Sunday, August 4, 2013

HABARI ZA MKOA WA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha

HALMASHAURI ya Mji Kibaha mkoani Pwani imesema kuwa haijarudisha hazina fedha za ujenzi wa barabara kiasi cha shilingi milioni 700 bali fedha hizo zilichelewa kutumika kutokana na makandarasi kukiuka taratibu za ujenzi.

Hayo yalisemwa jana na mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo Adhudadi Mkomambo, kwenye kikao cha madiwani kilichofanyika mjini Kibaha.

Mkomambo alisema kuwa kwenye kikao cha bunge kilichopita waziri wa ujenzi John Magufuli alisema kuwa mji huo umeshindwa kutumia fedha hizo kwanini waombe fedha nyingine.

“Licha ya Halmashauri kupata mafanikio makubwa kwa mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na kuweza kukusanya fedha kiasi cha zaidi ya bilioni moja changamoto kubwa ni ya makandarasi wa barabara kushindwa kazi hivyo kushindwa kulipwa kwa wakati,” alisema Mkomambo.

Alisema kuwa matatizo mengi ya kihandisi kwani baadhi yao walioomba kazi hawajasajiliwa na wengine wametumia hati feki kupata kazi hizo licha ya kwamba mchakato wa kuwapata ulizingatia taratibu za kihandisi.

“Fedha hizi tunatarajia ifikapo Septemba 30 tutakuwa tumezifanyia kazi fedha hizo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa ya kuboresha barabara za mji wetu ambao kwa sasa ndiyo unajengeka,” alisema Mkomambo.

Aidha alisema kuwa fedha hizo zipo na hazijarudishwa hazina tutahakikisha kuwa halmashauri inafanya tathmini ya hali ya juu kuwapata makandarasi bora ili kuachana na wakandarasi feki.

Aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi ili waweze kuwaletea maendeleo kwani bila ya wao kuwa na uchungu hawataweza kuwafikisha kwenye maisha bora.

Mwisho.

Na John Gagarini, Bagamoyo

MEYA wa Mji wa Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu amewataka waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu mkoani Pwani waungane katika kipindi hichi cha mfungo kuiombea nchi ili isiingie kwenye mgawanyiko wa kiimani.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akitoa chakula cha futari kwenye shule za sekondari za Kimange, Changarikwa, Lugoba, Wazee wa CCM wa kata ya Lugoba na kata ya Miono wilayani humo.

Sharifu alisema kuwa viongozi na waumini wa dini wana nafasi kubwa ya kuweza kuhakikisha kuwa nchi ina amani kwa kufanya maombi ikiwa ni pamoja na kufunga.

“Nawaombeni waumini na viongozi wa dini zote kuliombea Taifa ili lisiingie kwenye machafuko ambayo yatasabisha amani kutoweka hivyo watu na nchi kushindwa kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Sharifu.

Meya huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo alisema kuwa mbali ya viongozi wa dini na waumini kufanya maombi maalumu pia viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa nao wanapaswa kutochochea uvunjifu wa amani.

“Endapo nchi itaingia kwenye machafuko hakuna kitakachoweza kufanyika kwani watu hawataweza kusali hata hao wanasiasa hawataweza kufanya siasa hivyo ni vema wanasiasa nao wakafanya siasa ambazo hazitaleta chuki na kuwagawa watu kutokana na itikadi za dini na siasa,” alisema Sharifu.

Aidha alisema kuwa watu wanapaswa kuheshimu mamlaka zilizopo na kushangazwa na baadhi ya wanasiasa kuchochea vurugu hali ambayo si nzuri kwani vita ikitokea athari hazitaangalia chama, dini wala rangi.

Aliwataka Watanzania kutokubali kugawanywa kwani endapo watakubali hali hiyo kuingia nchini itasababisha watu waishi kwenye hali ngumu na kushindwa kuwa na amani ambayo iko kwa sasa.
Mwisho.

Na John Gagarini, Kisarawe

BAADHI ya wakazi kutoka mikoa mbalimbali wamevamia msitu wa hifadhi wa Ruvu Kusini na kufanya uharibifu mkubwa kwa kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na mbao kwenye maeneo mbalimbali ya vijiji kikiwemo Kijiji cha Mtamba wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kijiji hicho wakati wa operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao, ofisa wa kampeni ya (Mama Misitu) kupitia shirika lisilo la Kiserikali la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), kwenye hifadhi ya Ruvu Kusini Yahaya Mtonda amesema kuwa licha ya watu hao kufukuzwa lakini bado wanaenbdelea na uharibifu.

Mtonda amesema kuwa Mama Misitu ni kampeni yenye lengo la kuzuia na kupunguza uvunaji haramu wa mazao ya misitu na kuboresha utawala bora kwenye sekta ya misitu ili jamii ipate manufaa na misitu hiyo.

Amesema kuwa kweli hali ilikuwa mbaya kabla ya mradi huo wa miaka mitano kuanza kwani watu hao wamekuwa wakiwaondoa lakini bado wanarudi ambapo wamnevamia msitu huu na kukaa kwenye vijiji vilivyo jirani na hifadhi na kufanya uharibifu mkubwa licha ya kuwachukulia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaifisha vyombo vyao vya usafiri kama vile magari, pikipiki na baiskeli na kuwapiga faini au vipiga mnada lakini bado wanendelea.

