Saturday, July 27, 2013

DEREVA BODABODA AFA KWA KUJINYONGA

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

tweeterMWENDESHA aliyetambulikia kwa jina moja la Omary (25) mkazi wa mtaa wa Lumumba wilayani Kibaha mkoani Pwani amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwenye mkorosho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa huo Gidion Tairo amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 25 mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi.

Tairo amesema kuwa mwaili wake ulikutwa ukiwa unaninginia huku akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya Manila huku pembeni yake kukiwa na chupa ya bia aina ya Safari.

Amesema mwili huo uligunduliwa na moja ya majirani zake ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja amabaye alitoa taarifa kwake na yeye kuwasiliana na polisi.

Aidha amesema marehemu ambaye alikuwa akifanyia shughuli zake Kibamba CCM wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam kabla ya mauti kumkuta alikuwa haonekani nyumbani na hakuonekana kuwa na matatizo yoyote.

Amebainisha kuwa marehemu alikuwa akiishi kwenye nyumba na Roja Kwayu wa Jijini Dar es Salaam na ndiye alikuwa akiisimamia nyumba hiyo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Pwani Ulrich Matei amesema kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote.

Matei amesema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo ili kujua nini chanzo cha kifo chake, na mwili huo umehifadhiwa kwenye hospitali ya Tumbi kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi, baada ya uchunguzi wa daktari.

Mwisho.






No comments:

Post a Comment