Sunday, September 8, 2013

VIZIWI NA MAJI

Na John Gagarini, Kibaha
VIZIWI mkoani Pwani wamependekeza kwenye katiba ijayo iwe na kipengele cha matumizi ya lugha ya alama kwenye maeneo ya umma ili kurahisisha utoaji huduma kwa watu wote.
Hayo yalisemwa na katibu wa klabu ya Michezo ya Viziwi mkoani Pwani (PDSC), Daud Kulangwa wakati akitoa ripoti ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya baraza la katiba lililofanyika Mlandizi wilayani Kibaha.
Kulangwa alisema kuwa kwa katiba iliyopo inasema tu kuweka mazingira ya matumizi ya lugha ya alama ambayo utekelezaji wake kwani sehemu za umma na sekta binafsi  matumizi ya lugha hiyo hayapo kwa sasa.
“Tunataka kwanza kuwe na mafunzo ya lugha ya alama na nukta nundu kama ilivyo masomo mengine mashuleni na kwenye vyuo kwa watumishi wa umma na kila raia wa Tanzania awe anaijua lugha hiyo ambapo wafanyakazi wa umma wataweza kuwasiliana na watu wenye ulemavu kama wafanyavyo ndani ya ndege,” alisema Kulangwa.
Alisema kuwa kwa sasa watu wenye ulemavu wakiwemo viziwi wasioona wanapata tabu sana wanapokwenda kwenye sehemu za kupata huduma kama vile mahakamani, polisi, hospitali, maofisini, mahali pa kuabudia na sehemu nyingine hivyo kushindw akupata huduma stahili.
“Kama unavyojua ukienda sehemu za huduma unashindwa kuhudumiwa kwani wahusika hawajui kumwelekeza mteja kwa usahihi kutokana na mawasailiano kuwa magumu hivyo kushindwa kupata kile kinachostahili,” alisema Kulangwa.
Aidha alisema kuwa kwenye kipengele cha lugha ya Taifa ni Kiswahili pia kuwe na nyongeza ya lugha ya alama ili iwe kisheria na endapo mtu atashindwa kutekeleza iwe ni kosa kisheria.
“Uwepo wa lugha ya alama na nukta nundu utasaidia mawasiliano kwa watu wote hasa kwenye shughuli za serikali na watu watu wenye ulemavu watapata taarifa kwani kwa sasa upatajia wa taarifa ni mdogo sana kutokana na matumizi ya lugha ya alama kutopewa kipaumbele,” alisema Kulangwa.
Aliongeza kuwa juu ya haki za watu wenye ulemavu zitajwe na aina, kuwezeshwa na serikali vifaa maalumu vya kujipatia elimu, vyombo vya usafiri, kupata hifadhi ya jamii kwa watu wenye ulemavu na kuw ana chombo cha kuwaunganisha na kuwatetea kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa. Mabaraza hayo yaliwashirikisha wajumbe zaidi ya 100 na yalifadhiliwa na The Foundation for Civil Society (FCS).
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI 5,720 wa mtaa wa Mwanalugali wilayani Kibaha mkoani Pwani watanufaika na mradi wa maji safi na salama ya bomba wenye thamani ya shilingi milioni 210,768,135 baada ya mradi wa maji kwenye mtaa huo kukamilika na kuanza kutoa maji.
Mradi huo ambao ulizinduliwa na kiongozi wa mbio za mwenge hivi karibuni Juma Simai ulianza rasmi mwaka 2009 kwa kufanywa utafiti wa upatikanaji wa huduma ya maji ya ardhini na kukamilika Januari mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati ya maji wa mtaa huo Godfrey Mwandenga alisema kuwa mradi huo uliibuliwa na wakazi wa mtaa huo kupitia mpango shirikishi na kuwa kipaumbele cha kwanza cha jamii.
“Tumepata kisima kirefu cha mita 110 chenye kutoa maji ujazo wa lita 15,00 kwa saa na mradi huu utawawezesha wananchi wa mtaa wetu wa Mwanalugali sawa na asilimia 64 watapata maji safi na salama karibu na maeneo wanayoishi kama ilivyoainishwa kwenye sera ya maji ya Taifa ya mwaka 2002,” alisema Mwandenga.
Alisema kuwa kati ya fedha zilizofanikisha mradi huo kiasi cha shilingi milioni 207,168,135 ni fedha kutoka serikali kuu na shilingi milioni 3,600,000 ni michango ya jamii.
“Mradi huu umepunguza adha kwa akinamama kufuata maji mbali na makazi yao hivyo kutumia muda huo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na mradi huu unasimamiwa na uongozi wa jumuiya ya watumiaji maji wa mtaa wa Mwanalugali.
Aidha alisema kuwa wanajumuiya hao huwajibika kukusanya mauzo ya maji, kulipia matumizi ya umeme, kufanya usafi wa mazingira, kukarabati pamoja na kupanua huduma kwa maeneo yasiyofikiwa na huduma hii.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment