Wednesday, November 11, 2026

MRADI KUWAWEZESHA WASICHANA WANAWAKE VIJANA KIBAHA WAZINDULIWA

MAKUNDI ya wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 katika Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na mradi wa mwaka mmoja wa uwezeshaji kiuchumi unaolenga kukuza ajira, kujitambua na tija kwa jamii.

Mradi huo  ujulikanao kama ' Girls Round Table- Season 12',  utatekelezwa kwa pamoja na  shirka lisilo la lissrikali la  Nuruyetu Foundation na Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo ya mradi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi katika Shule ya Msingi Sofu, Manispaa ya Kibaha hivi karibuni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Sofu, Bi Aloysia Nyeto, alisema mradi huo unatarajiwa kubadilisha maisha ya wasichana na wanawake vijana ambao wamepoteza mwelekeo wa maisha, huku pia ukijenga uwezo wa jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Mradi huu utawafikia wasichana wetu na mabinti zetu, wengi wao waliokosa fursa za kufikia ndoto zao. Sambamba na hilo, jamii ambazo walengwa hawa wanatoka pia zitanufaika kwa namna moja ama nyingine kupitia programu za mradi huu. Tunashukuru sana Serikali kwa kutoa vibali kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kufanya kazi na makundi mbalimbali ya watu katika maeneo yetu, na hii inaonesha dhahiri dhana ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2050,” alisema.

Aliongeza kuwa, kupitia uwezeshaji wa kiuwezo na mtaji utakaotolewa kupitia mradi huo kwa walengwa hao, jamii katika maeneo husika zitajifunza umuhimu wa kuyajali makundi ya wanawake na wasichana kwa faida ya familia na jamii nzima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa  Nuruyetu Foundation, Bi Zauja Mohamed, alisema wanawake vijana na wasichana kutoka maeneo ya Picha ya Ndege, Kwamfipa, Visiga na Sofu watanufaika katika awamu ya kwanza ya mradi huo, ambao unafadhiliwa kwa pamoja na Global Affairs Canada na Cuso International.

Akifafanua mradi huo, alisema walengwa watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa kidijitali na fedha, utengenezaji wa kazi za mikono na ujuzi wa ujasiriamali.

“Tutaendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa walengwa wa mradi huu kadri muda unavyokwenda. Lengo ni kuwawezesha kunufaika kulingana na uwezo wao wa kutumia ujuzi watakaoujifunza,” alisema.

Aliongeza kuwa mwishoni mwa mradi, walengwa watapewa vifaa vya kuanzishia biashara ili kuanzisha biashara zao wenyewe.

Alisema shirika hilo pia litaunga mkono Serikali katika kuimarisha masomo ya ufundi stadi kwa wasichana katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, kama sehemu ya mradi huo.

Wakizungumza kwa niaba ya walengwa wengine, Olpa George wa Visiga na Rahma Hatibu wa Picha ya Ndege wote walionyesha matarajio makubwa ya mafanikio watakayoyapata kupitia mradi huo.


WANANCHI wametakiwa kuacha kuharibu noti kwani endapo wakikutwa na hatia adhabu yake ni faini ya shilingi 500,000 kwa noti moja au kifungo cha mwaka mmoja jela.

Aidha alisema kuwa kwa mtu atakayebainika kutengeneza noti bandia akibainika kifungo chake ni cha maisha jela na vifaa vyote vilivyotumika kuzitengeneza vitataifishwa.

Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Ofisa kutoka Kurugenzi ya usimamizi wa Sarafu kutoka Benki Kuu (BoT) Shedrack Mapunda alipokuwa akielezea kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa noti wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari juu ya uchumi na fedha.

Mapunda alisema kuwa baadhi ya watu hawafahamu sheria za fedha kuwa haziruhusu uharibifu wa sarafu kwani hilo ni kosa kisheria na adhabu zipo.

