Thursday, September 19, 2013

MATUKIO MBALIMBALI YA PWANI



Na Mwandishi Wetu, Kibaha
IMEBAINIKA kuwa uwepo wa mabanda ya kuonyeshea video mitaani ambayo hayapo kisheria kumechangia vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo ambao ni wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha umebaini kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo nyakati za usiku wanapokuwa wamekwenda kuangalia video ambapo waonyeshaji wa video hizo huonyesha picha chafu za ngono.
Mabanda hayo ambayo mengi yamejengwa kwa mbao au mifuko ya sandarusi na kuezekwa na makuti au nyasi na yasiyo na mvuto yamekuwa yakionyesha picha hizo maarufu kama pilau, kachumbari na ubwabwa na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.
Baadhi ya wakazi ambao wamelaani uwepo wa mabanda hayo ambayo huanza kuonyesha video majira ya asubuhi hadi usiku na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushinda humo huku wakiwa wameaga wanakwenda shule na kuishia humo na endapo wazazi hawatafuatilia kuna hatari ya mwanafunzi huyo kutohudhuria darasani kabisa.
Walimwelezea mwandishi wa habari hizi kuwa njia wanazotumia wabakaji hao ni kuwalipia kiingilio cha kuangalia picha ambacho ni shilingi mia tano kwa filamu ziltakazoonyeshwa kwa siku hiyo ambazo huonyeshwa kwa awamu na huchukua kila awamu zaidi masaa matatu kisha kubadili picha zingine.
Picha zinapokuwa zinaendelea mara hubadili na kuweka picha chafu za ngono hivyo kuhamasisha vitendo hivyo na kwa kuwa vijana hao wanaobaka watoto wanakuwa wamewalipia kiingilio huwachukua na kuwapakata watoto hao na wanapokuwa wamepandwa na msisimko huanza kuwaingilia watoto hao hadi wanapomaliza haja zao.
“Mara wamalizapo haja zao huwapa fedha kwa ajili ya kuwataka wasiseme kwa wazazi wao ambapo watoto hao baadaye huzoea na kujikuta kila wakati wakienda kwenye mabanda hayo na kufanyiwa vitendo hivyo na kuzoea hali ambayo ina waathiri kisaikolojia na kufanya maendeleo yao shuleni kushuka,” walisema wakazi hao.
Akizungumza na mwandishi mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lulanzi wilayani Kibaha mkoani Pwani Anna Bilali alisema kuwa wanafunzi wengi wameathiriwa na hali hiyo ambapo mbali ya kwenda kwenye mabanda hayo mara wasipokwenda shule huandika kazi walizofanya wenzao kisha kujisahishia ili kuwadanganya wazazi wao.
“Wanafunzi wa namna hii wamekuwa wakijisahishia madaftari yao lakini sisi tunagundua kwani usahishaji wao ni tofauti na wa walimu na tunapowaambia baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatetea watoto wao hali inayosababisha ugumu wa kuwadhibiti kwani baadhi ya wanafunzi hukaa kwenye mabanda hayo hadi saa tatu usiku bila hata kuulizwa walikokuwa,” alisema Bilali.
Alisema pia baadhi yao humiliki simu ambazo wanakwenda nazo shuleni na kuangalia picha hizo na kujikuta muda mwingi wakiutumia kwa kuangalia picha hizo kupitia simu ambazo huwa wanazificha na inakuwa vigumu kuwagundua hadi wenzao watoe taarifa.
Aidha alisema kuwa kuna watu wamekuwa wakiwaonyesha picha hizo kupitia simu kisha huwatoza kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo hali amabayo inaendelea kuongeza kusambaa kwa vitendo viovu.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema kuwa udhibiti wa mitandao kama hiyo ya uonyeshaji wa picha za ngono ni viongozi wa mtaa na vijiji kwa kuwachukulia hatua kwani hayako kisheria hivyo hayana sababu ya kuwepo ili kuondoa tatizo hilo.
Hivi karibuni wanafunzi wanne wa shule ya msingi Lulanzi walikamatwa na polisi wilayani Kibaha kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenzao wa darasa la pili mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia maumivu makali na kulazwa hospitali ya Tumbi ambapo aliruhusiwa kutoka wiki iliyopita baada ya kupata matibabu.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amewashukia maofisa ugani na kusema kuwa hatasita kuwaondoa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao na kudai maslahi na vitendea kazi huku uwajibikaji wao ukiwa chini hali inayowafanya washindwe kuwaletea mabadiliko wakulima.
Mahiza aliaysema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na madiwani, wenyeviti, watendaji na wataalamu wa mitaa na kata kwenye mji wa Kibaha, wakati mkutano wa kujadili changamoto na mafanikio kupitia mpango wa matokeo makubwa kwa sasa.
 Alisema kuwa maofisa ugani wengi mkoani Pwani wamakuwa hawawajibiki na kukaa tu huku wakifikiri wamekwenda kutalii ndani ya mkoa huo huku wakulima wakiwa hawana msaada wowote licha ya kulima bila ya kupatiwa stadi za kilimo bora.
“Mimi mwenyewe nimelima mashamba ya mazao mbalimbali lakini hakuna ofisa ugani hata mmoja ambaye aliweza kunitembelea kunipa ushauri wa kitaalamu sembuse mkulima wa kawaida ni jambo la kushangaza sana hakuna anayejishughulisha hali hii haikubaliki hata kidogo tutawaondoa wale watakaoshindwa kutimiza wajibu wao,” alisema Mahiza.
“Kama kuna ofisa ugani ambaye alimtembelea mkulima na kumpa ushauri wa kitaalamu asimame hakuna hata mmoja aliyefanya hivyo je mnafanya nini kama hamuwezi kazi ni vema mkaondoka mkafanye kazi sehemu nyingine lakini hapa kwangu sitakubali watu wasiowajibika,” alisema Mahiza.
Aidha alisema anashangazwa na maofisa hao kushindwa kuwa na eneo kwa ajili ya hata kulima bustani ya mchicha ili kuonyesha mfano ambapo kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa wale anaowaongoza si kukaa tu.
“Sasa hivi mnaomba usafiri wa kwenda wapi wakati uwajibikaji ni mdogo mtapewa pikipiki mtadai mafuta baadaye mtadai gari kisha dereva lakini utendaji kazi hauonekani itakuwa haisaidii mnapaswa kuwajibika ndipo mdai haki kwani huwezi kudai haki wakati hauwajibiki,” alisema Mahiza.
Aliongeza kuwa maofisa hao hakuna hata mmoja mwenye daftari la kujua idadi ya wakulima au mpango kazi wa mwaka mzima kujua atafanya nini sasa ataweza vipi kutekeleza majukumu yake bila ya kujua masuala mazima ya wakulima.
“Kutokuwa makini kunasababisha kupikwa kwa takwimu sisi tunachotaka hali halisi na si kutengeneza pia mkumbuke mwaka juzi tuliwaomba mipango kazi ya kata zenu mlituletea lakini cha kushangaza hamjatekeleza hata jambo moja,” alisema Mahiza.
Aliwataka watendaji wa sekta mbalimbali kuwajibika kwa nafasi zao na si kukaa tu pia watembee wasikae ofisini badala yake wawatembelee wananchi kujua mahitaji yao na kuachana na tabia ya kutengeneza takwimu mezani bali wajionee hali halisi.
Mwisho.     
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
KIJANA aitwaye Ibrahimu Jumapili (30)mkazi wa Kongowe wilayani Kibaha mkoani Pwani amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kanga kwenye mti wa mkorosho.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa wa Bamba wilayani Kibaha Amry Mavala alisema kuwa marehemu hakuweza kuacha ujumbe wowote wa sababu ya kuchukua maamuzi hayo  ya kujiua.
Mavala alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 17 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana kwenye mtaa wa Bamba kata ya Kongowe wilayani humo.
“Marehemu alikuwa akijishughulisha na kazi ya ufayatuaji matofali na kabla ya kifo chake alikuwa akilalamika kuwa kuna watu walikuwa wakitaka kumtoa kafara,” alisema Mavala.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo marehemu alisema kuwa anamwachia Mungu na itambidi arudi nyumbani kwao mkoani Singida ili ajinusuru na hali hiyo.
Kwa upande wake kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani Juma Ali alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukininginia kwenye mkorosho kwenye shamba la Mzee Rafael.
Ali alisema kuwa chanzo cha kifo chake hakijaweza kufahamika na mwili wa marehemu uko kwenye hospitali ya Tumbi kwa ajili ya uchunguzi wa daktari na taratibu za mazishi.
Wakati huo huo mwili wa mtu asiyefahamika umeokwotwa huko kwenye mtaa wa Kwa Mathiasi wilayani Kibaha ukiwa umeharibika vibaya ambapo ulikutwa na jeraha shingoni na mtu mmoja anashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, na mwili huo ulizikwa hapo hapo baada ya kushindwa kuhamishwa.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WATU sita  wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani wakiwemo wawili wanaodai kuwa ni askari polisi kwa tuhuma za kukutwa na nguo zinazosadikiwa kuwa ni za magendo kutokea nchini Kenya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Juma Ali alisema kuwa watuhumiwa walikamatwa na gari lililokuwa limebeba nguo za kike na kiume.
Ali alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9 alfajiri eneo la Vigwaza wilayani Bagamoyo kwenye kizuizi wakati askari wakiwa doria kwenye barabara ya Dar es Salaam Chalinze.
Alisema kuwa watuhumiwa wawili ambao ndiyo walikuwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 303 BAY lenye mzigo huo lilikuwa likiendeshwa na Omary Salehe (66) mkazi wa Arusha na utingo Fuwad Salimu (46) mkazi wa Moshi.
“Wakati gari hiyo ikiwa inaendelea na safari yake ilikuwa ikifukuzwa kwa kasi ilipofika Mbwewe na gari nyingine aina ya NOAH yenye namba za usajili T 641 CCH ikiwa na watu wanne wakiwemo watu hao wawili ambao bado hawajathibitishwa kama ni polisi kutokea mkoani Tanga au la huku mwingine akiwa askari mstaafu na mtu mwingine,” alisema Ali.
Aidha alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi juu ya kujua thamani ya mzigo huo na kuwatambua watu hao kama ni askari kweli au la ili hatua sahihi ziweze kuchukuliwa ambapo magari hayo bado yanashikiliwa na watuhumiwa wanahojiwa kupata ukweli.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MTU mmoja mkazi wa Kongowe Joseph John (17) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi (jina tunalo).wa shule ya Msingi Kongowe mwenye umri wa miaka 11.
Akizungumza na waandishi wa habari shangazi wa mtoto huyo Rukia Bora alisema kuwa alimgundua mtoto huyo kuingiliwa baada ya kulalamika kuwa anasikia maumivu shemu za haja kubwa.
Bora alisema kuwa alimgundua mtoto huyo wa mdogo wake wa kiume kuingiliwa Septemba 12 mwaka huu.
Alisema kuwa baada ya kumhojia alimwelekeza alipokuwa akifanyiwa mchezo huo kwa muda sasa ambapo ni karibu miezi mitatu iliyopita tangu kuanza kufanyiwa hivyo na mtuhumiwa na watu wengine ambao walikimbia na bado wanatafutwa.
“Huyu mtoto anaishi na bibi yake lakini kwa kuwa mimi na bibi yake tuko jirani hapa Kongowe Kati wakati mwingine anakuja kwangu hivyo tunamlea kwa pamoja ambapo baba yake yuko Jijini Dar es Salaam na mke we waliasha achana lakini kutokana na tabia za mtoto za utundu udhibiti wake ulikuwa mgumu,” alisema Bora.
Aidha alisema kuwa baada ya kumhoji alikataa kusema ikabidi wampeleke polisi na baada ya kubanwa ilibidi aseme ukweli na kueleza kila kitu.
“Alisema kuwa chumba (Ghetto) alichokuwa akifanyiwa mchezo huo wanaishi vijana watupu ambao wanajihusisha na uimbaji kwenye shghuli mbalimbali za sherehe, ambapo walikuwa wakimwingilia kwa nyakati tofauti muda wa usiku na kumwambia asiseme kwa mtu yoyote,” alisema Bora.
Alibainisha kuwa chanzo cha yeye kujua hilo ni baadhi ya majirani kuona kuwa mtoto huyo kuwa karibu na mtuhumiwa hali ilyowatia shaka majirani.
“Baada ya kugundua nilimfuata mtuhumiwa na kumkamata na kumpeleka polisi hata hivyo watuhumiwa wengien wawili walikimbia ambapo jana watoto wawili ambao nao walikuwa wakimfanyia hivyo walipelekwa polisi kuhojiwa na kinachosubiriwa ni mtoto huyo kwenda kuwatambua,” alisema Bora.
Alisema kwa sasa mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Tumbi.    
 Kwa upande wake kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani Juma Ali alisema kuwa mbali ya mtuhumiwa huyo watuhumiwa wengine walikimbia na wanaendelewa kutafutwa.
 Ali alisema kwa sasa kinachosubiriwa ni gwaride la utambulisho wa watuhumiwa wawili wadogo ambao ni wanafunzi ili nao waunganishwe na mtuhumiwa wa kwanza.
Mwisho.

  

No comments:

Post a Comment