Tuesday, July 16, 2024

VIONGOZI WA DINI WAHAMASISHA WANAWAKE KUSHIRIKI CHAGUZI NA KUJIINUA KIUCHUMI





VIONGOZI wa Dini Halmashauri ya Mji Kibaha wamekuja na mkakati wa kuhamasisha ushiriki wanawake na wasichana katika uongozi na haki za kiuchumi.  

Aidha wametakiwa kuwania nafasi za uongozi kwani nao wanauwezo wa kuwa viongozi na haki yao washiriki ili walete maendeleo ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mchungaji James Machage  wa Kanisa la Sabato Visiga wakati wa mafunzo ya Ushiriki wa wanawake na Wasichana katika Uongozi na Haki za Kiuchumi kwa Viongozi wa Dini yaliyofadhiliwa na UN WOMEN.

Mchungaji Machage amesema kuwa licha ya changamoto kubwa ya mila na baadhi ya imani lakini wataendelea kutoa elimu ya ushiriki kwenye uchaguzi na fursa za kiuchumi kwani wanauwezo wa kuwa viongozi.

Amesema kuwa watahakikisha wanasaidia wanawake ili waweze kupata haki zao na kuwatia moyo ili wajue fursa zilizopo kwani uongozi wa nchi unajali wanawake kwa kuwapatia fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo kupitia vikundi.

Naye Julieth Faustine katibu wa Kanisa la Katoliki Pangani amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kujua masuala ya uwiano kila linalofanyika lizingatie haki kwa wote na utendaji wa kazi bila ya kubagua kuwa baadhi ya kazi ni za wanawake na wanaume.

Faustine amesema kuwa kuna baadhi ya mila zinamkandamiza mwanamke ikiwa ni pamoja na ukeketaji kwa watoto wa kike, kunyimwa elimu, kunyimwa urithi wa ardhi na kutothaminiwa jambo ambalo atalipigia kelele ili jamii iachane na mila hizo.

Kwa upande wake Abdala Ngulengule amesema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea chachu ya kwenda kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mweishoni mwa mwaka huu.

Ngulengule amesema kuwa mfano kwenye Kata ya Pangani kuna mitaa nane lakini yote ilikuwa ikiongozwa na wanaume hivyo wanatarajia kuwa na mabadiliko makubwa kwenye uchaguzi huo kwani wanawake wengi wamehamasika kushiriki uchaguzi huo ili wapatikaneviongozi wanawake angalau wawili au watatu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Kibaha Leah Lwanji amesema kuwa  wanaendelea kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kuingia kwenye vyombo vya maamuzi na kuwa na usawa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ili waweze kujiinua kiuchumi na kupata fursa zilizopo ndani ya jamii.

Lwanji amesema kuwa Halamshauri inachokifanya ni kuwandaa wanawake kuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi kwa kuanzisha vikundi na kuwaunganisha katika taasisi za kifedha ambazo hutoa fursa za mikopo, mitaji, mafunzo  na masoko.

“Wanawake wengi wanakuwa na unyonge hivyo kushindwa kujiamini hivyo kupitia mradi huu tunawajengea uwezo kwani wakiwa na uwezo wa kiuchumi watakuwa na uwezo wa kujiamini na kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi za uongozi ndani ya jamii,”amesema Lwanji.

Naye mratibu wa mradi wa (WLER) Maria Nkangali amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa viongozi hao wa dini ili wakatoe elimu juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi kuleta maendeleo kwa wananchi.

Nkangali amesema kuwa wanatoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ili yatambue mchango wa wanawake na wasichana kwenye suala la maendeleo bila ya kujali jinsi. 

Mafunzo hayo siku moja yamewahusisha Viongozi wa Dini kwenye Kata mbalimbali na wataalamu wa idara mbalimbali za Halmashauri hiyo.  


No comments:

Post a Comment