Thursday, July 25, 2013

WALIOACHISHWA TANROADS WALIA

Na John Gagarini, Kibaha

WALIOKUWA wafanyakazi 59 wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani ambao wamepunguzwa kazi wameilalamikia wakala hiyo kwa madai kuwa imevunja mikataba yao na malipo waliyowapa hayalingani na muda waliofanya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha mwenyekiti wa kamati ya kufuatiia haki za wafanayakazi hao waliopunguzwa Andrew Lugano alisema kuwa malipo waliolipwa ni kidogo.

Lugano alisema kuwa inashangaza kuona mtu kafanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 lakini analipwa shilingi 400,000 ni ndogo na haziwezi kuwasaidia hasa kipindi hichi kigumu cha maisha.

“Jambo la kwanza tumekuwa tukiingia mkataba na mwajiri wetu kila mwanzo wa mwaka lakini cha kushangaza mwaka huu tumekaa hadi Juni 15 ndipo tuliposaini mkataba mpya lakini tukaambiwa mwisho wa ajira yetu ni Juni 30 jambo ambalo tunaona ni kinyume cha taratibu ni vema tungemaliza mwaka huu ndipo wangechukua hatua hiyo,” alisema Lugano.

Alisema kuwa hadi sasa hawajajua sababu ya wao kuachishwa kazi japo kuna tetesi kuwa ni wale wenye elimu ya darasa la saba lakini pia kuna wenye elimu kubwa zaidi ya hiyo lakini wameachishwa hivyo kushindwa kujua kiini hasa nini.

“Sisi tunachotaka ni kulipwa fedha ambazo zionalingana na utumishi wetu na kama ni suala la elimu mbona kuna wenzetu wawili kati ya watu 60 walioachishwa walirudishwa na wana elimu ya darasa la saba?,” aliuliza Lugano.

Aidha akizungumzia suala la elimu alisema kuwa Raisi Jakaya Kikwete alisema kuwa wafanyakazi ambao wanafanyakazi ambao wana elimu ya darasa la saba wasifukuzwe bali waendelezwe kwanini wao wanaondolewa pasipo taratibu kufuatwa.

“Fedha ambazo tumejumlisha kwa haraka haraka kwa watu 28 waliojiorodhesha kudai ni milioni 77 kama tungelipwa kulingana na hali ya sasa hivi, lakini tuliyopewa ni ndogo sana hivyo tunaomba watufikirie kwani hata gharama ya kusafiria kwenda makwetu haitoshi au kuendeshea maisha kwani jambo hili limekuwa la kushtukiza sana,” alisema Lugano.

Aliongeza kuwa walikwenda chama cha wafanyakazi cha TUICO na kupewa barua ya kumpelekea mwajiri wao ili wakutane kwenye baraza la usuluhishi (CMA) mkoa kuzungumzia suala hilo na watumishi waliokumbwa na hali hiyo ni madereva, walinzi, maopareta na wahasibu.

Kwa upande wake meneja wa TANROADS Tumaini Sarakikya alisema kuwa wamefuata taratibu zote za kisheria na juu ya mikataba mwajiri ana maamuzi ya kuongeza au kupunguza mkataba.

“Tayari wameshakwenda kulalamika CMA na sisi tumeshajiandaa tunasubiri muda ufike tukayazungumze masuala hayo, lakini tumewapunguza kwa kuzingatia sheria,” alisema Sarakikya.

Sarakikya alisema kuwa hawajamwonea mfanyakazi yoyote bali ni mabadiliko tu ambayo yametokea na wao wanafahamu hivyo hakuna uonevu.

MWISHO.



No comments:

Post a Comment