Na John Gagarini, Bagamoyo
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Mary
Nagu ameitaka kampuni ya Eco Energy ya wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kuendelea
na mchakato wa kufungua kiwanda cha kuzalishia sukari ili kukabiliana na
upungufu wa bidhaa hiyo hapa nchini.
Aliyasema hayo juzi alipotembelea kampuni hiyo ili kuona
maendeleo ya mradi wa kilimo cha miwa kwenye kijiji cha Razaba wilayani humo na
kusema kuwa mara kiwanda hicho kitakapoanzishwa kitasaidia kukabiliana na
upungufu huo.
Nagu alisema kuwa kiasi kikubwa cha sukari inayotumika
inatoka nje ya nchi hali ambayo inayaosababisha bei ya bidhaa hiyo kuwa juu
ambapo uzalishaji ungeanza ungekuwa mkombozi kwa Watanzania.
“Tunajua mnakabiliwa na changamoto nyingi lakini ni vema
mkaanza kutekeleza mradi huu ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa
sukari ambapo uzalishaji huo utaambatana na mazo mengine ikiwemo umeme, mafuta
ya mitambo ya Ethanol na mbolea,” alisema Nagu.
Aidha alisema kuwa serikali itahakikisha inaweka mazingira
mazuri kwa wawekezaji ili waweze kutekeleza miradi yao ambayo pia ina faida
kubwa kwa wananchi kama ilivyo kwa mradi huo ambao utainufaisha nchi ambayo inamiliki
asilimia 25 kutokana na ardhi.
“Kwa sasa kuna watu wawili wamefungua kesi kupinga wawekezaji
hao kutokana na kuchukua ardhi kwa ajili ya mradi huu licha ya taratibu za
malipo kufanyika hivyo isiwe sababu ya wao kuchelewa kuanza kutekeleza mradi,”
aliongeza nagu.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa kampuni hiyo Jonathan
Nkandala alisema kuwa mbali ya kuzalisha sukari tani 150,000 kwa mwaka pia mradi
huo pia utazalisha megawati 25 za umeme, mafuta na mbolea ambapo eneo la mradi
lina ukubwa wa hekta 22,000 huku eneo la miwa lkiwa na ukubw awa hekta 8,000.
Nkandala alisema kuwa umeme utakaozalishwa megawati 14 hadi 15 zitatumika kwenye gridi ya taifa huku
nyingine zikibaki kwenye mradi huo kwa ajili ya kuendeshea mashine na mitambo
mbalimbali ambapo hadi sasa umeshatumia dola milioni 50 na hadi kukamilika
kwake utagharimu kiasi cha shilingi dola milioni 500 na ulianza mwaka 2007 na
unatarajiwa kukamilika 2016.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment