Sunday, May 26, 2013

WEKENI WAZI MATUMIZI FEDHA MFUKO WA JIMBO



Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
WABUNGE nchini wametakiwa kuwa wazi juu ya matumizi ya fedha za maendeleo za mfuko wa Jimbo ili wananchi waweze kujua fedha hizo namna zinavyotumika.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alipokuwa akizungumza kwenye halmashauri za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za kata za Kiwangwa na Fukayosi.
Bwanamdogo alisema kuwa baadhi ya wabunge wamekuwa wakizitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi kinyume na taratibu za fedha za mfuko wa Jimbo.
“Baadhi ya wabunge wamekuwa wakizitumia fdedha hizo kwa siri kwa manufaa yao badala ya kuzitumia kwa shughuli za maendeleo ya wananchi jambo ambalo si zuri kwani ni kuwakatisha tama watu kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema Bwanamdogo.
Alifafanua kwa kusema kuwa fedha hizo lazima mbunge aonyeshe namna zilivyotumika kwani fedha hizo hazina siri yoyote kwani ni za maendeleo.
“Ni vema wabunge wakaweka wazi mapato na matumizi ya fedha hizo na kuwaeleza wananchi jinsi zilivyotumika kwani ni haki yao kujua lakini wengine wanazipiga (wanazila) huku wengine wakielekeza wazabuni Fulani ndiyo wapitishwe kufanya miradi mbalimbali,” alisema Bwanamdogo.
Aidha alisema kama yanavyosomwa mapato na matumizi ya sekta zingine hata fedha za mfuko wa Jimbo lazima zisomwe kwa wananchi ili wajue matumizi yalivyokwenda.
Katika kuweka sawa suala la uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo mbunge huyo ameelezea mapato na matumizi ya fedha hizo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment