Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa kushirikiana na Maafisa usafirishaji Wilaya ya Kibaha (bodaboda) limezindua zoezi la uvaaji viakisi mwanga katika Wilaya hiyo ili kuwezesha kuwa rasmi na kuepuka kukumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuporwa vyombo vyao vya moto.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Pius Lutumo amewataka maafisa hao kuhakikisha wanajisajili katika kanzi data ili kutambulika wao na vijiwe wanavyofanyia kazi.
Amesema endapo wadau hao watajisajili kati kanzi data na kutii sheria za usalama barabarani ajali zitapungua kwa kiasi kikubwa, matukio ya wizi kwa kutumia Bodaboda yatakwisha na wahalifu wanaojificha kwa mgongo wa bodaboda watadhibitiwa.
Lutumo amewakumbusha madereva waliosajiliwa kwenye kanzi data kutowaazima viakisi mwanga vilivyo na namba za utambulisho kwa wenzao ambao hawajajisajili kwani wanaweza kufanya matukio ya kihalifu na viakisi mwanga vikatumika kama utambulisho wa watuhumiwa hao kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Maafisa Usafirishaji Wilaya ya Kibaha Mwinyichande Mungi amesema watatekeleza zoezi hilo kwa weledi na kuhakikisha kila anayetaka kufanya kazi hiyo anafuata taratibu ikiwa ni pamoja na kujisajili na kupata namba ya utambulisho.
Aidha mwenyekiti wa CCM Kata ya Kongowe Saimon Mbelwa amewataka madereva hao kutambua kazi yao ina mchango mkubwa kwa jamii hivyo wale wenye kuingia kwenye kazi hiyo kwa lengo la kufanya vitendo vya Uhalifu wanapaswa kupigwa vita na kufichuliwa.
No comments:
Post a Comment