Saturday, July 6, 2024

WATUMISHI WA HALMASHAURI WATOA MISAADA MAKAO TISA YA WATOTO






WATUMISHI wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kushirikiana na Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha pamoja na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya CRDB wametoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa makao tisa ya vituo vya kulea yatima.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa watoto hao kwenye sherehe ya makabidhiano iliyofanyika kwenye kituo cha Shallom kilichopo Kidenge Kata ya Mkuza Wilayani Kibaha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema kuwa wako na watoto hao hivyo wasijione wapweke.

Shemwelekwa amesema kuwa wao na watoto hao ni familia moja hivyo wameamua kuwasaidia ili kuwapa faraja na amani hivyo wasijione wapweke na hakuna yatima na serikali inapenda watoto ndiyo sababu ikaweka elimu bure ili watoto wapate haki ya msingi ya kupata elimu.

"Serikali inawapenda kama isingekuwa kulipiwa hali ingekuwaje watoto hawa ni familia yetu wanahitaji sukari, madaftari na mahitaji mengine na tukiwasaidia tunaweka hazina mbinguni na sisi tutaendelea kuwasaidia,"amesema Shemwelekwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anapongeza wadau waliofanikisha kupatikana kwa misaada hiyo.

Mussa amesema kuwa wamejikita katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu kama ilivyo kwa watoto wanaoishi na familia zao kwani elimu ni haki yao. 

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Faustina Kayombo amesema kuwa Halmashauri ina makao tisa yenye watoto 601 na yote yamesajiliwa kisheria na kwa upande wa mafanikio ni makao kuwa na majengo bora.

Kayombo amesema kuwa changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu ni pamoja na kubakwa, wazazi kupoteza upendo, mahusiano mabaya na wazazi.

Mmiliki wa Kituo cha Shallom Lilian Mbise amewashukuru watumishi na wadau hao kujitolea misaada hiyo kwa vituo vyao kwani vitadaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mahitaji ya shule, magodoro, madaftari, kalamu, penseli, vichongeo, rula, mafuta ya kujipaka, mafuta ya watu wenye ualbino.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Halmashauri, wazee maarufu, viongozi wa dini, makundi mbalimbali yanayomuunga mkono Rais, vikundi vya sanaa na wananchi.


No comments:

Post a Comment