Na John Gagarini,
Chalinze
KATIKA kutekeleza
mpango wa Matokeo ya haraka (BRN) Wizara ya Afya imesema kuwa iko katika maongeza
na wafadhili kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kwa ajili ya
kutibu magonjwa mbalimbali badala ya kutegemea kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Asilimia 80 ya dawa zinaotumika
zinaagizwa toka nje ya nchi na kuifanya nchi kutumia gharama kubwa kwa ajili ya
kuagiza dawa hizo ambapo endapo kutakuwa na viwanda vingi kutasaidia kupunguza
gharama.
Hayo yalisemwa na
katibu mkuu wa Wizara ya Afya Donan Mmbando, kwenye Kijiji cha Msoga
alipotembelea ujenzi wa kituo cha afya cha kijiji hicho na kusema kuwa dawa
bado ni changamoto kubwa.
“Mpango huu kama
ulivyo kwenye sekta nyingine utatupima kwa kipindi cha miaka mitatu kutuona je
temeweza kufikia malengo ambapo kati ya malengo hayo ni kuhakikisha upatikanaji
wa dawa, upatikanaji wa vifaa tiba na mambo mengine,” alisema Mmbando.
Alisema BRN
itafanikiwa endapo kutakuwa hakuna tatizo la upatikanaji wa dawa pamoja na
vifaa tiba ambavyo vimeonekana kuwa ni changamoto kubwa.
“Mbali ya changamoto
ya upatikanaji wa dawa pia kuna baadhi ya watumishi wanaojihusisha na wizi wa
dawa hawa sasa tutawakamata na kuwatangaza kwenye vyombo vya habari,” alisema
Mmbando.
Kwa upande wake Mbunge
wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ujenzi wa Kituo hicho cha
afya ambacho ni cha kisasa ni ukombozi kwa watu wa Jimbo hilo ambao hutegemea
kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali ya Tumbi.
Ridhiwani alisema kuwa
pia majeruhi wa ajali ambao walikuwa wakipelekwa Tumbi sasa watapata huduma
hapo ambapo wanatarajia kituo hicho kufunguliwa mwezi Machi mwakani.
Naye diwani wa kata ya
Msoga Hussein Mzimba alisema kuwa kituo hicho kinajengwa kwa nguvu ya wananchi,
serikali pamoja na wadau wa maendeleo wa kata na wilaya hiyo.
Mwisho.
19,Des
Na
John Gagarinii, Chalinze
KITUO
cha Afya cha Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kinakabiliwa na ukosefu wa
gari la kubebea wagonjwa kwa kipindi cha miezi mine jambo ambalo linasababisha
wagonjwa kukodisha magari kwa ajili ya kupelekwa kwenye hospitali kubwa ikiwemo
ya Tumbi.
Hayo
yalisemwa na Mganga mkuu mfawidhi wa kituo hicho, Dk Victor Bamba wakati wa
ziara ya mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete alipotembelea kituo
hicho na kuangalia changamoto zinazoikabili sekta ya afya.
“Changamoto
hii imetokana na imetokana na gari la wagonjwa lililopo kuwa kwenye matengenezo
kwa muda wote huo,” alisema Dk Bamba.
Kwa
upande wake Ridhiwani alisema kuwa tayari kuna mkakati wa kuhakikisha
kunakuwepo na magari ya kubebea wagonjwa matatu mkakati utakaotekelezwa mapema
mwaka ujao.
“Magari
hayo yatagawiwa katika kituo cha afya Chalinze, Miono na kituo cha afya Msoga
ambacho kinatarajia kukamilika hivi karibuni,” alisema Ridhiwani.
Kituo
cha afya Chalinze kinakabiliwa na changamotombalimbali ikiwa ni pamoja na uhaba
wa madawa, chumba cha kuhifadhia maiti, vifaa vya kujifungulia mama wajawazito
ambapo kwa miezi 12 sasa havijasambazwa katika kituo hicho.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
IMEELEZWA kuwa ajali
kwa sasa zinaonekana kama ugonjwa usioambukiza ambao unaua watu wengi kwa sasa
hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana
mjini Kibaha na mkurugenzi wa Elimu Mafunzo na Uenezi wa kamati ya usalama
Barabarani Taifa Henry Bantu, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani
mkoani Pwani.
Alisema kuwa ajali kwa
sasa zinaelekea kuwa ugonjwa unaoua kuliko magonjwa mengine kwani mwelekeo
ndiyo unaoonekana.
“Endapo jitihada za
kuzuia ajali hazitafanyika ajali ndiyo zitakuwa ni ugonjwa usioambukiza unaoua
watu wengi nchini kwa sasa lakini hata hivyo baraza linajitahidi kuhakikisha
ajali zinapungua,” alisema Bantu.
Bantu alisema kuwa
madereva wanapaswa kuwa makini katika uendeshaji wa magari ili kupunguza ajali
zisizo za lazima.
“Ajali nyingi siyo
bahati mbaya kama wanavyosema watu bali ajali zinatokana na uzembe na si mpango
wa Mungu hivyo umakini unatakiwa kuwepo,” alisema Bantu.
Awali akisoma risala
ya kamati ya usalama barabarani mkoa Shaban Nkindwa alisema kuwa katika kipindi
cha Januari Mosi hadi Novemba 30 jumla ya watu 556 walifariki dunia.
Nkindwa alisema kuwa
ajali kwa jumla zilikuwa 1,859 za vifo zilikuwa 424 huku zilizojeruhi zikiwa
1,126 na watu waliojeruhiwa walikuwa 2,601.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limekusanya kiasi cha
zaidi ya shilingi bilioni mbili kutokana na makosa madogo madogo ya usalama
barabarani yaliyotokea kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu.
Akisoma risala ya kamati ya usalama barabarani mkoa
wa Pwani, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani zilizofanyika jana
mjini Kibaha, Shaban Nkwinda alisema kuwa fedha hizo zilitokana na makosa
yaliyotokana na makosa yaliyofanywa na madereva.
Nkwinda alisema kuwa makosa yaliyokamatwa yalikuwa
80,786 ambapo ni ongezeko la ajali 23,839 sawa na asilimia 41.8 ikilinganishwa
na mwaka jana.
“Makosa yaliyolipiwa yalikuwa 80,259 ikiwa ni
ongezeko la ajali 24,293 sawa na asilimia 43.4 ikilinganishwa na mwaka jana,”
alisema Nkwinda.
Alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana mkoa
uliweza kukusanya kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni moja kutokana na makosa
56,946 kutokana na makosa yaliyolipiwa na 55,966.
Mwisho.