"Endapo utabainika umeharibu noti utachukuliwa hatua za kisheria na ukibainika utafikishwa mahakamani kwani ukikutwa na hatia kila noti moja iliyoharibiwa adhabu yake ni 500,000 au jela mwaka mmoja,"alisema Mapunda.  

Alisema kwa mtu ambaye atakutwa na hatia kwa ya kukutwa na noti bandia sheria inambana na anaweza kufungwa kifungo cha miaka saba jela hivyo umakini unahitajika.

"Wananchi wanapaswa kutoharibu noti kwani sheria zipo lakini kwa sasa wamejikita kutoa elimu zaidi lakini baadaye wataanza kutumia sheria hizo ili kudhibiti wale wanaoharibu noti na unapokutwa ba noti bandia huwezi kusema hukufahamu .

Alisema kuwa wananchi anapaswa kutunza noti na kutoharibu kwani hilo ni kosa kisheria kwani kuna baadhi wanazikanyaga au kuzikata au kutumia kwa njia ambayo siyo sahihi.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano BoT Noves Moses alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia noti kutengeneza mataji wakati wa sherehe.

Moses alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitengeneza kadi kwa noti jambo ambalo ni kinyume cha sheria hivyo jamii inapaswa kupewa elimu juu ya matumizi mabaya noti kwani nikosa kisheria.

Friday, November 6, 2026

WATATU WAFA BAADA YA BOTI KUZAMA MTO RUFIJI

WATU watatu wamefariki dunia na wengine wawili hawajulikani walipo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama baada ya kugonga gogo kwenye Mto Rufiji.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Protas Mutayoba amesema kuwa ajali hiyo ilitokea Novemba 4 majira ya saa 12 jioni katika eneo la Kijiji cha Mloka Kata ya Mwaseni.

Mutayoba amesema kuwa boti hiyo mali ya Kijiji cha Mloka ilikuwa ikiendeshwa na Nassoro Mkandu (32) mkazi wa Mloka ikiwa na watu 23 waliokuwa wakitoka mashambani kuelekea Kijijini kupitia Mto Rufiji ambapo boti hiyo ilikuwa imebeba watu 23 ambapo watu 18 waliokolewa.

Mutayoba amewataja waliofariki kuwa ni Sikitiko Naimbu zaidi ya miaka (60) Shushani Kitimai (2) na Masha Buriani (17) wakazi wa Mloka huku Faimu Kitimai (6) pamoja na Nusra Makuka (28) ambao hawajulikani walipo.

"Kati ya watu 18 waliookolewa watatu ni wanaume na 15 wanawake ambao wanaendelea na matibabu katika Zahanati ya Mloka ambao watu wawili bado hawajapatikana,"amesema Mutayoba.      

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Luteni Kanali Fredrick Komba amesema kuwa ajali hiyo imeacha simanzi kwa wananchi huku shughuli za uokoaji zikiendelea na ufatiliaji katika Mto Rufiji.

MFANYAKAZI KITUO CHA MAFUTA AFA KWA KUSHAMBULIWA NA WATU WASIYO FAHAMIKA

MFANYAKAZI wa kituo cha kuuza mafuta cha Oryx Jimmy Lema (29) amepoteza maisha baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake na watu wasiofahamika ambao walikimbia mara baada ya tukio hilo.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Salim Morcase tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:15 usiku Novemba 5 mwaka huu 2026 kwenye kituo cha kuuzia mafuta cha ORYX kilichopo eneo la Kibosha Kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo. 

Morcase amesema kuwa marehemu akiwa kazini zamu ya usiku pamoja mwenzake Junior Jonh katika kituo hicho cha kuuzia mafuta alikutwa na umauti baada ya kushambuliwa na watu hao ambao hawakuweza kufahamika.

"Baada ya kupungua kwa wateja majira ya saa 8:30 usiku marehemu alienda kujipumzisha katika moja ya vyumba vilivyopo kwenye kituo hicho lakini ghafla akiwa ndani ya chumba hicho alivamiwa na watu wasiofahamika,"amesema Mircase.

