Tuesday, July 16, 2024

WATAKIWA KUACHA IMANI ZA KISHIRIKINA KUPATA UONGOZI











VIONGOZI wanaowania nafasi za uongozi wametakiwa kuacha kuwa na imani kuwa viungo vya watu wenye Ualbino vinasaidia kupata uongozi.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Diwani wa Viti Maalum Lyidia Mgaya wakati wa Kongamano la kupinga ukatili dhidi ya ya watoto na watu wenye Ualbino Halmashauri ya Mji Kibaha. 

Mgaya amesema kuwa kumekuwa na dhana kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaweza vikamfanya mtu akapata uongozi au mali hali ambayo inasababisha vitendo vya ukatili.

"Uongozi hutolewa na Mungu na siyo viungo vya binadamu na hata mali hazipatikani kwa kutumia viungo bali ni kutokana na jitihada za mtu mwenyewe kwa uongozi ni kuwajibika na mali ni kuwa na jitihada,"amesema Mgaya.

Amesema kuwa kutokana na dhana hizo potofu zimeendelea kuwafanyia ukatili watu wakiendekeza mila ambazo ni potofu na zinapaswa kupigwa vita.

"Jamii ifike wakati iachane na dhana potofu ambazo zina athari kwa watu wengine na zinasababisha jamii nyingine isiishi kwa amani tuziache na kupiga vita kwa nguvu zote,"amesema Mgaya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jukwaa la Vipaji Tanzania (ATF) Maryrose Bujashy amesema kuwa wameandaa kongamano hilo ni kutambua viashiria vya ukatili wa watoto na watu wenye albino na namna ya kudhibiti.

Bujashy amesema kuwa kutokana na matukio kadha ya ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ualbino ndiyo sababu ya kuandaa kongamano hilo ambalo wameshirikiana na asasi mbalimbali za serikali na zile zisizo za kiserikali ili kutambua uelewa wa wadau mbalimbali kuhusu swala hilo na kujua namna gani linaweza kupunguzwa au kutatuliwa.

Amesema wanatarajia kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutia elimu juu ya malezi ya watoto, watu wenye ulemavu, watu wenye ualbino, viashiria vya ukatili juu ya watoto na watu wenye ulbino na mjadala juu ya namna ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ualbino.

Aidha amesema kuwa matarajio baada ya kongamano hilo ni watoto na watu wenye ualbino kujua namna ya kutambua viashiria vya ukatili na namna ya kupambana navyo na jamii kujua wajibu wao katika kutunza watoto na watu wenye ualbino.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment