Thursday, August 15, 2013

YATIMA WTENGEWE ENEO

Na John Gagarini, Bagamoyo

KATA ya Miono wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imetakiwa kutenga eneo kwa ajili ya kufanya shughuli za watoto yatima na wale waishio kwenye mazingira magumu.

Akizungumza jana kwenye kata hiyo wakati wa kuzindua mfuko wa kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu Meya wa mji mdogo wa Bagamoyo Abdul Sharifu alisema lazima viongozi wa vijiji wanapaswa kutenga maeneo kwa ajili ya kundi hilo.

Sharifu alisema kuwa kundi hilo limekuwa halitendewi haki hasa zinapotokea fursa mbalimbali kutokana na baadhi ya viongozi kutoona umuhimu wa watoto hao na kuwaona kama hawastahili kwenye jamii.

“Watoto yatima na wale waishio kwenye mazingira magumu ni sawa na watoto wengine na wanastahili kuwekewa mazingira mazuri ili waweze kuishi na kupata huduma muhimu za kijami hivyo ni vema mkawatengea eneo lao kwa ajili ya kufanyia shughuli zao,” alisema Sharifu.

Alisema kuwa katika eneo hilo watakuwa wakilitumia kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusoma, michezo, kujifunza ufundi na masuala mengine kwa ajili ya watoto.

“Mimi mwenyewe nilikuwa yatima baada ya kufiwa na wazazi wangu ndiyo sababu nimeguswa na jambo hili la kuanzisha mfuko kwa ajili ya kuwasaidia kwani najua taabu wanazozipata na sisi ndiyo wa kuwasemea na kuwasaidia,” alisema Sharifu.

Kwa upande wake moja ya watoto yatima Yusuph Ally alisema kuwa jambo alilolifanya meya ni la kuigwa na viongozi wengine pamoja na jamii inayowazunguka.

Katika uzinduzi huo Meya huyo alichangia kiasi cha shilingi 500,000 kwa ajili ya mfuko huo na kuahidi kutoa shilingi milioni 2 mara ufunguaji wa akaunti utakapokamilika, jumla ya watoto zaidi 200 walihudhuria.    

Mwisho.

 
Meya wa mji wa Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu katikati akiangalia watoto walipokuwa wakicheza wakati wa uzinduzi wa mfuko wa watoto yatima kata ya Miono wilayani humo.

No comments:

Post a Comment