Saturday, February 16, 2013

STORY PWANI



Na John Gagarini, Mkuranga
IMEELEZWA kuwa kuishi mbali na vituo vyao vya kazi kwa baadhi ya maofisa
ugani kwenye vijiji wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani kumechangia kudumaza
shughuli za kilimo wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo kwenye kijiji cha
Msufini kata ya Mbezi, mratibu wa mradi wa Wajibu wa Jamii Katika Usimamizi
wa Rasilimali za Umma za Sekta ya Kilimo wilaya hiyo (POCUSO), Bw Said
Gwaja alisema kuwa maofisa hao wamekuwa hawafiki kwenye vijiji
walivyopangiwa.

Bw Gwaja alisema kuwa kutokana na kuishi mbali na vituo vyao vya kazi
wamekuwa wakiishia ofisini na kushindwa kwenda kwenye maoeneo waliyopangiwa
hasa yale ya vijijini.

“Ni vema wangekaa kwenye maeneo yao ya kazi ili iwe rahisi kwao kutoa
huduma kwa wakulima ambao wanakosa fursa nyingi kutokana na kutofahamishwa
namna ya kuweza kuzipata,” alisema Bw Gwaja.

Alisema kuwa fursa ambazo wakulima walipaswa kuzijua zinashindwa kuwafikia
kwani wanazipata wakati muda wa kilimo unakuwa umepita hivyo kushindwa kupata pembejeo za ruzuku kwa wakati muafaka.
Aidha alisema kuwa endapo wangekuwa wanafanya kazi kwenye maeneo waliyopangiwa hususani vijijini ingekuwa raisi kwao kujua chanagamoto zinazo wakabili wakulima hivyo ingekuwa rahisi kuwasaidia kuliko ilivyosasa.
Aliwataka wakulima kujitokeza kwenye mafunzo yanayoandaliwa na shirika lake ili waweze kujua namna ya kufuatilia matumizi ya rasilimali za wananchi zikiwemo zile za kilimo ambazo nyingine zinawalenga wao moja kwa moja.
Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

WATANZANIA wametakiwa kuwekeza kwenye hisa za makampuni na taasisi za fedha nchini badala ya kuwaachia wageni pekee ili  nao wamiliki makampuni na taasisi hizo.
Hayo yamesemwa na mjumbe wa bodi ya soko la hisa Dar es Salaam  Bw Arphaxad Masambu  wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha.

Bw Masambu alisema Watanzania wengi hawana tabia ya kuwekeza katika hisa za makampuni mbalimbali na kusababisha makampuni mengi na taasisi nyingi nchini kumilikiwa na wageni kutoka katika mataifa ya nje na kuwaacha wazawa wakiwa masikini wa kipato.

“Faida ya kununua na kumiliki hisa kuwa si kwa mnunuzi wa hisa pekee bali ni pamoja na vizazi yaani watoto wajukuu, vitukuu kunufaika na hisa hizo,” alisema Bw Masambu.

Alisema kuwa uuzaji wa hisa za makampuni na taasisi ni kwaajili ya kuonfgeza nguvu ya pamoja katika kuendesha na kusimamia kampuni hizo na taasisi hizo ili kuzalisha na kutoa faida yenye tija kwa wengi zaidi.

Naye Mwenyekiti wa chemba ya wafanyabiashara (TCCIA) mkoa wa Pwani Bi Kasa Mlonja aliwataka wananchi, wakulima na wafanyabiashara kuwekeza katika hisa mbalimbali zinazouzwa katika taasisi za fedha na makampuni ilikuwa na madaraka kamili ya hizo kampuni na taasisi kwa lengo la kuendeleza nchi yetu.

Mwisho.   
Na John Gagarini, Kibaha
DIWANI wa kata ya Maili Moja Bw Andrew Lugano amesikitishwa na mamalaka ya maji safi na majitaka (DAWASCO) kushindwa kuwahudumia wananchi hali inayosababisha kukosa maji kwa zaidi ya mwezi sasa.
Akizungumza mara baad aya kufanya ziara kwenye kata hiyo kuangalia maeneo ambayo yamekuwa yakikosa maji kwa muda mrefu, huku akiwa ameambatana na meneja wa DAWASCO Bw Robert Mugabe alisema kuwa hakuna sababu ya wananchi kukosa maji kwa muda wote huo na uongozi upo.
Bw Lugano alisema kuwa amekuwa akipata kero hiyo ya maji toka kwa wananchi na jitihada zake za kufuatilia zimekuwa zikigonga mwamba hali iliyomlazimu kumtoa meneja huyo ofisini kwake Jumamosi na kumwonyesha jinsi gani wananchi wanavyotaabika kwa kukosa maji.
“Siwezi kukubali kuona wananchi wakihangaika kutafuta maji huku chanzo cha maji kikiwa jirani hivyo lazima kampuni hiyo ijali wananchi ili waondokane na kero hiyo,” alisema Bw Lugano.
Moja ya wakazi wa kata hiyo ambaye anakaa mtaa wa Mzimuni Bw Mohamed Atiki alisema kuwa wamekuwa wakipata tabu kubwa ya kupata maji hali inayowasababisha kununua maji kwa bei ya shilingi 500 kwa dumu la lita 20.
“Tumekuwa tukihangaika kwa kipindi kirefu licha ya kutoa taarifa ya ukosefu wa maji kwenye kampuni hii ya maji hivyo lazima wabadili utendaji kazi wao,” alisema Bw Atiki.
Kwa upande wake meneja wa DAWASCO Kibaha Bw Robert Mugabe alisema kuwa tatizo kubwa lililosababisha wananchi kukosa maji ni kutokana na ujenzi wa barabara katika kata hiyo.
“Mabomba mengi yamekatwa kutokana na ujenzi wa barabara lakini hata hivyo tayari tumewasiliana na mkandarasi ili kuangalia namana ya kuweza kurekebisha hali hiyo,” alisema Bw Mugabe.
Bw Mugabe alisema kuwa tayari wameshafanya tathmini ya uharibifu uliofanyika na wakati wowote wataanza kufunga mabomba yaliyokatwa ili wananchi hao waendelee kupata maji kama kawaida.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
IMEELEZWA ukosefu wa vifaa kwa watoto wenye ulemavu 89 wilayani Kisarawe mkoani Pwani wameshindwa kuanza masomo kutokana na kukosa vifaa vya kusomea.
Hayo yalisemwa na katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wilayani Kisarawe Bw Ibrahim Tully alisema kuwa jumla ya watoto wenye ulemavu katika wilaya hiyo ni 218.
Bw Tully alisema alisema kuwa kati ya watoto hao ni 34 hivyo kuwafanya watoto hao kushindwa kuanza shule hadi kufikia umri wa miaka 12 na kuendelea.
“Tatizo hilo linasababishwa na uhaba wa fedha wa kununua vifaa hivyo kutoka kwa wazazi na kukosekana kwa wafadhili wa kudumu kusaidia hali hiyo,” alisema Bw Tully.
Aidha alisema mbali ya hayo ,tatizo jingine kubwa ni baadhi ya wazazi na walezi kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu wanaoishi nao kwa kuona aibu kuwaanzisha shule jambo linalowanyima haki yao msingi.   
“Tunakabiliana na hali hiyo kwa kutafuta wafadhili ili kusaidia upatikanaji wa baiskeli maalum kwa ajili ya watoto hao waweze kwenda shule,” alisema Bw Tully.
Bw Tully alisema katika jitihada hizo tayari wamepata baiskeli  50 za aina hiyo na kati ya hizo 10 wamezigawa kwa watoto wa Tarafa ya Chole na nyingine 40 zilizobaki watazigawa kwa watoto wenye ulemavu katika kata zilizopo wilayani kisarawe.
Pia wilaya hiyo ina changamoto ya ukosefu wa shule maalum ya watoto wenye ulemavu ikiwemo wenye ulemavu wa akili ambao  hawawezi kuchanganywa na watoto wengine kwasababu ya mahitaji yao kuhitajika kuwa rafiki zaidi.
Hata hivyo alisema kufuatia tatizo hilo jitihada za hali na mali zinafanyika kujenga shule hiyo mwaka huu ambapo wameshapata eneo lenye heka 100 katika kijiji cha Kidugalo  kata ya Mzenga na mchakato wa kupata hati unaendelea.
Mwisho                                                                                     
Na John Gagarini, Bagamoyo
VIONGOZI wa vikundi vya ujasiriamali kwenye kata ya Msata wilayani Bagamoyo wametakiwa kutumia fedha wanazopewa na sereikali na wafadhili mbalimbali kuzitumia kwa mipango waliojiwekea ili waweze kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Kata ya Msata Bw Edgar Nazar wakati
akizungumza na kikundi cha Lulenga kinachojihusisha na ufugaji
nyuki na mazingira ambacho kimepatiwa zaidi ya sh. Mililioni nne  kwa ajili ya
utoaji wa elimu inayohusiana na sekta ya nyuki.

Bw Nazar alisema kuwa serikali na wadau mbalimbali wa maenedeleo wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo kupitia vikundi hivyo lazima zitumike kwa malengo husika.
“Serikali  imekuwa ikielekeza masuala mbalimbali yanayohusiana na ujasiliamali na
ushahidi huo ni huu wa Wizara ya Misitu kutoa kiasi hiki cha fedha kwa
ajili ya kuendeleza ufugaji nyuki na mazingira, niwaombe fedha hizi
zitumike kama zilivyolengwa,” alisema Bw Nazar.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho Bw Douglas Kilomo alisema kuwa kwa msimu wa mwaka uliopita kulikuwepo na mgongano kati yao na
wafugaji jamii ya wamasai hali iliyosababisha kusimama kwa shughuli
zetu kutokana na mgongano huo,” ilieleza sehemu ya taarifa.

Bw Kilomo alisema uwa zoezi la ufugaji nyuki linaendana na sanjali na utunzaji wa
mazingira hivyo amewaasa kuzingatia hayo ili kujiletea mafanikio katika zao la asali ambalo kwa sasa lina soko kubwa.

“Ufugaji nyuki ni sekta ambayo haihitaji mtaji mkubwa kama ilivyo
miradi mingine, unapokuwa na mzinga tu unasubiri mazao ambapo kwa
mwaka unavuna mara tatu sawa na sh. Laki 9 hivyo niwaombe muwe makini
kwa hilo,” alisema Bw Kilomo.

Naye mmoja wa wanakikundi Bw Mohamed Mrisho ameeleza kuwa mafunzo hayo anaimani yatawaongezea ufanisi wa shughuli zao na kujiongezea kipato chao.

MWISHO.

Friday, February 15, 2013

MWANAFUNZI AJINYONGA


Na John Gagarini, Kibaha
MWANAFUNZI wa darasa la kwanza wa  shule ya Msingi Mbaya, Geuza Patrick (12) amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani Gregory Mushi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 13 mwaka huu majira ya saa 12 jioni huko kitongoji cha Msufini tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Bw Mushi alisema kuwa mwanafunzi huyo alijinyonga kwenye Mti wa Mwembe nyumbani kwao.
Alisema kuwa chanzo cha kujinyonga bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
Aidha alisema mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHULE ya Sekondari ya Bundikani ya Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha imeanza kuchukua hatua kali kwa wanafunzi wanaovaa suruali za kubana maarufu kama modo kwa kuzichana.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Flora Chibululu alisema kuwa juzi walichana suruali za wanafunzi watatu kutokana na kwenda shuleni na suruali hizo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa na tabia ya kuzirekebisha  kwa kuzibana suruali hizo licha ya kuwa zinashonwa kawaida na kukiuka taratibu za shule.
“Suruali hizo za shule hushonwa vizuri lakini wao huzipeleka kwa fundi na kuzibana sawa na miili yao maarufu kama modo, tulishawapiga marufuku kuzibadili nguo hizo lakini wanakaidi hali iliyotufanya tuchukue hatua hiyo ili kuleta nidhamu shuleni,” alisema Bi Chibululu.
Bi Chibululu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikiuka taratibu za shuleni na kuiga tabia ambazo zinashusha taaluma hivyo shule itakabiliana na vitendo kinyume cha taratibu za shule.
Aidha alisema wataendelea kuzichana suruali hizo kwa mwanafunzi atakaye vaa kinyume cha sheria za shule kwani huo ni utovu wa nidhamu na lazima wanafunzi wafuate taratibu za shule.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kibaha
AKINA Mama Lishe na Baba Lishe kwenye kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa sheria ili waweze kuhudumia wateja wao wakiwa na afya njema vinginevyo watapelekwa mahakamani kwa kukiuka kanuni za afya.
Hayo yalisemwa na ofisa afya wa kata hiyo Bw Ally Shah, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha na kusema kuwa watakao kataa kupima afya watapelekwa mahakamani.
Bw Shah alisema kuwa hivi karibuni baadhi ya wahusika waligoma kwenda kupima afya zao wakidai kuwa kiwango cha kupima ambayo ni shilingi 5,000 ambayo ilipangwa na halmashauri kuwa ni kubwa.
“Makundi hayo yanatakiwa kupima afya ili kutoa huduma wakiwa na afya njema ili kuepuka maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu na magonjwa ambayo yanaambukizwa kwa haraka,” alisema Bw Shah.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa na hofu ya kupima afya kuwa wataonekana na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI jambo ambalo alisema kuwa upimaji huo hauhusiani na kupima vipimo vya ugonjwa huo.
“Wasihofie kupima afya kwani magonjwa yanayopimwa hayahusiani na ugonjwa huo na kama mtu anataka kupima ugonjwa huo ni hiyari yao wenyewe na si kwa lazima kama sheria inavyoelekeza,” alisema Bw Shah.
Aidha alisema kuwa magonjwa yanayopimwa ni pamoja na magonjwa ya zinaa, kifua kikuu na haja kubwa hivyo wafanyabiashara wapime kwani ni kwa faida yao na wateja wanaowahudumia.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wanaendelea na kuboresha usafi wa mazingira ambapo vimeundwa vikundi mbalimbali vya usafi kwa ajili ya kuhakikisha mazingira ya Mji wa Kibaha ambapo sheria ndogondogo ya halmashauri inawatoza kiasi cha shilingi 50,000 kwa mtu atakayetupa uchafu kiholela.
Mwisho.

