Sunday, March 10, 2013

STORY ZA PWANI



Na John Gagarini
 MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza amesema kuwa serikali haitakaa kimya kuona baadhi ya kinamama wakifanya vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na kutupa watoto wanaowazaa.
Mahiza aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kusherehekea siku ya Wanawake Duniani kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kusema kuwa baadhi wanawake wamekuwa wakiwafanyia ukatili hata watoto wao wa kuwazaa.
Alisema kuwa moja ya ukatili ambao umekithiri mkoani Pwani ni kuwatupa watoto jambo ambalo limekuwa likishika kasi siku hadi siku kwenye mkoa huo.
“Serikali haitaweza kuvumilia kuona baadhi ya akinamama wakitenda vitendo vya ukatili kwa watoto wao kwani nao wana haki ya kulelewa na wana haki ya kupata matunzo pamoja na kuishi hivyo ni vema kila mtu akatimiza wajibu wake kwani hiyo ni haki ya msingi ya mtoto,” alisema Mahiza.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa haipendezi kuona wanawake wanakuwa mstari wa mbele kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wao.
“Kama unaona bado hujajianda kulea kwanini uzae kama wewe ungefanyiwa hivyo sasa hivi ungekuwa wapi na mtu wa aina gani ni lazima mjilinde na kuachana na vietendo hivyo kwani ni ukatili ambao hutaweza kuvumiliwa na serikali na hatua kali zitachukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema vitendo hivyo ni vibaya kwani mbali ya kuwaua watoto pia ni kuwafanya wawe watoto wa mitaani na kuathirika kisaikolojia  na kuwajengea mazingira mabaya ya kuishi.
Kwa upande wake mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka alisema kuwa aliamua kuwakusanya wanawake kwa pamoja ili kubadilishana mawazo na kutafakari siku hiyo katika kutimiza majukumu yao kama mama.
Koka alisema kuwa siku hiyo ina maana kubwa kwa akinamama katika kuihudumia jamii na Taifa ambalo linawategemea katika kujenga uchumi wa nchi.
Mwisho.
WAANDISHI wa Habari wa Kanda ya Mashariki wametakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa Jamii inayowazunguka ili kuondokana na dhana juu ya chanjo mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa watoto kuwakinga na magonjwa yanayosababisha vifo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kaimu katibu Tawala mkoa wa Pwani Injinia Michael Mrema wakati akifungua mafunzo ya siku moja juu ya chanjo mpya ya magonjwa ya Nimonia na Uti wa Mgongo ya Rotavirus kwa waandishi wa Kanda ya Mashariki.
Injinia mrema alisema kuwa jamii imekuwa na dhana mbaya kuwa baadhi ya chanjo zina athari kwa watoto hivyo kushindwa kuwapeleka kupata chanjo.
“Waandishi ni watu wanaoaminiwa na jamii hivyo kwa kutumia kalamu zenu mnaweza kutoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo hizo kwa  watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao wanakufa kutokana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali,” alisema Injinia Mrema.
Alisema kuwa magonjwa kama hayo husababisha vifo kwa asilimia 80 hivyo lazima itumike nguvu ya ziada ya kutoa elimu ili jamii ione umuhimu wa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwa lengo la kupunguza vifo hivyo visivyo vya lazima.
“Chanjo hii mpya inatoa kinga kwa asilimia 87 hadi 88 ambapo nchi imejitahidi sana kwani imeweza kupunguza vifo toka 99 hadi 51 kwa watoto 1,000 kwa mwaka 2010,” alisema Injinia Mrema.
Aidha alisema kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote na endapo jamii itapata taarifa sahihi hawataweza kupotoshwa na watawapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ambayo ni bure na haina gharama zozote.
Kwa upande wake ofisa habari idara ya habari maelezo Veronica Kazimoto alisema kuwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yatasaidia kufikisha ujumbe sahihi na haraka kwa walengwa hivyo wanaamini kuwa waandishi ni njia sahihi ya kutoa elimu. Mafunzo hayo ya siku moja waliwahusisha waandishi toka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Mwisho.
