Na John Gagarini, Kibaha
MATAWI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini yametakiwa
kuanzisha vitega uchumi ili kujiongezea kipato badala ya kuyafanya matawi hayo
vijiwe vya kukaa bila ya tija.
Hayo yalisemwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC)
kutoka wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Rugemalira Rutatina, wakati akizindua tawi
la Mtazamo lililopo kata ya Tumbi wilayani humo.
Rutatina alisema kuwa matawi hayo ndiyo msingi wa chama hivyo
lazima matawi hayo yajianzishie vyanzo vya kupata mapato badala ya kukaa tu na
kubweteka.
“Hili ni kati ya matawi ambayo yameonyesha mwanga kwani kuwa
na fedha kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ni kitu muhimu na si vema
tawi kuwa sehemu ya kukaa tu bila ya kubuni vyanzo vya mapato na si kusubiri
kusaidiw akwa kila kitu,” alisema Rugemalila.
Alisema kuwa kwa kuwa matawi ndipo sehemu ya kukiimarisha
chama lazima matawi hayo yawe na nguvu za kiuchumi ili waweze kukiimarisha
chama.
“Mkiwa na uchumi imara mnaweza kuisaidia jamii mfano kutoa
vitanda kwa wagonjwa kwenye hospitali au kuihudumia kwa njia yoyote ile ili iwe
mfano mzuri,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa wanachama wa CCM wanatakiwa kuwaeleza
viongozi changamoto zilizopo na si kuanzisha makundi ambayo hayana manufaa.
Aliwataka Watanzania kuwa na imani na chama na kukataa
propaganda za wapinzani kuwa hakuna kilichofanyika tangu nchi kupata uhuru
jambo ambalo ni upotoshaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment