Wednesday, August 27, 2025

GRACE JUNGULU ARUDISHA FOMU UDIWANI KATA YA PICHA YA NDEGE

DIWANI Mteule kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Picha ya Ndege Grace Jungulu amerudisha fomu ya udiwani na kuwataka wana CCM kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba mwaka huu.

Jungulu amerudisha fomu kwenye ofisi ya Kata ya Picha ya Ndege Manispaa ya Kibaha huku akisindikizwa na wanachama na wananchi wa Kata hiyo.

Amewataka wanaccm na wananchi kwa ujumla kuhakikisha Oktoba wabakipigia kura za kishindo chama ili kiendelee kuongoza serikali.


KOKA ACHUKUA FOMU UBUNGE KIBAHA MJINI

MBUNGE Mteule wa Jimbo la Kibaha Mjinj kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Silvestry Koka amewataka wale waliowania nafasi hiyo na kura hazikutosha washirikiane ili chama kipate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Koka aliyasema hayo mjini Kibaha wakati akichukua fomu kuwania nafasi hiyo kupitia CCM na kuwa ni wakati wa kuungana ili kuleta ushindi wa chama.

Alisema kuwa kama kulitokea kutofautiana kwa namna moja au nyingine ni kusameheana na kuungana wakati wa kutafuta kura za chama.

"Huu ni wakati wa kuungana na kuondoa tofauti ambazo zilijitokeza wakati wa ndani ya chama ambapo kila mmoja alikuwa akitafuta namna ya kushinda,"alisema Koka.

Alisema kuwa kilichoshinda ni hivyo kusiwe na kuona kuwa fulani kashinda wote ni wana ccm hawapaswi kutofautiana wote wanakipambania chama.

"Tuungane ili kuhakikisha tunakipatia ushindi chama kuanzia Urais, Ubunge na Udiwani tunataka ushindi uwe mkubwa na wakishindo na kuweka historia,"alisema Koka.

Aidha alisema kuwa wanaccm wahakikishe ushindi wa asilimia 100 kama ilivyokuwa kuwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kwenye kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

Kwa upande wake Alhaji Mussa Mansour ambaye alikuwa moja ya wagombea wa nafasi hiyo alisema kuwa uchaguzi ndani ya chama umekwisha kinachofuata ni kuzitafuta kura za CCM.

Naye mgombea wa nafasi hiyo Abubakar Allawi alisema kuwa baada ya uchaguzi ndani ya chama kwisha watashirikiana na mgombea huyo kuhakikisha anashinda na nafasi nyingine za Urais na Udiwani ili chama kiendelee  kushika dola.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Hawa Mchafu alisema kuwa anawapongeza wawania nafasi ya ubunge hao kwa kuonyesha ushirikiano na kukipa urahisi chama kupata ushindi itakapofika Oktoba.

mwisho.

Thursday, June 26, 2025

DMI MISSION TANZANIA KUKABILI MIMBA NDOA ZA UTOTONI









SERIKALI imesema kuwa elimu ni nguzo ya kuwalinda watoto na ukatili ndoa na mimba za utotoni na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza haki ya msingi ya mtoto kupata elimu.

Hayo yamesemwa na Madina Mussa ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika iliyoandaliwa na DMI Mission Tanzania.

Mussa amesema kuwa ili kutekeleza mazingira rafiki kwa watoto waweze kupata haki hiyo ya msingi imejenga miundombinu mizuri ya watoto kujisomea.

"Katika kukabiliana na ukatili na ndoa za utotoni wazazi na walezi lazima washirikiane na serikali kuhakikisha haki za msingi za mtoto zinalindwa ikiwa ni pamoja na elimu, kumlinda na ukatili na kuishi katika mazingira mazuri kwani haki za mtoto zinaanzia nyumbani,"amesema Madina.

Awali Mkurugenzi wa DMI Mission Tanzania Sister Fathima Jacintha Ran amesema kuwa dhima ya siku hiyo ni Kupanga bajeti na kuweka bajeti kwa haki za watoto.

Ran amesema kuwa lengo ni kuhakikisha ustawi, elimu, na hatma njema za watoto ikiwa ni kukumbusha wajibu wa pamoja kuhakikisha watoto wa Afrika wanapata haki za msingi za elimu bora, huduma za afya, ulinzi na fursa ya kukua.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha watoto Halmashauri ya Mji Kibaha Hanifa Mruma amesema kuwa mradi ulioanzishwa na shirika hilo wa kupambana na mimba za utotoni ni mzuri na utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake moja ya wanufaika kwenye mradi huo wa Klabu za Wanawake Vijana Chiku Hamis amesema kuwa wanalishukuru shirika hilo kwa kuwapatia vifaa kwa ajili ya kutengeneza batiki na sabuni kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji vitu hivyo. 

Mradi huo wa kupunguza mimba za utotoni unatekelezwa kwenye Kata tatu za Pangani, Tumbi na Kongowe.

Wednesday, June 25, 2025

MATUMLA PROMOTION KUINUA VIPAJI VYA NGUMI KIBAHA

MATUMLA Promotion ya Kibaha imeandaa pambano la ngumi kati ya Abdully Said au Dully Bwengo na Rashid Hassan au Makali litakalopigwa kwenye baa ya UEFA Kongowe Kibaha Juni 28 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na pambano hilo ambalo litasindikizwa na mapambano mengine matano Mkurugenzi wa Matumla Promotion Abuu Matumla amesema kuwa maandalizi ya awali yamekamilika.

Matumla amesema kuwa maandalizi yakiwemo ya kuwalipa fedha za awali yameshafanyika na mabondia hao watakamilishiwa fedha zao baada ya pambano hilo kukamilika.

