MKOA wa Pwani umepatiwa jumla ya Wauguzi 120 ikiwa ni asilimia 50 ya watumishi walioletwa mkoani humo pia umepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 25 kuboresha huduma za afya.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu Tawala Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Pwani Edina Kataraiya ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel wakati wa Maadhimisho siku ya Uuguzi Duniani kwa Mkoa wa Pwani.
Kataraiya amesema kuwa serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali za huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuongeza wahudumu wa afya ili kuboresha utoaji huduma.
"Kada ya uuguzi ni uti wa mgongo wa huduma za afya ndiyo sababu serikali inaboresha kwani bila ya wauguzi hakuna huduma hizo hivyo toeni huduma kama kiapo chenu kinavyosema upendo, utu na uadilifu,"amesema Kataraiya.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Steven Brown amesema kuwa katika Muundo wa Utumishi wa Kada ya Uuguzi na Ukunga ambacho kinamtaka Ofisa Muuguzi kabla hajafikia Kiwango cha mwisho cha Mshahara wake yaani (TGHSG) awe na Masters ambacho ni kikwazo kwa wauguzi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio amesema kuwa huduma wanayotoa wauguzi ni ibada na Hospitali ni madhabahu hivyo waendelee kudumisha ibada zao.
No comments:
Post a Comment