Thursday, August 15, 2013

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WASHUKIWA

Na John Gagarini, Bagamoyo

WAKURUGENZI wa Halmashauri za wilaya na Miji mkoani Pwani wametakiwa kuwashirikisha maofisa tarafa kwenye vikao mbalimbali vya maendeleo kwani wao ni wasimamizi wa mambo yote kwenye tarafa zao.

Hayo yalisemwa mjini Bagamoyo na katibu tawala wa mkoa wa Pwani Beatha Swai, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa tarafa wa mkoa huo.

Swai alisema kuwa anawashangaa wakurugenzi wa halmashauri kutowatenga maofisa hao ambao ni kiungo muhimu baina ya serikali na wananchi lakini wamekuwa wakiwekwa pembeni na kuonekana kama hawastahili kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Inashangaza hata kwenye vikao vya uongozi juu ya maendeleo hawashirikishwi kama ilivyo kwa wataalamu wengine kwenye halmashauri hawa nao wanapaswa kupewa kipaumbele katika michakato mbalimbali ya maendeleo,” alisema Swai.

Alisema kuwa tayari serikali ilishawapa waraka wakurugenzi hao kuwashirikisha kwenye masuala yote yanayohusu utendaji kazi ili wafanye kazi kwa pamoja lakini bado wanakaidi maagizo hayo.

“Tumeona kuwa kwenye vikao vya uongozi juu ya maendeleo hawashirikishwi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu hivyo tutawachukulia hatua kali za kisheria wakurugenzi wote ambao wanakiuka taratibu za kazi,” alisema Swai.

Aidha alisema kuwa wakurugenzi hao wamekuwa na dhana kuwa maofisa tarafa hao wanakwenda kwa ajili ya kupata posho jambo ambalo halina ukweli kwani kushiriki kwenye vikao kama hivyo ni haki yao.
Awali akifungua mafunzo hayo mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa baadhi ya maofisa tarafa wengine hawajui wajibu wao.

Mahiza alisema kuwa maofisa tarafa hao wanapaswa kujua wajibu wao kwa kutimiza malengo ambayo yanawekwa na halmashauri na wanapaswa kuwa na taarifa zote za shughuli za maendeleo na changamoto ndani ya tarafa zao.

Mwisho.

 
mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza akizungumza na maofisa tarafa wa mkoa huo alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo kwenye ukumbi wa chuo cha uongozi cha ADEM Bgamaoyo mkoani Pwani

baadhi ya maofisa tarafa wa mkoa wa Pwani wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza hayupo pichani wakati akifungua mafunzo kwa maofisa hao kwenye ukumbi wa chuo cha uongozi cha ADEM Bagamoyo mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment