazi ili kuiletea nchi maendeleo na endapo watakwenda kinyume na taratibu watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nyadhifa zao.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Skauti mkuu wa Tanzania Mwantumu Mahiza alipokuwa akimwapisha kamishna mkuu wa Skauti Abulkarim Shah na kusema kuwa sifa kuu ya skauti ni uadilifu.

Mahiza alisema kuwa  ili kiongozi aaminike na jamii  ni lazima aonyeshe  juhudi, weledi uamnifu na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa jamii na anapaswa kuhakikisha chama kinarudi kwenye mstari na sitasita kumwondoa kiongozi anayeshindwa kutimiza majukumu yake kama katiba inavyosema ili kujenga heshima ya chama hicho ndani na nje ya nchi,” alisema Mahiza.
  
Aidha alibainisha kuwa hatutakuwa tayari kufanyakazi na baadhi ya viongozi walioonekana kupoteza sifa ya chama hicho na badala yake wale wote waliohusika kukipunguzia sifa watabaki kuwa wanachama na kazi ya uongozi tutaendelea na wachache wanaokidhi vigezo.
 MWISHO.
  
Na John Gagarini, Kibaha
MAHAKAMA ya hakimu Mkazi Kibaha Mkoa wa Pwani imemuhukumu  mkazi wa Miembe Saba wilayani Kibaha Amosi Chacha (40)  kwenda jela miaka 6 baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya Wizi wa vocha za mtandao wa simu za Tigo pamoja na kukutwa na mihuri bandia.

Mtuhumiwa huyo alikutwa na hatia kwa makosa yote mawili yaliyokuwa yakimkabili Katika kesi iliyokuwa ikisikilizawa na Hakimu Mkazi,  Aziza Mbadyo.

Mwendesha mashitaka wa Serikali  Emmanuel Maleko  ameieleza mahakama kuwa mtuhumiwa  huyo alikutwa akiwa na Mihuri ya Afisa Mtendaji Mtaa wa Kwesimu pamoja na wa Kituo cha Ukaguzi wa Maliasili cha Soni kilichopo Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga mnamo tarehe 03 Juni 2013 huko eneo la Sinza Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mihuri hiyo katika usafirishaji wa mali asili kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam kwa lengo la kuweza kuvuka vizuizi vya mali asili vilivyopo kwenye barabara kuu.

Aidha Maleko alieeleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Kibaha Mkoa wa Pwani akiwa na vocha za muda wa hewani za kampuni ya simu ya Tigo zenye thamani ya Tsh. 5,000,000/= akizisafirisha kwenda Tanga akitokea Dar es Salaam.

Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali aliongeza kuwa makosa yote hayo mawili aliyokutwa na hatiya dhidi yake,  Chacha anadaiwa kuyatenda kwa nyakati tofauti.

Akisoma hukumu hiyo kwa muda wa saa moja na nusu, Mbadyo alisema kuwa Mahakama imeridhika na maelezo ya upande wa Jamhuri hivyo imemtia hatiani Amosi Mwita Chacha kwenda Jela miaka sita ambapo katika kosa la Wizi wa vocha za Tigo alihukumiwa miaka minne na kosa la Kukutwa na Mihuri bandia alihukumiwa miaka miwili  hivyo adhabu zote mbili zitakwenda pamoja na atatakiwa kwenda Jela miaka sita.

Na John Gagarini, Kibaha
 MKAZI wa kijiji cha Nyanduturu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Ally Makakatau (46) amepoteza maisha baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kukatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishana Msaidizi wa Jeshi la Polisi Juma Ally alisema kuwa  tukio hilo lilitokea Julai 19 majira ya saa 7:30 usiku baada ya watu wapatao sita kuvamia nyumbani kwa Makakatua na kuvunja mlango wa nyumba aliyokuwemo kisha kumshambulia kwa kutumia mapanga kichwani, mkononi na miguuni.

Ally alisema kuwa watu hao walivamia katika nyumba hiyo na kumtaka marehemu kuwapatia pesa ambazo alikuwa amepata baada ya mauzo ya mafuta aliyokuwa amefanya jioni ya siku hiyo na alipokataa kutoa ndipo waliamua kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili.

“Watu hao mbali ya kuvunja  nyumba ya mfanyabiashara huyo, pia walivunja duka na kuchukua pesa taslimu shilingi m 2,800,000 ambazo zilikuwa ni za mauzo ya mafuta,” alisema Ally.   

Aliongeza kuwa Jeshi la linawasaka watu hao na kuwataka wanachi kuwapatia taarifa zitakazo saidia kuweza kuwapata waliohusika na tukio hilo.

Aidha alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa Daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Katika tukio lingine, JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu ishirini (20) raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchi bila kibali.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:30 usiku eneo la Mkuranga Mjini Wilaya ya Mkuranga.

Kaimu Kamanda huyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watu hao walikamatwa na askari waliokuwa doria wakiwa wanatembea makundi makundi  katika eneo la Mkuranga Mjini.

Alifafanua kuwa watu hao baada ya kuwahoji walibaini kuwa walishushwa kwa gari na kuamua kutembea ili kuweza kuvuka kwenye eneo lililokuwa na kizuizi cha Polisi.

Aliwataja raia hao wa Ethiopia waliokamatwa kuwa ni Habtamu Ambesi (21), Yesak Mishamo (19), Biuk Moltumo (20), Apepe Eshetu, (20), Mesfin Taddes, (20), Debero Shenke, (20), Teamat Kesse, (18), Gerenu Debere, (20), Tofek Anshabo, (25), Lomabebo Gahtchowo, (20) na Asle Mugoro, (20).

Wengine ni Chakiso Eriso, (20), Wondimu Birhanu, (18), Mulatu Menuru, (22), Gezahegn Lire, (21), Tileahnu Desta (20), Muly Geta (21), Abdi Mohamed (22), Ali Lonsako (25), Johann Bincebo (20), Degnat Tesema (16), Femasene Fitamo (17) na Temaggne Kebeda (25).

Aidha Ally alisema pia Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata John Kataraya (50) mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam ambaye alikuwa akiwasafirisha Waethiopia hao.

“Rai hawa waliingia nchini kwa kutumia njia ya usafiri wa gari kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kusini ili kuweza kwenda nchi jirani ya Msumbiji na watakabidhiwa kwa idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria,” alisema Ally

Aidha, aliwataka wanachi waendelee kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wanapowatilia mashaka wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.
Mwisho


No comments:

Post a Comment