Thursday, May 23, 2013

MBUNGE KUSAIDIA VIKUNDI VYA SANAA NA MICHEZO


Na John Gagarini, Bagamoyo
MBUNGE wa Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani Said Bwanamdogo amevitaka vikundi vya sanaa na michezo kwenye kata ya Miono kumpelekea mahitaji yao ili aweze kuwasaidia.
Alitoa ahadi hiyo wakati akikabidhi fedha kwa kikundi cha akinamama cha upendo cha Upendo Saccos cha Miono na kusema kuwa vikundi hivyo vinahitaji misaada ili viweze kukua.
Bwanamdogo alisema kuwa vipaji vingi vijijini huwa vinapotea kutokana na kushindwa kuendelezwa kutokana na kukosa vifaa na mahitaji mbalimbali.
“Lengo ni kutaka kusaidia vikundi mbalimbali ili viweze kujiendeleza hasa tukizingatia kuwa sanaa na michezo ni sehemu ya ajira na si kujairiwa maofisini pekee,” alisema Bwanamdogo.
Aidha alisema kuwa vikundi vya sanaa na michezo viko vingi lakini havina sehemu ya kusaidiwa ili viweze kuwa na ustawi kama vilivyokuwa vya mijini.
“Nimeona vikundi vingi vya sanaa na michezo vinauwezo mkubwa lakini havijaendelezwa hivyo nitahkikisha kuwa navisaidia ili viweze kusonga mbele,” alisema Bwanamdogo.
Aliongeza kuwa kwa sasa anajipanga vema ili aweze kuandaa mashindano mbalimbali ya michezo kwa vijana waweze kuonyesha vipaji vyao.
Mwisho. 

No comments:

Post a Comment