Amesema kuwa watu hao wamevamia kijiji hicho kwenye eneo linaloitwa kwa Bibi Hindu na kujifanya wanaishi hapo ambapo ni jirani kabisa na hifadhi hiyo ambapo wakishafanya shughuli za kuharibu misitu hurudi kijijini ili kuficha kile wanachokifanya.

Aidha amesema kampeni ya Mama Misitu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya changamoto hizo za wavamizi kurejea mara kwa mara, lakini wameweza kuwawezesha wanajamii kuanzisha kamati za uhifadhi misitu ambapo endapo watakamata mali za wahalifu hao asilimia 20 ya vifaa vinavyokamatwa mara baada ya kuuzwa kwa nji ya mnada hubaki kijijini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Nasoro Mzeru amesema kuwa watu hao walipewa notisi ya kuondoka miezi mili iliyopita lakini wanaonekana kukaidi agizo hilo la serikali.

Mzeru amesema kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini watu hawea walivamia na kufanya makazi huku wakijihusisha na uharibifu wa msitu huo wa Ruvu Kusini na kila wakati wanaondolewa lakini wanarudi.

Mwenyekiti huyo amesema mbali ya kuharibu misitu pia wamekuwa wakijihusisha na vitendo viovu vikiwemo vya ubakaji, uvutaji bangi, uuzaji wa pombe haramu na wanawake kufanyabiashara za ngono jambo ambalo ni hatari na eneo hili ni hatarishi kwani watu hao licha ya kuitwa waishi kijijini wamekataa na kukaa kwenye eneo hilo la kwa Bibi Hindu,” alisema Mzeru.

Aidha amesema kuwa makazi ya yalichomwa moto hivi karibuni kwa lengo la kuwaondoa na kutakiwa kuondoka ambapo baadhi yao waliondoka lakini wengine walirudi na kuendelea na uharibifu wa msitu.

Mradi huo wa Mama Misitu kwenye hifadhi ya Msitu wa Ruvu Kusini una ukubwa wa Hekta 35,000 unaofadhiliwa na nchi za Finland na Norway, ulipewa jina hilo kwa lengo la kumuenzi mwanamke kwani endapo misitu itaharibiwa mwathirika mkuu ni mwanamke, na unatekelezwa kwenye vijiji 16 kwenye wilaya za Kibaha na Kisarawe ambapo hadi mwaka 2010 zaidi ya 40 za msitu huo ziliharibiwa na endapo udhibiti hautakuwepo msitu huo utatoweka ifikapo 2025

Mwisho.  

Na John Gagarini, Kibaha

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt Abdala Kigoda amesema kuwa uchumi wa Tanzania hauwezi kutegemea kilimo pekee bali viwanda ndivyo vinaweza kuinua uchumi na kuifanya nchi kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo kwenye Mtaa wa Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani, wakati akizindua kiwanda cha kutengenezea Jipsamu cha kampuni kutoka China ijulukanayo kama Sun Shine Gypsum Limited  Group na kusema kuwa viwanda ndiyo moja ya vyanzo vya nchi kupata fedha nyingi.

Dkt Kigoda amesema kuwa hata nchi zilizoendela zilianza na viwanda vidogo na viwanda vya kati hadi vikafikia kuwa na utajiri mkubwa walionao sasa ambapo China ni moja wapo ya nchi zilizoanza kwa utaratibu huo lakini kwa sasa iko mbali kiuchumi.

Waziri amesema kuwa Viwanda vinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa huku asilimia 40 ya wananchi wakiwa wameajiriwa kwenye sekta ya viwanda hapa nchini na kufanya uchumi kutegemewa kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hiyo ambayo kwa sasa inaendelea kukua licha ya baadhi ya watu wakidai kuwa eti Tanzania haina viwanda vingi jambo ambalo si kweli.

Aidha amesema kuwa hata wajasiriamali wa tanzania wanaweza kuungana kujenga viwanda kama hivi ambavyo ni vya daraja la kati hasa ikizingatiwa malighafi za kutengenezea bidhaa hiyo zote zinapatikana hapa hapa nchini.

Ameongeza kuwa wamiliki hao wanapaswa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa Kibaha ili nao wafaidi matunda ya uwepo wa kiwanda hicho na wasaidie huduma za kijamii na kujenga mahusiano mazuri pia wazingatie viwango ili bidhaa hizo ziweze kuwa na soko ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameipongeza kampuni hiyo na kusema kuwa dhana ya kurudisha uchumi kwa wananchi sasa imeanza kuonekana kwani baadhi ya wakazi wa hapa wamepata ujuzi na ajira.

Koka amesema kuwa kampuni hiyo imezingatia suala la ajira kwani hadi sasa watu 60 wamepata ajira huku baadhi yao wakipewa kazi za umeneja na si kuwa zile za ufagizi tu kwani hayo ndiyo yanayopaswa kufanywa na viwanda vingine ili kuweka usawa wa utendaji kazi 

Amebainisha kuwa Mji uliamua eneo hilo la Kata ya Visiga kuwa eneo la viwanda hivyo wajasiriamali na watu mbalimbali wana nafasi kubwa ya kuweka viwanda vyao hapo na si kung'ang'ania kujenga Dar es Salaam pekee ambapo hadi sasa eneo hilo tayari kuna viwanda vinne vingine vikiwa ni cha kusafishia mafuta, madini na nondo,  vimeshajengwa.

Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka jana na kina thamani ya dola za Kimarekani milioni tatu na kimeajiri watu 60 na tayari kimeanza uzalishaji ambapo bidhaa zake zinauzwa ndani na nje ya nchi.

mwisho. 


No comments:

Post a Comment