Thursday, February 14, 2013

TANESCO YAONDOA RIBA KWA WATEJA WANAODAIWA

Na John Gagarin, Kibaha
SHIRIKA la ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani imeanza utaratibu wa kuingia mkataba na wadeni wake kwa kuwaondolea riba ya madeni yao katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TANESCO mkoa huo Bw Jonson Mwigune, alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwapunguzia mzigo wateja wao.
Bw Mwigune alisema kuwa mbali ya kuwaondolea riba ya madeni yao kwa kipindi hicho pia watakuwa wakilipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza madeni.
“Mkataba huo utawawezesha wateja wetu kupata nafuu ya madeni pia atarejeshewa umeme huku akiendelea kulipa kidogokidogo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mteja alikatiwa umeme hadi atakapomaliza deni lake,” alisema Mwigune.
Alisema kuwa kwa sasa shirika liko kwenye mkakati wa kupunguza madeni kwa wateja wao ambapo moja ni kuingia mikataba na wateja wao ili waonyeshe jinsi gani watakavyolipa huku wakiendelea kupata huduma.
“Mkakati mwingine wa kupunguza madeni ni kuweka Luku ambapo kwa sasa asilimia zaidi ya 95 wameshaunganishwa kwenye mfumo huo ambao mteja hulipia kadiri anavyotumia,” alisema Bw Mwigune.
Aidha alisema mkakati ni wateja wote kutumia Luku ambapo Wizara ya Nishati na Madini imepunguza gharama za umeme kwa asilima 30 ili wananchi wengi waweze kuwa na umeme huku mkoa ukiwa na mpango wa kuwafikia wateja 17,500.
Aliwataka wananchi kushirikiana na shirika hilo kulinda miundombinu ikiwa ni pamoja na nyaya, mafuta na mafuta yake ili kutosababisha umeme kukatika
Mwisho.   

UBALOZI MISRI WATOA MSAADA HOSPITALI


Na John Gagarini, Bagamoyo

UBALOZI wa Misri nchini umetoa msaada ya vifaa mbalimbali vya kisasa katika hospitali ya wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.

Vifaa hivyo vilivyotolewa ni Madawa, Vitanda pamoja na vya wodi ya upasuaji kwa ajili ya kuboresha hudum za afya kwenye hospitali hiyo.  
 
Akikabidhi vifaa hivyo balozi wa Misri hapa nchini Bw Hossam Eldin Moharam alisema wananchi wa Misri wameamua kutoa msaada huo kwa  marafiki zao wa Bagamoyo ili kudumisha na kuenzi urafiki wa muda mrefu baina ya wananchi wa nchi hizo mbili.
 
Bw Moharam alisema kuwa hapendi kuita ni msaada wa vifaa walivyovitoa kutokana na ukaribu na urafiki  uliopo baina ya nchi hizo.
 