WAKAZI wa Mji wa Kibaha waliojenga vibanda na nyumba kwenye maeneo ya barabara wametakiwa kuvunja mara moja kabla serikali haijavunja ili kupisha matengenezo ya barabara za kuingia kwenye mitaa ya mji huo.
Hayo yalisema na Injinia wa Halmashauri ya Mji huo Ezekiel Kunyaranyara alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa tayari watendaji kwenye mitaa hiyo walishapewa barua ya kuwajulisha walengwa.
Kunyaranyara alisema kuwa baadhi ya watu wamejenga vibanda vya biashara na nyumba kwenye eneo la barabara za mitaani na kufanya barabara hizo kushindwa kupitika hasa pale yanapotokea madhara mbalimbali yakiwemo ya moto.
“Athari za watu kujenga kwenye maeneo zinakopita barabara ni nyingi lakini mojawapo ni magari kushindwa kupita hata pale kunapotokea mfano mgonjwa anatakiwa kuchukuliwa na gari na kupelekwa hospitali au moto unapotokea gari la zimamoto linashindwa kupita hivyo kuleta athari kubwa,” alisema Kunyaranyara.
Alisema walitoa maelekezo kwa watendaji wa mitaa yote kwenye maeneo husika na walitoa miezi sita tangu mwaka jana hadi Machi mwaka huu ambapo endapo hawatafanya hivyo wakati wowote watatekeleza kazi hiyo.
“Katika awamu hii tulitenga kiasi cha shilingi milioni 9 kwa ajili ya kuchonga barabara zote za Mji wa Kibaha kwani lengo ni kuhakikisha mji unakuwa na barabara ambazo zinapitika kwa mkipindi chote cha mwaka,” alisema Injinia Kunyaranyara. 
Alisema kuwa hivi karibuni halmashauri ilinunua greda lake hivyo kuanza kukarabati barabara zote kwenye kata zote za halmashauri hiyo 11 zenye mitaa 53.
KUFUATIA kilio cha mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kuiomba ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuisaidia kupata fedha kiasi cha shilingi miloni 160 kwa ajili ya kukarabati mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Tumbi hatimaye kilio hicho kimesikika ambapo ofisi hiyo imeahidi kutoa fedha hizo.
Akizungumza juzi mara baada ya kutembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) lililopo wilayani Kibaha mbele ya viongozi wa shirika hilo ambalo linamiliki hospitali hiyo, Kaimu katibu mkuu TAMISEMI Alafayo Kidata alisema watatoa fedha hizo ili kufanya ukarabati wa chumba hicho.
Kidata alisema kuwa chumba hicho ni muhimu hivyo Wizara imeona kuna umuhimu wa kutoa fedha hizo ili kufanya ukarabati kwani haipendezi kuona chumba hicho kikiwa kwenye hali mbaya ambapo marehemu wanahifadhiwa humo.
“CHumba cha maiti ni muhimu sana na kila mtu atapitia hapo hivyo kiubinadamu lazima mazingirra yake lazima yawe mazuri kutokana na maombi toka kwa viongozi wa shirika tumeona mahali hapa panahitaji kuangaliwa mapema huku sehemu nyingine zikifanyiwa kazi,” alisema Kidata.
Aidha alisema kuwa kutokana na umuhimu wa hospitali hiyo kupokea majeruhi wengi wa ajali pamoja na maiti zinazopokelewa hapo ni vema ukarabati ukafanyika ili kuondoa hali mbaya iliyopo.
“Tunatarajia mwishoni mwa mwezi huu fedha zitatolewa ili kuboresha chumba hicho ambacho kwa sasa ni kidogo na kinapokea marehemu wengi,” alisema Kidata.
Alibainisha kuwa madeni mbalimbali ambayo yanafikia kiasic ha shilingi bilioni moja watahakikisha yanalipwa hadi ili huduma ziendelee kutolewa kwani kuna hatari ya baadhi ya watoa huduma kusitisha.
Awali akitoa taarifa ya shirika kwa kaimu katibu mkuu, mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa chumba cha maiti kwa sasa kinahifadhi miili miwili miwili kutokana na udogo wake jambo ambalo si zuri.
Dkt Mpemba alisema kuwa chumba hicho hakijafanyiwa matengenezo tangu hospitali hiyo ilipoanzishwa miaka ya 70 na wafadhili wa nchi za Nordic, pia linakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia zaidi ya bilioni moja.
Mwisho.