"Taratibu za awali zimekamilika ikiwa ni pamoja na malipo ya awali kwa mabondia, vibali na ulinzi vyote viko tayari kinachosubiriwa ni siku ya pambano hilo,"amesema Matumla.

Alisema kuwa malengo ya kuandaa mapambano hayo ni kuhamasisha mchezo huo kwa vijana wa Kibaha kwani mchezo huo ni ajira na kujenga afya bora na kuwaondoa vijana kwenye vitendo hatarishi.

"Tunataka tuinue mchezo wa ngumi Kibaha ambapo pia kutakuwa na pambano la wanawake ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wanawake nao washiriki mchezo huo kwani hata wao wanauwezo wa kushiriki mchezo huo,"amesema Matumla.

Aidha alisema kuwa mbali ya mapambano hayo pia kutakuwa na burudani za muziki zikiongozwa na mkali wa Singeli Yuda Msaliti na waimbaji wengine wakali wa miondoko hiyo ya singeli.

"Nawaomba wapenzi wa mchezo wa ngumi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya vijana wao ili kuwapa hamasa wapende mchezo huo ambao umekuwa ukipendwa na wengi,"amesema Matumla.

Thursday, June 19, 2025

DIWANI KATA YA MBWAWA JUDITH MLUGE AELEZA MAFANIKIO YA MIAKA 5

KATA ya Mbwawa Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani imeweza kufungua barabara 35 kwenye kata kupitia fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi milioni 10 zilizotolewa kwenye kila kata.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano Diwani aliyemaliza muda wake wa Kata hiyo Judith Mluge amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano maendeleo makubwa yamepatikana.

Mluge amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji ambayo haikuwepo ikiwa ni asilimia 80, umeme unapatikana kwa asilimia 80 hadi 100.

"Kuhusu suala la afya kwenye zahanati za Kata hiyo kwa sasa dawa zinapatikana kwa asilimia 90 na ukarabati wa jengo la mama wajawazito liko mbioni kukamilika,"amesema Mluge.

Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto za mimba kwa wasichana wanaendelea na ujenzi wa bweni kwenye shule ya sekondari ya Mbwawa.

"Katika kipindi hicho tumefanikiwa kujenga ofisi ya kata pia nimekinunulia chama kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na Mungu akipenda ujenzi utaanza mwakani,"amesema Mluge.

Amesema kuwa kwa upande wa mikopo asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri fedha zilitolewa lakini baadhi wameshindwa kurejesha mikopo kiasi cha shilingi milioni 88.

"Changamoto tuliyoipata ni baadhi ya wakazi wanaokaa ngambo ya mto Ruvu ambapo tulitaka kujenga daraja lakini Mto huo umekuwa ukibadili mwelekeo,"amesema Mluge.

Ameongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.

Sunday, June 15, 2025

RIDHIWANI KIKWETE AKISHIRIKI MAADHIMISHO UELEWA KUHUSU ALBINO

Nimeshiriki shughuli za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa Kuhusu Albino.

Shughuli hii iliongozwa na Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa , Waziri Mkuu wa JMT , zilizofanyika katika viwanja wa Mwanga Mkoani Kigoma tarehe 13 Juni 2025.

Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka na utumika kukumbushana umuhimu wa kushirikisha wenye Ualbino, Haki zao, umuhimu wa serikali kuendelea kuangalia maslahi na ulinzi wao.  

Katika Shughuli ya Mwaka huu mtandao maalum wa kusajiri watu wenye Ulemavu unaowezesha usajiri kwa njia ya Elektronik hata kwenye maeneo yaliyo nje ya mtandao nao ulizinduliwa. 

Mfumo huo unawezesha taarifa za watu wenye ulemavu kuchukuliwa na kuchambuliwa ambapo zitaiwezesha serikali kupata taarifa za kina zitakazowezesha kupanga mipango ya maendeleo ikiwemo kuwashirikisha wenye Ulemavu.  


Waziri Mkuu wa JMT alitumia nafasi hiyo pia kutoa maagizo mahsusi kwa wakuu wa Mikoa na wadau waliokuwapo kuhusu matumizi sahihi ya mtandao huo na kuwashirikisha watu wenye Ulemavu kwa jumla katika shughuli mbalimbali ikiwemo Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadae Mwezi Oktoba mwaka huu uku akiwahamasisha watu wenye Ualbino nao kujitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Friday, June 13, 2025

SUBIRA MGALU ATOA GARI KWA (UWT) BAGAMOYO

MBUNGE wa Mkoa wa Pwani Subira Mgalu ameupatia gari uongozi wa Jumuiya ya Wanawake CCM kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo aina ya Noah Mgalu amesema kuwa moja ya nadhiri aliyojiwekea kipindi cha nyuma ilikuwa ni kuhakikisha anainunulia chombo cha usafiri Jumuiya hiyo ili kurahisisha utendaji kazi.

Mgalu amesema kuwa ni vyema gari hilo likatumika kutafuta kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan huko kwenye matawi kwa kuwakumbusha wananchi kile kilichofanyika kwenye maeneo yao.

"Gari hili likatumiwe na Jumuiya zote za chama ikiwemo Wazazi na Vijana ili ziweze kufanikisha malengo ya chama chetu,"amesema Mgalu.

Akikabidhi gari hilo kwa Katibu wa  Wilaya ya Bagamoyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mery Chatanda amempongeza  Mbunge huyo kwa jinsi ambavyo amekuwa akijitoa kwa Jumuiya hiyo.

Chatanda amewataka viongozi wa Bagamoyo kuhakikisha wanaitumia gari hiyo kwa makusudio yaliyokusudiwa ili kurahisisha shughuli za utendaji wa Jumuiya