Tuesday, August 20, 2013

MAJAMBAZI YAVAMIA KWA DAVIS MOSHA YAPORA




Na John Gagarini, Kibaha

WATU 10 wanaozaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi kama marungu na mapanga wamevamia kituo cha mafuta cha Delina mali ya Davis Mosha na kufanikiwa kupora vitu  mbalimbali ambavyo thamani yake bado haijaweza kufahamika mara moja.

Akithibitisha kutokea tukio hilo kamanda wa Polisi mkoa Pwani  Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea usiku saa saba Agosti 19 eneo la Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani humo.

Matei alisema kuwa watu hao walifika kituoni hapo wakiwa na gari mbili moja  aina ya Prado na nyingine aina ya Saloon rangi nyeupe walizoegesha karibu na pampu za kuwekea mafuta.

“Baada ya hapo walimkamata mfanyakazi wa zamu  aitwaye Samsoni Rufunga na mlinzi wa kituo hicho Mohamed Shaban na kuwafunga  kamba  za miguu na mikono na kuwafungia ndani ya chumba kimoja kilichopo katika kituo hicho na kupora fedha hizo ambazo bado hazijafahamika,” alisema Matei.

Aidha alisema kuwa majambazi hao yalimkamata Frank Nyamahaga ambaye ni dereva mkazi wa Tabata nakumpora laki moja ,simu mbili za laki mbili na funguo za gari lake aina ya scania lililokuwa limeegeshwa kituoni hapo.

“Watu hao walimkamata Isack Silinu  ambaye alikuwa utingo wa scania hiyo ambaye naye aliporwa simu aina ya Itel yeny thamani ya sh.38,000, wakati Shabani Ramadhani aliporwa simu aina ya nokia yenye thamani ya sh. 45,000, Issa Mohamed aliyeporwa
simu aina ya nokia yenye thamani ya sh.75,000 na pesa taslimu sh.68,000  na wote walikuwa  wakisafiri katika lori aina ya scania
likitokea Iringa kuelekea Dar,” alisema Matei.

Aliongeza kuwa kama haitoshi watu hao walimpora Juma Seleman wa Mwanalugali, pikipiki aina ya Sanlg na fedha kiasi cha shilingi 46,000 alipokwenda kituoni hapo kwa ajili ya kununua mafuta.

Alibainisha kuwa katika tukio hilo hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo na jeshi hilo linaendelea na jitihada za kuwasaka majambazi hao ili waweze kutiwa nguvuni.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment