WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na mkoa huo wametakiwa kuandika ombi maalumu la fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo ya uwekezaji.
Hayo yemesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Denis Londo wakati wa majumuisho ya ziara ya siku moja kutembelea barabara zilizojengwa na Tarura Mkoa huo.
Londo amesema kuwa kutokana na mkoa huo kuwa na uwekezaji mkubwa hasa wa viwanda ambao una manufaa kwa Taifa ni vema wakaomba maombi maalumu ya fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara badala ya kuomba kidogo kidogo.
"Angalieni mahitaji ya barabara zote ambazo zinahitajika kwenye maeneo muhimu ya uwekezaji badala ya kuomba sehemu chache ili muweze kuboresha kwa pamoja,"amesema Londo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kukiwa na miundombinu mizuri ya barabara kwenye maeneo hayo kutakuwa ni kivutio kwa wawakezaji kuendelea kuwekeza.
Kunenge amesema kuwa Tarura imeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilometa 12.5 kwenye eneo la viwanda la Zegereni yenye thamani ya shilingi bilioni 16.4 ambayo imekamilika kwa sasa ikiwa kwenye muda wa matazamio.
Naye Meneja wa Tarura Mkoa wa Pwani Mhandisi Leopold Runji alisema miradi mitatu ambayo imetembelewa na kamati hiyo ni kutoka barabara ya Morogoro kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha yenye urefu wa mita 300 na umekamilika unathamani ya shilingi milioni 500.
Runji alisema kuwa barabara nyingine ni Visiga Zegereni ni eneo la viwanda kiwango cha lami kilometa 12.5 tunamshukuru kutoa fedha bilioni 16.4 na umekamilika sasa kipindi cha matazamio barabara nyingine ni ya Picha ya Ndege Boko Timiza kilometa 7.8 ambapo hadi sasa zimekamilika kilometa 1.2 awamu ya kwanza milioni 950 kwa awamu ya kwanza ujenzi huku ukiwa na awamu tatu.
Mjumbe wa Kamati hiyo Saasisha Mafuwe alisema kuwa katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Tarura kuwe na kiwango maalum cha gharama za ujenzi ijulikane mfano kwa kilometa na kuwe na bei maalumu siyo kila mtu kujenga kwa utashi ambapo gharama zinatofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Kamati hiyo ilitembelea barabara za Picha ya Ndege-Boko Timiza, barabara kuelekea ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Visiga Zegereni na kuridhishwa na ujenzi wa barabara hizo.
No comments:
Post a Comment