Thursday, June 19, 2025

DIWANI KATA YA MBWAWA JUDITH MLUGE AELEZA MAFANIKIO YA MIAKA 5

KATA ya Mbwawa Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani imeweza kufungua barabara 35 kwenye kata kupitia fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi milioni 10 zilizotolewa kwenye kila kata.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano Diwani aliyemaliza muda wake wa Kata hiyo Judith Mluge amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano maendeleo makubwa yamepatikana.

Mluge amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji ambayo haikuwepo ikiwa ni asilimia 80, umeme unapatikana kwa asilimia 80 hadi 100.

"Kuhusu suala la afya kwenye zahanati za Kata hiyo kwa sasa dawa zinapatikana kwa asilimia 90 na ukarabati wa jengo la mama wajawazito liko mbioni kukamilika,"amesema Mluge.

Aidha amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto za mimba kwa wasichana wanaendelea na ujenzi wa bweni kwenye shule ya sekondari ya Mbwawa.

"Katika kipindi hicho tumefanikiwa kujenga ofisi ya kata pia nimekinunulia chama kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na Mungu akipenda ujenzi utaanza mwakani,"amesema Mluge.

Amesema kuwa kwa upande wa mikopo asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri fedha zilitolewa lakini baadhi wameshindwa kurejesha mikopo kiasi cha shilingi milioni 88.

"Changamoto tuliyoipata ni baadhi ya wakazi wanaokaa ngambo ya mto Ruvu ambapo tulitaka kujenga daraja lakini Mto huo umekuwa ukibadili mwelekeo,"amesema Mluge.

Ameongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.

No comments:

Post a Comment