Thursday, August 15, 2013

KIFAA KIPYA KUDHIBITI MADEREVA WAENDAO MWENDO KASI CHAINGIA NCHINI

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la polisi nchini limeanza mradi wa majaribio wa matumizi ya kifaa cha kisasa cha kuangalia mwenendo wa magari yanayokwenda mwendo kasi ili kupunguza ajali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wakifanya majaribio ya vifaa hivyo kwenye barabara ya morogoro, kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani Nasoro Sisiwaya   alisema kuwa vifaa hivyo vimeanza kufanya majario mkoani humo kwa majaribio.

Sisiwaya alisema kuwa vifaa hivyo ni vya kisasa kwani vitafungwa sehemu ya juu na kuyaona magari tofauti na vile vya awali ambavyo hushikwa mkononi na vilikuwa havina taarifa za kutosha hasa wakati wa kuthibitisha kosa .

“Kifaa hichi kina uwezo wa kutoa taarifa za gari ambalo limeonekana kwenda kwa mwendo kasi  kwani kinauwezo wa kuonyesha kasi ya gari, muda na namba za gari husika, tofauti na kile cha zamani ambacho kinaonyesha mwendo kasi pekee ambapo dereva ana uwezo wa kukana kwani hakuna ushahidi wa kutosha,” alisema Sisiwaya.   

Naye mwakilishi wa kikosi cha usalama barabarani nchini Notker Kilewa, alisema kuwa kifaa hichi cha kisasa na kinauwezo wa kufungwa sehemu ambayo kitaona magari na mienendo yao na kulitambua gari lenye mwendo kasi kinyume cha sheria.

Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya TMT ya Afrika Kusini, hapa nchini Twaha Ngambi ambayo inasambaza vifaa hivyo alisema kuwa kifaa hicho kitasaidia kukabiliana na madereva wanaokwenda mwendo wa kasi pamoja na makosa mengine ya barabarani.

Ngambi alisema kuwa kifaa hicho kitakuwa na uwezo wa kuona umbali wa mita 200 toka kilipofungwa hivyo itaondoa usumbufu wa kulisimamisha ghafla gari ambalo linabainika kuwa kwenye mwendo wa kasi.

Mwisho.



 Moja ya wataalamu toka Afrika Kusini kupitia kampuni ya TMT akiunganisha mitambo wakati wa wakifanya majaribio ya namna ya kutumia kifaa hicho ambacho kitakuwa na uwezo wa kuona magari ambayo yanakwenda kwa mwendo kasi kinyume na sheria za usalama barabarani, huko Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
 

No comments:

Post a Comment