Thursday, July 25, 2024

WANAOZUSHA UZUSHI WATOTO KUTEKWA KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

KUFUATIA watu wanne kukamatwa kwa tuhuma za kuzusha uzushi kuwa kuna gari aina ya Noah linateka watoto mkoa huo umetoa onyo kwa watu wanaoleta taharuki hizo kuwa hawatavumiliwa.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa kuadhimisha Kumbukumbu ya Mashujaa kimkoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo.

Kunenge alisema kuwa baadhi ya watu ambao hawana uzalendo wamekuwa wakizua taharuki na kuwafanya watu washindwe kufanya shughuli zao wakihofia watoto wao kutekwa.

"Suala la utekaji watoto baadhi ya watu wanapotosha na kuketa hofu pamoja na kuzua taharuki na tunatoa onyo kwa wale wanaosababisha hali hiyo hatutasita kuwachukulia hatua kali za kisheria,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa wananchi wakabiliane na vitendo vya ukatili, mauaji ya watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino, unyanyasaji kwa kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo au viashiria.

"Tayari tunawashikilia watu wanne kwa kutoa taarifa za uongo juu ya madai kuwa kuna watoto wametekwa wakati wakijua siyo jambo la kweli hatutasita kuchukua hatua za kisheria kwa watu wa namna hiyo,"alisema Kunenge.

Aidha alisema watu wasishabikie vitendo hivyo kwani wanazua taharuki na mtu kama jambo huna uhakika nalo usisambaze kwani ikiwa ni uongo unaleta uchochezi.

"Jukumu la usalama ni la kila mwananchi tumieni polisi kata, polisi jamii, kamati za usalama za vijiji na jeshi la akiba na sisi tumejipanga yaani ukirekodi uongo tutakukamata kwani hutaweza kujificha,"alisema Kunenge.

Aliongeza kuwa watu wanaoleta mambo hayo siyo wazalendo wa nchi yao kwani matukio ya utekaji baadhi wanayapotosha.

No comments:

Post a Comment