Thursday, March 7, 2013

RC AOMBA MSAADA CHUMBA MAITI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahizaameiomba ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kuipatia hospitali ya wilaya ya Tumbi kiasi cha shilingi milioni 160 kwa ajili ya kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti ambacho kiko kwenye hali mbaya.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambalo linamiliki hospitali hiyo ambalo liko chini ya Wizara hiyo.
Mahiza alisema kuwa chumba hicho kiko kwenye hali mbaya kwani kimekuwa ni kidogo na kimechakaa na hakijafanyiwa ukarabati tangu kuanzishwa miaka ya 70.
“Waziri tunaomba utusaidie kuweza kupata fedha hizo kwani licha ya kuwa na madeni makubwa na mahitaji ya fedha, kikubwa ni chumba hichi ambacho kinahitaji kufanyiwa ukarabati kwani kiko kwenye hali mbaya na kinahitaji msaada wa haraka,” alisema Mahiza.
Alisema maiti zinahitaji kuhifadhiwa katika mazingira mazuru ili kuzienzi lakini kwa hospitali yetu hali si nzuri kwani tutakuwa hatuzitendei haki kwa kuzitunza kwenye mazingira mabaya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa hospitali Peter Datan alisema kuwa tatizo la chumba hicho ni kubwa kwani kwa sasa maiti zinakaa mbili mbili ambapo kwa utaratibu wanapaswa kukaa mwili mmoja kutokana na udogo wake.
“Kwa sasa chumba kimekuwa ni kidogo kwani maiti zimeongezeka tofauti na zamani ambapo zilikuwa chache kwani kwa sasa maiti zinazohifadhiwa ni 20, pia maiti nyingine zinakaa muda mrefu hasa zile ambazo zinakuwa zimeokotwa,” alisema Dkt Datan.
Dkt Datan alisema kuwa chumba hicho kinapata mzigo mkubwa wa maiti kutokana na baadhi ya maeneo ya mikoa kama vile Dar es Salaam, Morogoro na Tanga kuletwa TUmbi.
Naye Mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa wanakabiliwa na madeni makubwa ambayo kwa sasa yanafikia zaidi ya bilioni moja hali ambayo ni madai ya wafanyakazi na wazabuni ambao wanatoa huduma kwao.
Kwa upande wake waziri Ghasia alisema kuwa atayafanyia kazi maombi hayo kwa kupeleka ombi maalumu hazina ili kuweza kutatua chanagamoto zilizopo kwenye shirika hilo la Umma ambalo lilianzishwa miaka ya 70 na nchi za Nordic kwa ushirikiano na serikali.
Mwisho.  

WAWILI WAFA


Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MLINZI wa kampuni ya ulinzi ya S&M ambaye alikuwa akilinda ofisi ya DAWSCO wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Juma Hassan (45) ameuwawa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi baada ya kuvamia ofisi hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa watu hao ambao idadi yao haikuweza kufahamika mara moja walimteka kasha kumtupa baada ya kumfunga kamba miguuni na mikononi pia walimziba na plasta mdomoni na puani.
Alisema kuwa baada ya kumteka waliingia kwenye ofisi hiyo na kuiba kompyuta nne ambazo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja kasha kutoweka.
“Tunaendelea na upeelelezi kujua ni watu gani waliofanya tukio hilo la kusikitisha na tunawaomba wananchi kutoa taarifa endapo watasikia juu ya watu walio husika na tukio hilo.
Alisema kwenye tukio linguine makazi wa Mkoani Kibaha Amani Aidan au Mgaya (24) amepoteza maisha baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kugongana na gari.
Kamanda Matei alisema tukio hilo lilitokea Machi 5 saa 1 usiku eneo la TAMCO barabara ya Dar es Salaam – Morogoro ambapo pikipiki hiyo ili gongana na gari namba T 787 AWC aina ya Toyota Coaster lililokuwa likiendeshwa na Thadei Makala (58).
Aidha alisema katika ajali hiyo mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Amina (22) mkazi wa Picha ya Ndege Kibaha alikimbizwa hospitali ya Tumbi kwa matibabu zaidi baada ya kupata majeruha sehemu za kichwani kulia.
Mwisho.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamtafuta Ramadhan Mfaume maarufu kama Ngosha kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya Short Gun na fuvu la mnayama aina ya Fungo na Ngiri.
Akizungmza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani hapo Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 4 mwaka huu.
 Kamanda Matei alisema kuwa vitu hivyo vilikamatwa nyumbani kwake kwenye eneo la Fitina haina Posho Kijiji cha Mwavi kata ya Fukayosi wilaya ya Bagamoyo.
 Aidha alisema kuwa mbali ya silaha hiyo ambayo namba zake hazikuweza kufahamika mara moja pia kulikutwa risasi 29.
Alisema mtuhumiwa huyo alitoroka na anatafutwa kuhusiana na tukio hilo na kuwataka wananchi kutomiliki silaha hizo bila ya kibali ili kuepukana na mkono wa sheria.
Mwisho. 


Tuesday, March 5, 2013

MADENI MAKUBWA SHIRIKA



WAAFANYAKAZI na Wazabuni mbalimbali wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) mkoani Pwani wanalidai shirika hilo kiasi cha zaidi ya shilingi biloni moja.
Hayo yalisemwa juzi na mkurugenzi wa shirika hilo Dkt Cyprian Mpemba, wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia.
Dkt Mpemba alisema kuwa madeni hayo ni ya wazabuni wanaodai kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 286, wafanyakazi wanaodai zaidi ya shilingi milioni 277 na makandarasi mshauri wa hospitali ya Tumbi anayedai kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 600.
“Madeni hayo ni changamoto kwetu kwani ruzuku inayotolewa na serikali haitoshelezi kabisa ambapo kwa bajeti ya mwaka 2010/2011 fedha zilizotolewa na serikali zilikuwa ni pungufu kwa asilimia 15 huku bajeti ya mwaka 2011/2012 ilikuwa pungufu kwa asilimia 48,” alisema Dkt Mpemba.
Alisema mbali ya madeni hayo pia shirika lina mahitaji makubwa ambapo wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kumalizia jengo la hospitali, zaidi ya bilioni moja, milioni 500 kwa ajili ya mafunzo kwa madaktari bingwa na wasaidizi, uchakavu wa majengo kiasi cha shilingi milioni 300, matengenezo ya magari na majengo zaidi ya milioni 131, maji, umeme, bima, madawa na shajala shilingi zaidi ya milioni 143, chumba cha kuhifadhia maiti shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukarabati.
“Kutokana na changamoto ya fedha ripoti ya mkaguzi mkuu wa serikali ya mwaka huu imetahadharisha kuwa shirika lipo kwenye hatari ya kushindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani inaonekana mahesabu ya shirika yana mwelekeo mkubwa wa uhaba wa kumudu kulipa watoa huduma wastani wa bilioni moja,” alisema Dkt Mpemba
Aidha alisema wastani wa mapato ya ndani ya shirika hilo ni kati ya shilingi milioni 800 na bilioni moja kwa mwaka ambazo hazikidhi matumizi stahiki kwa idadi ya watumishi waliopo 985 hivyo kuiomba serikali kuongeza ruzuku ya mwaka kutoka bilioni 1.9 na kufikia bilioni 3.6.
Akijibu hoja hizo Waziri Ghasia alisema kuwa kuhusu madeni watalifanyia kazi suala hilo ili kuweza kupunguza chanagamoto ya ukosefu wa fedha kwenye shirika hilo la Umma ambalo limekuwa na mchango mkubwa ambayo ni kutoa huduma za kielimu, afya na kupambana na umaskini.
‘Pia  ifike wakati mwende kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kukopa kuliko kutegemea ruzuku ya serikali ambapo kwa bajeti iliyopita hali ya kifedha haikuwa nzuri, kwani mashirika ya umma yanatakiwa yajiendeshe yenyewe na si kuisubiri serikali pekee,” alisema Ghasia.
Alisema KEC ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo ufugaji kuku na ng’ombe endapo vitapatiwa fedha litaweza kujiendesha kwa kiasi fulani hivyo kumudu kufanya shughuli zake za kila siku, awali Waziri alitembelea mashamba ya kuku, kiwanda cha kutengenezea trei za mayai na hospitali ya Tumbi akiwa na uongozi wa shirika na bodi.
Mwisho.  

Friday, March 1, 2013

MTOTO AUNGUZWA NA MAJI YA MOTO




Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Mtaa wa Kwa Mfipa wilayani Kibaha Nuru Rashid amewashangaza wakazi wa mtaa huo kwa kushindwa kumpeleka hospitali mwanae mwenye umri wa miaka miwili na nusu baada ya kuungua na maji ya moto.
Akizungumza na baba mzazi Ally Said alisema mwanae ambaye ni wa jinsi ya kiume ameungua kifuani na kusababisha kidonda kikubwa hadi kwenye mkono wake wa kushoto hakumpatia matibabu yoyote hadi siku iliyofuata.
Said alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 27 mtaani hapo nyumbani kwa mama yake mazazi ambaye walitengana naye zaidi ya mwaka mmoja uliopita ambapo aliolewa na mume mwingine.
“Mimi baada ya kupata habari juu ya mwanangu kuunguzwa na maji siku iliyofuata nilikwenda nyumbani kwake kutaka kumchukua mwanangu ili nimpeleke hospitali lakini alikataa na kusema hadi baba yake wa kambo aje jambo ambalo alilikataa na kumchukua kwa nguvu,” alisema Said.
Alisema kuwa mkewe amekuwa akimficha juu ya matatizo hasa pale anapoumwa na mbaya ni pale alipomficha mwanae baada ya kuungua na kushangaa ni kwanini hataki kumpeleka hospitalini.
Jitihada za kumpata mama huyo yazikuweza kuzaa matunda licha ya mwandishi kufika nyumbani kwake na kuambiwa kaenda dukani na hata aliposubiriwa hakuweza kutokea.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo Hai Hai alikiri kupata tukio hilo na kusema kuwa ukweli halisi alikuwa nao mama huyo ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na mtoto huyo ambaye alikuwa akilia kutokana na maumivu makali aliyoyapata.
Hai alisema kuwa hatua aliyoichukua ni kuandika barua ambayo ilibidi ipelekwe polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria na kupatiwa matibabu kwa mtoto huyo na kusema hicho ni kitendo cha unyanyasaji na kuwanyima haki watoto wadogo.
Mwisho.     
 Mtoto aliyeunguzwa na maji ya moto akiwa amepumzika huku nyumbani kwao huko Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani (Picha na John Gagarini)






MBUNGE ALIPA HASARA ILIYOSABABISHWA NA MGAMBO


Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka amelazimika kuwalipa fedha kiasi cha shilingi 275,000 wanawake watatu wanaouza samaki baada ya mgambo wa kata ya Maili Moja kumwaga samaki wao kwa madai ya kukiuka kanuni za afya.
Koka ilibidi alipe fedha hizo kwa wafanyabiashara hao baada ya kuangua kilio mbele ya mbunge huyo wakati wa mkutano na wananchi wa Kibaha.
Alisema hayo yalikuwa makosa ya kibinaadamu yaliyofanywa na mgambo hao wakati wakitekeleza zoezi la usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha.
“Suala la afya ni muhimu na mgambo hawa waliteleza na kujikuta wakiharibu mali za wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki zao huku wengine wakiwa wamekopa fedha kwa ajili ya kufanyia biashara hiyo,” alisema Koka.
Mbunge huyo alisema kuwa kuanzia sasa wafanyabiashara na mgambo hao kwa kushirikiana na ofisi ya afya ya kata kila upande kufuata kanuni na sheria ili kufanikisha suala la afya.
Kwa upande wao wakinamama hao mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Said alisema kuwa mgambo hao walifika kwenye biashara yake na kusema kuwa kwakuwa hakupima afya yake na kuwamwaga samaki wake wenye thamani ya shilingi 65,000.
Naye mfanyabiashara mwingine Nuru Msangi alisema kuwa mgambo hao walichukua samaki wake wenye thamani ya shilingi 75,000 na kuzimwaga kwa madai kuwa naye hakupima afya yake.
Alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanashindwa kupima afya zao kutokana na gharama kubwa ya kupima ya shilingi 5,000 na pia walisema wao kama wanshinikizwa kupima je kwa wateja wanaokwenda kununua mbona hawabanwi.
Mbunge huyo alizitaka pande mbili hizo kati ya idara ya afya ya kata hiyo na wafanyabiashara kuanza mahusiano mazuri upya ili kuondoa ugomvi unaojitokeza mara kwa mara pia halmashauri itoe elimu juu malipo hayo ya kupima afya ya shilingi 5,000.
Mwisho.