“Tunaomba vifaa hivi vilivyotolewa kwenye hospitali hii vilindwe kwani vinahitaji uangalizi mkubwa ili viweze kusadia kutoa huduma bora za afya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Bw Shukuru Mbatto alisema msaada huo ni chachu kwa watumishi wa hospitali hiyo katika uboreshaji wa utoaji  huduma bora .
 

Naye mmoja wa wadau waliofanikisha upatikanaji wa msaada huo, Bw Yusuph Kikwete alisema akiwa ni kiongozi wa muungano wa marafiki wa Bagamoyo walizungumza na balozi huyo kuhusiana na ombi la msaada wa vifaa kwa ajili ya maabara mpya ya hospitali hiyo .
 
 Mwisho

TANESCO KUONDOA RIBA KWA WATEJA WENYE MADENI


Na John Gagarin, Kibaha
SHIRIKA la ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani imeanza utaratibu wa kuingia mkataba na wadeni wake kwa kuwaondolea riba ya madeni yao katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TANESCO mkoa huo Bw Jonson Mwigune, alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwapunguzia mzigo wateja wao.
Bw Mwigune alisema kuwa mbali ya kuwaondolea riba ya madeni yao kwa kipindi hicho pia watakuwa wakilipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza madeni.
“Mkataba huo utawawezesha wateja wetu kupata nafuu ya madeni pia atarejeshewa umeme huku akiendelea kulipa kidogokidogo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mteja alikatiwa umeme hadi atakapomaliza deni lake,” alisema Mwigune.
Alisema kuwa kwa sasa shirika liko kwenye mkakati wa kupunguza madeni kwa wateja wao ambapo moja ni kuingia mikataba na wateja wao ili waonyeshe jinsi gani watakavyolipa huku wakiendelea kupata huduma.
“Mkakati mwingine wa kupunguza madeni ni kuweka Luku ambapo kwa sasa asilimia zaidi ya 95 wameshaunganishwa kwenye mfumo huo ambao mteja hulipia kadiri anavyotumia,” alisema Bw Mwigune.
Aidha alisema mkakati ni wateja wote kutumia Luku ambapo Wizara ya Nishati na Madini imepunguza gharama za umeme kwa asilima 30 ili wananchi wengi waweze kuwa na umeme huku mkoa ukiwa na mpango wa kuwafikia wateja 17,500.
Aliwataka wananchi kushirikiana na shirika hilo kulinda miundombinu ikiwa ni pamoja na nyaya, mafuta na mafuta yake ili kutosababisha umeme kukatika
Mwisho.     

Tuesday, February 12, 2013

WANANE WAFA AJALINI


Na Mwandishi Wetu, Kibaha

WATU nane wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika Kitongoji cha Kibiki Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
                   
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa kati ya watu waliokufa wanafunzi ni wanne.

Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 11 majira ya jioni na kuyahusisha magari T363 AZG aina ya Toyota Mark II likitokea mkoani Tanga kwenda Morogoro likiendeshwa na Bw Abuu Ahmed na kugonagana na gari namba T 433 AYQ aina ya Mitsubishi Fuso likitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Bw Mweta Daniel.
 
“Chanzo cha ajali  hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa Toyota Mark II ambaye alipoteza mwelekeo baada ya kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake kisha kugongana uso kwa uso na Fuso lililokuwa likitokea mbele na kusababisha vifo hivyo,” alisema Kamanda Matei.
 
Kamanda Matei aliwataja waliokufa kuwa ni Esaau Enos (16) aliyekuwa kidato cha tatu, Bahati Mbene  (18) kidato cha nne, Latifa Shabani (17) kidato cha nne na Stella Kazimoto (18) wote  wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze.
 
“Wengine ni Maria Lelela na mtoto wake Samweli Ismail kati ya miaka mitatu au minne, Hassan Kalunga na Abuu Ahmed dereva wa gari dogo,” alisema Kamanda Matei.
 
Aidha alisema kuwa majeruhi ni William Tobias na  Ahmada Juma aliyekuwa utingo wa fuso ambapo dereva wa Fuso anashikiliwa na Jeshi la polisi kwa uchunguzi zaidi.
 
Alitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kudai kuwa Jeshi hilo halitowavumilia madereva wazembe kwa kuwakamata na kuwachukuliwa hatua kali wote watakaoshindwa kutii sheria za usalama barabarani.
           
MWISHO