Amesema kuwa watu hao waliiingia ndani majira ya saa 9:00 usiku na kumshambulia na kitu cha ncha kali na kusababisha kifo chake.

"Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeanza msako mkali wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,"amesema Morcase.

MAMA MKUBWA NA WENZAKE WAWILI WASHIKILIWA TUHUMA KIFO CHA MTOTO BAADA YA KUMNYWESHA WANZUKI

WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani akiwemo mama mkubwa wa mtoto mwenye umri wa miaka (3)  kwa tuhuma za kumpa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki na kusababisha kifo.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha.

Morcase amesema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 30 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi Kijiji cha Kwaruhombo Kata ya Mbwewe Wilaya ya Kipolisi Chalinze ambapo mtoto huyo akiwa na wenzake wawili walinyweshwa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki wakiwa nyumbani kwao na mama yao mkubwa aitwaye Bahati Shabani (32).

"Mara baada ya kunywa pombe hiyo mtoto Mustapha Mubaraka alizidiwa na kukimbizwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kwaruhombo
kutokana na hali yake kutokuwa nzuri mtoto huyo, alihamishiwa kutoka Zahanati ya Kwaruhombo,"amesema Morcase.

Amesema kuwa mtoto huyo alihamishiwa katika Hospitali ya Msoga kwa matibabu zaidi ambapo alifariki tarehe Oktoba 31 mwaka huu akiwa anaendelea na matibau katika Hospitali hiyo.

"Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Bahati Shabani (32) mama mkubwa wa mtoto huyo na Rehema Gabriel (37) na Elizabeth Dibison (35) wote wa kazi wa Kijiji cha Kwaruhombo Kata ya Mbwewe ambao ni wauzaji wa pombe hiyo ili kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha mtoto huyo iwapo yalitokana na kunyweshwa pombe hiyo,"amesema Morcase.

MAMA WAKAMBO ASHIKILIWA TUHUMA KIFO CHA MTOTO

JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Irene Machumu (32) mama wa kambo kwa tuhuma za kumuua mtoto mwenye umri wa miaka (5) akidai amechezea maji yaliyokuwa yamewekwa kwenye beseni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Salim Morcase amesema kuwa tukio hilo limetokea huko Mtaa wa Msumbiji Wilaya ya Kisarawe Novemba 2 mwaka huu majira ya mchana.

Morcase amesema kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na baba yake na mama yake huyo wa kambo pamoja na pacha wa marehemu.

"Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kumwadhibu mtoto huyo kwa fimbo akimtuhumu kuchezea maji yaliyokuwa kwenye beseni akiwa yeye na pacha wake,"amesema Morcase.

Amesema kuwa kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Machumu kwa mahojiano huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.

"Tunachunguza tukio hili ili kuweza kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha mtoto huyo pamoja na chanzo cha kifo chake,"amesema Morcase.

Aidha amesema kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi wa tukio hili kukamilika wa tukio hilo.


Thursday, November 5, 2026

MALI ZA SEKTA YA FEDHA ZAFIKIA TRILIONI 10.9

SEKTA ya fedha nchini inaendelea kukua ambapo hadi kufikia Desemba mwaka 2025 jumla ya mali za mfumo wa fedha zimefikia takribani trilioni 10.9.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkaguzi Mwandamizi wa Benki kutoka BoT Joel Charles wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya utendaji kazi wa Benki Kuu.

Charles amesema kuwa Benki Kuu ndiyo msimamizi wa taasisi za fedha na imekuwa ikihakikisha wateja wanalindwa.

"Sekta ya kibenki imewekeza asilimia 70 mifuko ya hifadhi ya jamii ni asilimia 23.6 mifuko ya uwekezaji wa pamoja asilimia nne na sekta ya bima ni asilimia 2.4,"amesema Charles.