Monday, August 26, 2013

MWANALUGALI WATWAA UBINGWA



Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka ya Mwanalugali imenyakua ubingwa wa Micho Cup baada ya kuifunga timu ya Bamba zote za wilayani Kibaha mkoani Pwani kwa magoli 2-1.
Mchezo huo ilipigwa kwenye uwanja wa Kwa Mbonde wilayani Kibaha ulikuwa mkali na wa kusisimua muda wote na kuwafanya mashabiki waliojazana uwanjani hapo kushindwa kukaa kwenye viti vyao.
Washindi walianza kupata bao la kuongoza dakika ya nane ya mchezo kupitia kwa Makida Makida baada ya gonga za hapa na pale na kuwainua mashabiki wake.
Huku Bamba wakiwa hawajajiweka sawa walishtukia wakipachikwa bao la pili kupitia kwa Laurence Mugia dakika ya 13, hata hivyo Bamba walifanikiwa kupata bao la kufuta machozi dakika ya 44 ya mchezo.
Naye wandaaji wa mashindano hayo Athuman Shija alisema kuwa jumla ya timu 14 zilishiriki mashindano hayo ambayo yalikuwa na lengo la kuhamasisha michezo kwenye wilaya hiyo.
Kwa upande wake meneja wa kampuni ya 3 J’s ambao ndiyo wadhamini wa mashindano hayo Samwel Mwegoha alisema kuwa wataendelea kudhamini michezo ili vijana waweze kupata ajira kupitia michezo.   
Kufuatia ushindi huo wa Mwanalugali washindi walipata zawadi za jezi seti mbili, mipira miwili na mipira miwili, Bamba walipata mipira miwili  na fedha taslimu kiasi cha shilingi 150,000.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment